Taarifa mpya zikufikie kwamba kuna kocha huko kwao keshaaga kwa mabosi wake kwamba anakuja kupiga mzigo Tanzania, lakini hapa nchini mabosi pale Jangwani inadaiwa kwamba wamezungumza naye na kila kitu kipo freshi.
Ujio wa Romuald Rakotondrabe maarufu kama Roro umechagizwa zaidi na bosi mmoja wa idara ya ufundi kutoka Shirikisho la Soka Madagascar aliyesema kocha wao huyo ataondoka na anakuja Tanzania.
“Roro ametuambia anaondoka hapa kwetu na ametuambia anakuja huko Tanzania. Tulitaka kumbakisha lakini naona amesisitiza sana amepata ofa nzuri na klabu kubwa,” amesema bosi huyo.
“Huyu ni kocha wa kisasa sana anafundisha soka zuri. Kwa muda aliokaa hapa kwetu ametuboreshea viwango vya wachezaji.”

Yanga inalazimika kuachana na Folz kutokana na presha iliyopo nje ya uongozi kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo ambao hawakubaliani na soka la kocha huyo Mfaransa licha ya kutopoteza mechi yoyote ya mashindano msimu huu kati ya tano ilizocheza. Yanga katika mechi hizo imeshinda nne na sare moja.
Kwa sasa hesabu kubwa sana zinapigwa pale Yanga, huku mabosi wa juu wakiwa wamekamilisha mchakato wa kocha mpya na wakikubaliana tu kumuondoa Folz, basi mwamba huyo anatua fasta. Mpaka leo mabosi wa juu wa Yanga walishamalizana na Roro.
Rakotondrabe maarufu kwa jina la ‘Roro’ sio jina geni kwani alikuwa hapa nchini kwani wakati wa Fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN 2024) aliiongoza Madagascar kumaliza nafasi ya pili baada ya kupoteza mechi ya fainali kwa mabao 3-2 dhidi ya Morocco.

Yanga imevutiwa na ubora wa Roro na yeye akavutiwa na mradi wa klabu hiyo ambapo hatua iliyosalia ni uongozi wa Yanga kumalizana na Folz kisha jamaa atue nchini.
Awali, Yanga ilikuwa inafikiria kumrudisha Sead Ramovic ambaye yupo CR Belouizdad alikotua baada ya kutokea Jangwani, lakini dili hilo lilishindwa kukamilika.
Ilikokwama Yanga ni kwamba bado Ramovic hajamalizana na Waarabu, lakini pia kocha huyo raia wa Ujerumani alitaka kuzungumza na familia yake ambayo awali ilishindwa kukubaliana na maisha ya Tanzania kufuatia kuchelewa kupata nyumba iliyoitaka.
Mwanaspoti linafahamu kwamba Roro ameshaanza kufuatilia mafaili mbalimbali ya mechi za timu hiyo kisha kuwaambia mabosi wa Yanga wapi timu yao inakwama.
Roro (60), aliingia kwenye rada za Simba wakati ikitafuta mrithi wa Fadlu Davids, lakini mambo mawili yakaua dili hilo ikiwemo mshahara alioutaka na namna anavyotaka benchi lake liwe katika kikosi hicho.

Yanga ilianza kuichapa Simba bao 1-0 kwenye Ngao ya Jamii na kutetea taji hilo, kisha ikaitoa Wiliete SC ya Angola hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 5-0, ikaifunga Pamba Jiji mabao 3-0 na matokeo ya 0-0 dhidi ya Mbeya City, hizi zikiwa ni mechi za Ligi Kuu Bara.
Kocha Roro ambaye hajawahi kufundisha timu ya klabu, amekuwa na Madagascar tangu alipoteuliwa kwa mara ya kwanza Mei 30, 2023.
Kocha huyo anamiliki leseni ya Uefa PRO ambayo inakidhi vigezo vya kuiongoza timu yoyote Afrika katika mashindano mbalimbali.