Dk Mwinyi: Serikali itaendelea kuwekeza kwenye uchumi wa buluu

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali itaendelea kusimamia sekta ya uchumi wa buluu kwa kujenga masoko ya kisasa na kuimarisha miundombinu ya uvuvi na kilimo cha mwani ili kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja na mnyororo wa sekta hiyo.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Oktoba 8, 2025, wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la soko la kisasa la uvuvi Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba, sambamba na kugawa boti kwa wakazi wa Kisiwa cha Makoongwe na vifaa vya kilimo cha mwani kwa wakulima wa kijiji cha Mkiang’ombe.

Amesema lengo la hatua hiyo ni kuongeza thamani ya mazao ya baharini, kupanua fursa za ajira na kuongeza kipato cha wananchi.
“Hatua hii ni sehemu ya kuendeleza miradi iliyopangwa kuhakikisha uchumi wa buluu unakua, thamani ya mazao ya bahari inaongezeka na wananchi wanapata kipato cha uhakika,” amesema.

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, sekta ya uvuvi na mwani ni nguzo muhimu kwa uchumi wa Zanzibar, ikizalisha ajira zaidi ya 100,000, ambapo wanawake wanachangia takribani asilimia 17.

Amesema Serikali imeendelea kuwapatia wajasiriamali vifaa vya kisasa, elimu na mafunzo, pamoja na kuwezesha upatikanaji wa masoko ya uhakika.

Aidha, amesema jitihada hizo zimezaa matunda kwa kuongezeka uzalishaji wa mwani na kiwango cha uvuvi wa samaki, huku Serikali ikiendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya kisasa.

“Awamu ya kwanza ya ujenzi wa bandari ya Shumba imekamilika, na hatua zinazofuata zitahusisha ujenzi wa masoko na madiko ya kisasa, ikiwemo soko na diko la samaki Kiwani na kiwanda cha kusarifu mwani Chokocho,” amesema.

Akizungumzia makabidhiano ya boti mpya kwa wananchi wa Kisiwa cha Makoongwe, Rais Mwinyi amesema hatua hiyo itaboresha usafiri wa majini, huku akinukuu pia mpango wa kuwakabidhi kina mama wa Mkiang’ombe boti kwa ajili ya kilimo cha mwani.

Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla amesema soko jipya la Mkoani litakuwa la kwanza nchini kuwa na lifti ya kisasa, jambo alilolitaja kama ishara ya maendeleo makubwa yanayotekelezwa kwa wananchi.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Rashid Hadid Rashid, amesema mkoa huo umeendelea kuwa salama na ustawi wake umechochewa na miradi ya uchumi wa buluu.

Amesema Serikali imeshakabidhi jumla ya boti 270, majokofu 90 ya kuhifadhi samaki na zaidi ya vikundi 84 vya wakulima wa mwani vimenufaika.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Hamad Bakar Hamad amesema soko hilo litahudumia zaidi ya watu 10,000 kwa siku na kuwa na uwezo wa kushusha vyombo vidogo 350, huku wafanyabiashara 60 na maduka 40 yakitarajiwa kufanya shughuli zao.

Ameongeza kuwa Serikali imegawa vihori 150 vyenye thamani ya Sh375 milioni na uwekezaji katika sekta ya uvuvi umefikia Sh36.65 bilioni, hali iliyochangia ongezeko la uzalishaji wa samaki kwa asilimia 201.

Akitoa shukurani kwa niaba ya wananchi wa Kisiwa cha Makoongwe, Dhamir Kombo amesema boti waliyopewa itasaidia kupunguza changamoto za usafiri zilizokuwa zikiwakabili, hasa nyakati za upepo mkali.

Ameahidi kuwa wananchi wataitumia ipasavyo na kuepuka matumizi kinyume na taratibu za Serikali.