BAADA ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA), kuridhia timu ya Fountain Gate kufanya usajili nje ya dirisha la usajili, uongozi wa kikosi hicho umepanga kuandaa tamasha maalumu la kuwatambulisha rasmi nyota wapya wa msimu huu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Fountain Gate, Wendo Makau, alisema wamepokea taarifa hiyo kwa mikono miwili kwa sababu imeleta ari kwa benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki wa kikosi hicho kutokana na mwanzo mbaya walioanza nao.
“Hii ni habari njema sana kwetu kwa sababu ni jambo lililokuwa linatuumiza kutokana na idadi ndogo ya wachezaji tulioanza nao msimu, tunachotaka kufanya kwa sasa ni kuandaa tamasha hivi karibuni la utambulisho wa nyota wetu wapya,” alisema Wendo.

Wendo, alisema tamasha hilo ambalo litatoa fursa kwa mashabiki kuona kikosi kipya cha msimu, litatumika pia kutambulisha jezi mpya, ambapo shughuli hiyo itafanyika kabla ya mechi ijayo ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji, Oktoba 17, 2025.
Mwanzoni timu hiyo haikuruhusiwa kusajili baada ya FIFA na TFF kuifungia kutokana na madeni iliyokuwa ikitakiwa kuwalipa wachezaji kwanza na japo iliwalipa ndani ya muda, taarifa zilichelewa kuzifikia mamlaka hizo hadi mfumo wa usajili ukafungwa.

Taarifa iliyotolewa juzi na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilisema FIFA imeiruhusu timu hiyo kusajili nje ya dirisha la usajili lililofungwa Septemba 7, 2025, kwa sababu za kiufundi pia zilizojitokeza na kushindwa kukamilisha usajili huo kwa wakati.
Timu hiyo ilifungiwa kusajili kutokana na kudaiwa na waliokuwa nyota wake wawili wa kigeni,
Miongoni mwa nyota wapya ambao hawajaitumikia timu hiyo ni beki wa kati, Mrundi Derrick Mukombozi aliyeachana na ‘Wauaji wa Kusini’ Namungo sambamba na mshambuliaji, Joshua Ibrahim aliyekichezea pia kikosi hicho kwa mkopo akitokea KenGold.

Timu hiyo inayonolewa na Mohamed Ismail ‘Laizer’, aliyerithi nafasi ya Denis Kitambi, imechapwa mechi tatu za Ligi Kuu Bara, ikianza na bao 1-0, dhidi ya Mbeya City, Septemba 18, 2025, kisha 3-0 na Simba, Septemba 25, 2025.
Mechi hizo zilikuwa za mwisho kwa Kitambi kusimamia benchi la ufundi, kisha Laizer, ambaye kwa msimu wa 2024-2025, ndiye aliyeinusuru kutoshuka daraja, aliiongoza na kushuhudia akipoteza mabao 2-0, dhidi ya Mtibwa Sugar, Septemba 28, 2025.