Babati. Mkazi wa kijiji cha Bermi wilaya ya Babati mkoani Manyara, Hamis Mfangavu (42) amehukumiwa kwenda jela miaka sita na kupigwa faini ya Sh1 milioni baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kujeruhi kwa kumkata masikio mtoto wa jirani yake mwenye umri wa miaka 13, aliyeelezwa alimuibia yai moja la kuku.
Hukumu hiyo imesomwa mbele ya hakimu mkazi Mkoa wa Manyara, Martini Masao, ambapo mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo mjini Babati Agosti 23 mwaka 2025.
Katika kesi hiyo ya mwaka 2025 hukumu yake imetolewa mjini Babati Oktoba 7 mwaka 2025 kwenye Mahakama ya Hakimu mkazi Mkoa wa Manyara.
katika kesi hiyo mshtakiwa huyo ametiwa hatiani kwa kumkata masikio yote mawili kwa kutumia kiwembe, kumchanja kifuani pamoja na kumbamiza kichwa ukutani akidai kuwa mtoto huyo kwa madai ya kumuibia yai.
Imeelezwa mahakamani hapo kuwa mtoto huyo alienda nyumbani kwa Mfangavu na kuiba yai moja la kuku na kukamatwa na kaka wa mshtakiwa.
Ameeleza kwamba Mfangavu alipofika nyumbani hapo alitaka apewe mtoto huyo ili amalizane naye na kisha akamjeruhi maeneo mbalimbali ya mwili.
Awali, hakimu Masao ameiambia mahakama hiyo kuwa kosa hilo ni kinyume na kifungu cha sheria namba 225 cha kanuni za adhabu kwa makosa ya jinai sura ya 16 marejeo 2023.
Kwa upande wake, wakili wa Serikali, Esther Malima ameeleza kwamba kosa hilo limefanyika kwa kiwango kikubwa na lina majeraha zaidi ya moja.
Malima alisema kuwa mtoto huyo amepata majeruhi ya kukatwa masikio na kusababisha ulemavu kwani hayataota tena.
Ameiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa huyo ili iwe funzo kwa watu wengine wenye tabia ya kuchukua sheria mkononi.
Hakimu Masao alipomuuliza mshtakiwa huyo endapo ana chochote cha kujitetea baada ya kutiwa hatiani, mshtakiwa huyo aliijibu kwa kifupi hana cha kujitetea. Ndipo Hakimu Masao akatoa hukumu hiyo kwa mshtakiwa kwenda jela miaka sita na kulipa faini ya Sh1 milioni.
Akizungumza nje ya mahakama baada ya hukumu hiyo, mzazi wa mtoto huyo, Thomas Herman ameridhika na hukumu hiyo kwani kitendo hicho cha kikatili kwa mtoto wake kimemuathiri kisaikolojia.
Amesema hali ya kiafya ya mtoto wake siyo nzuri kwani hakai kwa amani na mwonekano wake ni tofauti na alivyoumbwa na Mungu.