Moshi. Watu wawili wamefariki dunia katika matukio mawili tofauti baada ya kuzama kwenye mito ya Kifaru na Mamba, mkoani Kilimanjaro wakati wakijaribu kuvuka pembezoni mwa mito hiyo.
Waliofariki ni mkazi wa Kata ya Kaloleni Manispaa ya Moshi, Asha Chamtanda (47) na mkazi wa Kijiji cha Gonjanza, Wilaya ya Same, Mkwavi Vicent Mapombe (31).
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, mkoani Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi amethibitisha kutokea kwa matukio hayo ambayo amesema yametokea Oktoba 6, mwaka huu.
Aidha, Kamanda Mkomagi amesema, mwili wa Chamtanda uliopolewa jana Oktoba 6,2025 baada ya kuzama katika mto Mamba na ulikabidhiwa kwa familia kwa ajili ya taratibu za maziko.
“Baada ya kupata taarifa, askari wetu walifika katika eneo la tukio na kubaini kuzama maji kwa mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Asha Chamtanda ambaye alizama katika mto Mamba,”amesema Kamanda Mkomagi.

Mwili wa mkazi wa kata ya Kaloleni, Asha Chamtanda(47) ukiwa umebebwa baada ya kuopolewa mto Mamba.
Amesema, “Askari walianza juhudi za kutafuta mwili wa mtu huyo na kufanikiwa kuuopoa na kukabidhi kwa Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi ambapo baadaye ulikabidhiwa kwa familia.”
Amesema chanzo cha tukio hilo, ni kwamba mwanamke huyo alikuwa akipita pembezoni mwa mto huo bila kuchukua tahadhari iliyopelekea kuteleza na kutumbukia.
Kuhusu mwili wa Mapombe, amesema umeopolewa leo Oktoba 7, 2025 baada ya kutafutwa tangu jana Oktoba 6 katika mto Kifaru bila mafanikio.
“Niwaombe wananchi mnapopita pembezoni mwa vyanzo vya maji kama mito, mabwawa, maziwa mchukue tahadhari muda wote,”amesema Kamanda Mkomagi