Kampeni za mgombea mwenza wa urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi leo Jumatano, Oktoba 8, 2025 zitahamia visiwani Zanzibar.
Dk Nchimbi anatarajiwa kufanya mikutano miwili mikubwa Kaskazini Pemba kisha atamalizia Kusini Unguja.
Katika mikutano hiyo, Dk Nchimbi atainadi Ilani ya uchaguzi mkuu ya chama ya mwaka 2025/2030 na kumwombea kura Samia Suluhu Hassan za urais, wagombea ubunge na udiwani.

Pia, atamnadi mgombea urais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, anayetetea nafasi hiyo kwa miaka mitano mingine.
Dk Nchimbi anakwenda kusaka ushindi wa CCM Zanzibar huku akiwa amefanya hivyo katika mikoa 18 ya Tanzania Bara.
Mikoa hiyo 18 ambayo ameifikia ni Mwanza, Mara, Simiyu, Shinyanga, Geita, Kagera, Rukwa, Katavi, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Ruvuma, Njombe, Iringa, Dar es Salaam, Mtwara, Lindi na Tabora.
Akimaliza Zanzibar, Dk Nchimbi ataendelea kuchanja mbunga akihamia mkoa wa Pwani, Kigoma, Dodoma na maeneo mengine kwa mujibu wa ratiba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) itakavyoelekeza.
Kwa upande wake, Samia ambaye pia ni Rais anaendelea na mikutano kanda ya ziwa akianzia jijini Mwanza na akimaliza atakwenda Simiyu, Mara, Shinyanga na Geita.
Kampeni za uchaguzi mkuu zilianza Agosti 28 na zitahitimishwa Oktoba 28, 2025 na kesho yake yaani Jumatano ya Oktoba 29, 2025 itakuwa siku ya kupiga kura.
Kwa mujibu wa INEC, Watanzania wenye sifa za kupiga kura walioandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Mpiga Kura ni milioni 37.6 watakaoamua nani awe Rais, diwani na mbunge wao kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Imeandikwa na Ibrahim Yamola