BWANGA KUANZISHWA LIGI YA MPIRA WA MIGUU

Kulia ni mgombea Ubunge Jimbo la Chato Kusini, Paschal Lutandula, na Kushoto ni mgombea Udiwani Kata ya Minkoto, Paulo Mfanisi.

::::::::

Na Mwandishi Wetu – CHATO

KATIKA kile kinachoonekana ni kusaidia ongezekao la ajira kwa vijana nchini, mgombea Ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Chato Kusini, Paschal Lutandula, ameahidi kuanzisha ligi ya mpira wa miguu ili kuchechemua uchumi kwa jamii.

Mbali na hilo, amedai vijana wanapaswa kuwa na uchangamfu wakati wote ikiwa ni pamoja na kuonyesha vipaji vyao katika kuinua, kukuza na kuendeleza uchumi wa kila kijana na kuepuka utegemezi ambao huwafanya kuwa wanyonge.

Baadhi ya michezo itakayopewa kipaumbele ni mpira wa miguu, kuimba na kucheza muziki,sarakasi, bao, drafti, goma za asili pamoja mbio fupi na ndefu.

Ili kufikia azma hiyo, Lutandula amesema iwapo atachaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Chato Kusini Oktoba 29 mwaka huu, atahakikisha anaazisha tamasha la michezo mbalimbali litakalofanyika kila mwaka kwenye mji wa Bwanga likiambatana na nyama choma.

Amesema hayo kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya kampeni za Uchaguzi zilizofanyika kwenye Kata ya Minkoto wilayani Chato mkoani Geita,huku akiahidi kushirikiana kwa ukaribu na wananchi katika kuhakikisha maendeleo ya haraka yanapatikana.

“Mkinichagua kuwa Mbunge wenu nitahakikisha ndani ya siku 100 za Ubunge wangu nakamilisha vyumba 10 vya madarasa ya Sekondari ya Kalembela, natambua mmeianzisha kwa nguvu zenu kwahiyo nitahakikisha nawaunga mkono katika hilo”,

Amesema hatua hiyo itapunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu na kuwanusuru wa kike na mimba za umri mdogo.

Kadhalika ameahidi kufikisha huduma ya maji safi na salama kupitia mradi mkubwa wa miji 28 nchini, ambao pia unatekelezwa katika wilaya ya Chato.

Kuhusu suala la ukosefu wa umeme, mgombea huyo ameahidi kushirikiana na Shirika la Umeme nchini(Tanesco) kutatua changamoto hiyo ili kukuza uchumi wa wananchi kwa kufanya kazi saa 24 huku akiwahamasisha wananchi kujiandaa kwa miradi itakayotumia nishati hiyo.

Kwa upande wake Mgombea Udiwani wa CCM Kata ya Minkoto, Paulo Mfanisi, amemwomba mgombea huyo kuwasaidia wananchi kupata maeneo ya kilimo baada ya maeneo waliokuwa wakitumia awali kutwaliwa na Wakala wa huduma za misitu nchini(TFS) kupitia shamba la miti la Silayo.            



Mwisho