MABORESHO ya benchi la ufundi la Simba yanaendelea, baada ya ujio wa Dimitir Pantev na msaidizi wake, Simeonov Boyko Kamenov waliotokea Gaborone United ya Botswana, sasa ameshushwa mtu mwingine.
Alfajiri ya leo Jumatano Oktoba 8, 2025, Simba SC imemshusha kwa siri sana kocha wa makipa kutoka Bulgaria kwa ajili ya kuimarisha benchi la ufundi la timu hiyo linaloongozwa na Dimitir Pantev.
Mtaalamu huyo aliyetua majira ya saa 9:05 alfajiri na ndege ya Shirika la Uturuki, ni Vitomir Vutov mwenye umri wa miaka 53 ambapo amekuja kuungana na wenzake siku chache baada ya kuondoka kwa Fadlu Davids.

Ujio wa Vutov, unalifanya benchi la ufundi la Simba kuwa na raia watatu kutoka Bulgaria, wengine ni Pantev aliyetambulishwa kama Meneja Mkuu na msaidizi wake, Simeonov Boyko Kamenov.
“Ni kweli jamaa amekuja na leo asubuhi amefika uwanja wa mazoezi kutambulishwa kwa wachezaji,” kimesema chanzo kutoka Simba.
“Amekuja kwa ajili ya kuwafundisha makipa kwa sababu nafasi hiyo haikuwa na kocha baada ya Fadlu kuondoka na wasaidizi wake.”
Hata hivyo, Simba inafanya siri sana juu ya ujio wa kocha huyo huku ikielezwa muda wowote atatambulishwa.
Vutov ambaye rekodi zinaonyesha mara ya mwisho alikuwa na kikosi cha FC Lovech huko Bulgaria, anakuja kuchukua nafasi ya Wayne Sandilands ambaye ameondoka na Fadlu kuelekea Raja Casablanca.
Rekodi zinaonyesha Vutov kabla ya kutua Simba, amepita kufundisha klabu kadhaa ikiwemo Spartak Varna, PFC Lokomotiv Plovdiv, FC Lokomotiv Gorna Oryahovitsa, Litex Lovech zote za Bulgaria.

Septemba 22, 2025, wakati Fadlu anaaga ndani ya Simba, aliondoka na wasaidizi wake wanne ambao ni Darian Wilken (Kocha Msaidizi), Wayn Sandilands (Kocha wa Makipa), Durell Butler (Kocha wa Utimamu) na Mueez Kajee (Mchambuzi wa Video).
Kuondoka kwa Fadlu na wasaidizi wake, imeifanya Simba kuboresha benchi la ufundi ambapo sasa Seleman Matola aliyeendelea kubaki kama kocha msaidizi, Pantev amekuja na msaidizi wake mwingine aliyekuwa naye Gaborone United. Pia Vutov ametua kwa ajili ya kuwanoa makipa, huku kocha wa utimamu akipewa jukumu hilo amepewa mzawa, Mohamed Mrishona Mohamed ‘Xavi’.