BAADA ya Mtibwa Sugar kucheza mechi mbili za Ligi Kuu Bara ikiwa chini ya kocha Juma Awadhi, uongozi umezungumzia ujio wa Mkenya Yusuf Chipo ambaye ataanza majukumu ligi itakapoendelea kwa kucheza dhidi ya Coastal Union.
Mtibwa Sugar ambayo imerejea Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kushuka 2023-2024, imeanza na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Mashujaa, kisha ikaichapa Fountain Gate mabao 2-0. Mechi ijayo ni Oktoba 19, 2025 nyumbani dhidi ya Coastal Union.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mtibwa Sugar, Swabri Aboubakar, amesema ni mengi yamekuwa yakizungumzwa juu ya Chipo, hivyo anathibitisha huyo ndiye kocha wao mkuu.
Kila kitu kimekamilika na kocha alikuja nchini akasaini mkataba kwa ajili ya kuinoa Mtibwa Sugar, kuna mambo yakaingiliana hapa kati, alipata matatizo ya kifamilia na sisi kama viongozi tulimruhusu aondoke akayatatue.

“Muda wowote kuanzia sasa atarudi na kujiunga na timu kuendelea na kazi yake, tuna imani kubwa na Chipo ni aina ya makocha ambao wana uwezo wa kuendana na mfumo wa timu yetu, hivyo matarajio ni kuiongoza timu kufikia malengo,” amesema
Aboubakar amesema kocha huyo anatarajia kurudi nchini muda wowote kuanzia sana na kabla ya ligi kuendelea, baada ya kusimama kupisha Kalenda ya FIFA atakuwa amejiunga na timu na kuendelea na maandalizi kwa kusaidiana na Awadhi Juma ambaye ndiye anakaimu nafasi ya kocha mkuu.
Mkenya huyo si mgeni Tanzania kwani mara kadhaa amefundisha timu za Ligi Kuu ikiwamo Coastal Union na safari hii anatajwa kuwa na kibarua cha kuirejeshea makali Mtibwa Sugar iliyorejea katika ligi hiyo ikitokea Championship.

Chipo aliyekuwa akiinoa Murang’a Seal ana kazi ya kuibeba Mtibwa ili kurejea mafanikio ya kubeba ubingwa wa ligi baada ya kufanya hivyo 1999 na 2000.
Kocha huyo atasaidiana na Awadh ambaye alishuka na timu hiyo Championship na kuipandisha daraja kwa kubeba ubingwa wa ligi hiyo msimu uliopita.