Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala Ndogo ya Dar es salaam imepanga Oktoba 9, 2025 kusikiliza maombi ya Wakili Peter Kibatala juu ya madai ya kutekwa kwa Mwanasiasa Humphrey Polepole.
Wakili Kibatala aliwasilisha maombi hayo chini ya hati ya dharura, Oktoba 7, 2025 akiiomba mahakama itoe amri ya Polepole afikishwe mahakamani ama mamlaka husika ziseme yupo wapi.
Kwa mujibu wa hati iliyosajiliwa baada ya kupokelewa kwa maombi hayo imepewa namba 24514 ya mwaka 2025 na imepangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Salma Maghimbi, ambapo katika maombi yake, Kibatala ameiomba Mahakama iingilie kati mara moja akidai kuwa Polepole alitekwa nyara alfajiri ya Jumatatu, Oktoba 6, 2025, kutoka katika makazi yake yaliyoko eneo la Ununio, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam na watu wasiojulikana wanaoshukiwa kuwa ni askari wa Jeshi la Polisi la Tanzania.
Katika hati hiyo ya dharura Wakili Kibatala ameieleza Mahakama kuwa Polepole hajawahi kushtakiwa kwa kosa lolote la jinai katika Mahakama yoyote, na kwamba kwa sasa inaaminika anashikiliwa katika eneo lisilojulikana na maafisa wa Jeshi la Polisi.
Maombi hayo yamewasilishwa dhidi ya wajibu Maombi watano, akiwemo Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Afisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalum ya Dar es Salaam (RCO) na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (RPC).
Related