Mapya kutekwa kwa Polepole | Mwananchi

Dar es Salaam. Siku moja baada ya kusambaa taarifa za kutekwa kwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, taarifa mpya zimeibuka huku mawakili wake wakifungua kesi ya kutaka mamlaka husika zimfikishe mahakamani.

Mbali na hatua hiyo, mmoja wa majirani wa nyumba anayodaiwa kutekwa Polepole, ameeleza kile alichoshuhudia wakati wa tukio, huku msimamizi wa nyumba hiyo akibainisha kuwa hakuwahi kufahamu kama Polepole ndiye alikuwa akiishi hapo.

Wakati hayo yakijiri, Jeshi la Polisi kupitia kwa Msemaji wake, David Misime lilitoa taarifa Oktoba 6, 2025, likieleza kuwa uchunguzi wa madai ya utekaji huo umeanza.

Wakati huohuo, Misime alisema bado wanamsubiri Polepole kufika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kutoa maelezo kuhusu madai mbalimbali aliyoyatoa dhidi ya Serikali na viongozi wake.

Hata hivyo, taarifa nyingine ya polisi iliyotolewa leo Oktoba 7, 2025, imeeleza kuwa jeshi hilo linamtafuta kaka wa Polepole, aitwaye Augustino Polepole, kufuatia madai aliyosambaza kwenye mitandao ya kijamii, akimtuhumu ofisa mmoja wa polisi kuwa ndiye aliyehusika na utekaji huo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, wanamtafuta Augustino kwa lengo la kupata maelezo ya kina na vielelezo, vinavyoweza kusaidia kufafanua madai yake.

Wakati hayo yakiendelea, mmoja wa majirani na nyumba alikotekwa Polepole, amesema damu zilizomwagika wakati wa kutekwa kwa Humphrey Polepole ni nyingi.

Jirani huyo ambaye jina lake linajifadhiwa, amedai baada ya kusikia kelele usiku alijua ni za kifamilia, hivyo waliendelea kulala, lakini baada ya kusikiliza kwa utulivu, alibaini jambo la tofauti na aliamka kuhakikisha kinachoendelea, japo hakufungua geti.

“Sikufungua geti nilichungulia nje niliona magari mawili aina ya Land Cruiser, moja limesimama upande wa kushoto lingine upande kulia, mtu aliwekwa ndani na niliona magari yakiondoka.

“Asubuhi tulitoka kuangalia nini kilitokea tulikuta damu nyingi, tulijuiliza kama huyu mtu atakuwa hai, hatukuwa tukifahamu ni nani hadi tulipoona mitandaoni kuwa ni Polepole,” amesema jirani huyo alipozungumza na Mwananchi.

Kwa upande wake Annamary Polepole, mama mzazi wa Polepole ameeleza masikitiko yake akitoa wito mwanawe aachiwe huru.

“Wamwachie mwanangu kama yupo hai, kama hayupo hai waniletee nimzike mwenyewe, waniletee mwanangu nimzike mwenyewe wasiende kumtupa baharini,” ni kauli ya mama huyo alipozungumza na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

“Unapokuwa umemsomesha mtoto tangu akiwa kichanga hadi akafika sehemu unamtegemea kuwa anaweza kukuletea doti la kanga, leo wenzio wanakuja kukukatia ghafla tu sababu ni nini hasa….?” amehoji.

Mama huyo amesema hata dada yake Polepole alichukuliwa kwa ukuta kubomolewa.

“Inasikitisha sana, ina maana wanaumiza watu kama nyati wa porini au tembo, inasikitisha sana kwa nchi ya Tanzania hayati Mwalimu Julius Nyerere hakutulea hivyo,” amelalamika.

Amesema Polepole alikuwa mwanaye wa kipekee na alipenda kusomea urubani na uchungaji, lakini wazazi hawakuwa na uwezo wa kumsomesha fani ya urubani.

Annamary ameeleza kuwa Polepole mara zote ni mtu mwenye upendo na mcheshi muda wote, ambaye husalimiana na watu kila wakati na alipokuwa mdogo mara zote hakuwa muomgeaji, bali mwenye kusalimu na kujisomea.

Msimamizi wa nyumba alikotekewa Polepole amesema yeye hakuwahi kufahamu kama Polepole ndiye alikuwa kwenye nyumba hiyo, kwa kuwa aliyempangisha ni mtu mwingine.

Amesema, awali hakumfahamu aliyekwenda kutafuta nyumba kwa jina na aliambatana na mtu mwingine aliyetemtambulisha kama mama yake.

“Kwa hiyo nilimpangisha kwa sababu huyo kijana aliniambia mama yake ndiye atakuwa anakaa humo na atakuwa yeye anakuja kwenye nyumba hiyo siku moja moja kwa sababu anafanya kazi Dodoma. Kwa hiyo sikujua nani anaishi humo ndani hadi tukio hili lilivyotokea,” amesema.

Nyumba ilipangishwa Julai 11, 2025 na msimamizi huyo amesema tangu wakati huo haikufahamika nani yupo ndani, ingawa kila wiki wapo vijana wanakwenda kufanya usafi ndani ya nyumba hiyo.

Baada ya uvamizi kutokea, msimamizi huyo amesema walipata taarifa asubuhi kutoka kwa mmoja wa sungusungu anayezunguka kwenye mtaa huo.

Baada ya kupata taarifa hiyo, akafika eneo la tukio na kuangalia kilichotokea na kwa njia ya simu akawasiliana na aliyepanga nyumba hiyo, akimuuliza kama anafahamu tukio lililotokea.

“Nilipomweleza kuwa nyumba imevunjwa na damu zimetapakaa, alishtuka na akaniambia yeye yupo Kinyerezi, anakuja. Na alipofika alikuwa na ndugu zake wengine watatu, ndipo alipoanza kunielezea ukweli, ni nani aliyekuwa ndani ya nyumba hiyo,” amesema.

Msimamizi huyo amesema baada ya ndugu hao kusema aliyekuwemo ni Polepole, wote walifika eneo la tukio kubaini damu nyingi zilizovunja ndani na nje ya nyumba.

Ametaja uharibifu uliofanyika kwenye nyumba hiyo ni kuvunjwa geti la nje na la ndani, milango miwili, wa nje na wa chumba alichokuwa amelala Polepole.

Msimamizi huyo amesema alipouliza majirani nini kimetokea, aliambiwa usiku walisikia milio ya magari ikipita na baadaye walisikia kishindo cha kuvunjwa magaeti na milango katika nyumba hiyo lakini hawakuweza kutoka, ingawa baadhi yao walichungulia kupitia madirishani majira ya saa nane usiku.

Hata hivyo, msimamizi huyo amesema majirani hao waliendelea kusikia vishindo na kisha kelele za kuomba msaada na sauti za magari yakiondoka.

“Kwa sababu sikuwepo katika tukio, ila kwa maelezo ya majirani hata kelele walizosikia walishindwa kutoka kutokana na usiku mkubwa na hivyo waliamua kutoka asubuhi na kukuta damu na milango iliyovunjwa,” amesema.

Pia, amezungumzia mazingira ya nyumba ya vyumba vitatu vya kawaida, kuwa haijawahi kuwekwa kamera.

Kufuatia tukio hilo, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limelaani tukio la kutekwa kwa Polepole.

“Kwa vyovyote iwavyo, tunasema maisha na uhai wa Watanzania wenzetu ni kipaumbele cha kwanza kwa amani ya taifa letu. Amani ni tunda la haki, na hatuwezi kukubali vitendo vya utekaji vinavyozua hofu miongoni mwa wananchi,” imesema TEF katika taarifa yake iliyotiwa saini na Mwenyekiti wa Deodatus Balile.

Kwa upande wake, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) umelaani tukio hilo na kumtaka Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati sakata hilo kwa kutumia rasilimali zote zilizopo ili kuokoa maisha ya Polepole.

Wakati hayo yakiendelea, leo Oktoba 7, 2025, jopo la mawakili wakiongozwa na Peter Kibatala limefungua shauri la maombi maalumu kwa niaba ya Polepole.

Miongoni mwa mambo yanayoombwa katika shauri hilo lililofunguliwa katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, ni amri ya mahakama kuwaamuru wajibu maombi kumfikisha Polepole mahakamani.

Wajibu maombi katika kesi hiyo ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZCO) na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZPC).

Katika hati hiyo ya dharura iliyothibitishwa na Wakili Kibatala, imeelezwa kuwa tangu Oktoba 6, 2025, Polepole aliripotiwa kutekwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni maofisa wa Jeshi la Polisi waliovamia nyumbani kwake eneo la Ununio, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Pia, Kibatala amedai katika maombi hayo yaliyosajiliwa kwa njia ya mtandao, kuwa hadi sasa Polepole hajashtakiwa kwa kosa lolote la jinai katika mahakama yoyote ya kisheria, na kwamba inaaminika amewekwa kizuizini mahali kusikojulikana na wajibu maombi.

“Hivyo haki zake za Kikatiba zimekiukwa bila sababu za msingi,” amesema Kibatala na kuongeza:

“Ustawi wa mwombaji unahitaji uangalizi na uingiliaji wa haraka, ikiwemo kujua hali ya maisha yake.”

Katika hati ya maombi hayo, mawakili hao wameomba wasikilizwe upande mmoja na mahakama iamuru Polepole afikishwe mahakamani, akisubiri uamuzi wa maombi hayo kusikilizwa pande zote.

Wameomba pia mahakama iwaelekeze wajibu maombi wamwachie huru Polepole kwa dhamana au wamfikishe katika mahakama ya kisheria na kumshtaki kwa mujibu wa sheria.