Kunambi: Wanawake tusitishwe, tujitokeze kwa wingi kupiga kura

Moshi. Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT), Suzan Kunambi amewataka wanawake nchini kutoogopa vitisho vinavyotolewa na baadhi ya watu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.

Bali amesisitiza kuwa wanayo nafasi kubwa ya kuhakikisha ushindi wa mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, pamoja na wagombea wengine wa chama hicho unapatikana kwa kishindo.

Akizungumza leo Jumatano Oktoba 8, 2025 na wanawake wa mjini Moshi, Kunambi amesema vitisho vinavyosambazwa havina ukweli wowote na vina lengo la kuwatia hofu wananchi ili wasijitokeze kupiga kura.

“Tusikubali kutishwa wala kuhadaiwa. Haki ya kupiga kura ni ya kila Mtanzania kwa mujibu wa Katiba. Tuwe mabalozi kwa familia zetu, marafiki na majirani. Oktoba 29 twendeni tukachague kiongozi jasiri, mchapakazi na mvumilivu ambaye ni Samia Suluhu Hassan,” amesema Kunambi.

Amesisitiza kuwa Tanzania ni kisiwa cha amani na wanawake wanapaswa kuwa mstari wa mbele kutetea, kulinda na kuidumisha bila kuyumbishwa.

“Msikubali vitisho, Tanzania ni nchi ya amani, tusije kuthubutu kuivuruga na wanawake ni jeshi kubwa, simameni kuilinda amani yetu,” amesema kiongozi huyo.

Aidha, Kunambi amewataka wagombea wa CCM wa kiti cha udiwani kuhakikisha wakishinda, wanaondoa mifumo kandamizi ya mikopo kwa wanawake na kusimamia utoaji wa mikopo nafuu kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.

“Wapo wanawake wanaoingia katika mikopo ya kausha damu. Tuwaondoe huko, tuwaongoze kuchangamkia fursa za mikopo iliyotolewa na Rais Samia. Hii ndiyo njia ya kweli ya kumkomboa mwanamke,” amesema.

Akigusia maendeleo ya Serikali, amesema awamu ya sita chini ya Samia imetekeleza miradi mikubwa katika sekta za elimu, afya, barabara, maji na nishati, hivyo ni wajibu wa wananchi kumuunga mkono ili amalizie kazi aliyoanza.

Kunambi ameongeza kuwa CCM inaamini itashinda majimbo yote tisa na kata 169 za Mkoa wa Kilimanjaro, kupitia ilani yake ya 2025–2030 ambayo imebeba dira ya maendeleo kwa Taifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Kilimanjaro, Elizabeth Minde amesema wanawake wa mkoa huo wako tayari kushiriki uchaguzi kwa mshikamano na amani ili kuhakikisha wagombea wa CCM wanapata ushindi.

Naye mgombea ubunge wa viti maalumu mkoani humo, Esther Maleko amewaomba wanawake wote kumuunga mkono mgombea urais wa CCM kwa vitendo, akieleza kuwa chama chao kimejiandikia historia kubwa kwa kumsimamisha mwanamke kuongoza nchi.

“Tuende tukamheshimishe mama yetu Samia kwa kazi kubwa alizofanya. Dunia nzima inashuhudia mabadiliko aliyoyaleta. Wanawake tusifanye makosa Oktoba 29,” amesema Maleko.

Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Mercy Mollel amesisitiza kuwa kazi kubwa iliyobaki ni kuhakikisha wananchi wanajitokeza kwa wingi kupiga kura kwa rais, wabunge na madiwani wa Chama cha Mapinduzi ifikapo Oktoba 29.