MFAUME KHAMIS HASSAN: Mwanajeshi anayehitaji urais wa Zanzibar awe kama Karume

Aghalabu (mara nyingi), uelekeo wa kifamilia hujenga wasifu wa vizazi. Wazazi wanasheria, watoto wanaibuka kuwa mawakili, mahakimu, au majaji. Madaktari kadhalika. Ni kutimia kwa methali ya wahenga kwamba maji hufuata mkondo.

Inawezekana mtoto kuchukua mkondo tofauti na wazazi wake, lakini kwa kawaida, mapendeleo ya wazazi huingia kwa urahisi ndani ya watoto, hivyo kuwafanya wafuate nyayo zao.

Majadiliano ya hapa na pale, ubishi ndani ya kuta za nyumba, na mazungumzo kwenye meza ya chakula ‘hushepu’ uelekeo wa watoto.

Haiwi ajabu mtoto wa mwanamuziki kuwa mwimbaji, daktari, au mwanasiasa kama wazazi wake. Mfaume Khamis Hassan, ambaye jina lake linaunda orodha ya wanaowania urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu 2025, ni mwanasiasa baada ya hamasa ya nyumbani na sasa anapeperusha bendera na kunadi Ilani ya Chama cha National League for Democracy (NLD).

Familia yake imekuwa na uitikio mkubwa kwenye siasa. Kuanzia baba yake mzazi, marehemu Khamis Hassan Kombo, na mama yake, Miza Silima Khamis, waliokuwa wanachama wa Afro Shiraz Party (ASP), chama kilichofanikisha Mapinduzi ya Zanzibar, Januari 12, 1964.

Mfaume anasema kuwa wazazi wake wote wawili hawakuwepo Zanzibar kushuhudia Mapinduzi, bali walishiriki moja kwa moja harakati zilizochagiza mageuzi ya mfumo wa kiutawala Zanzibar, ya kuuondosha utawala wa Sultan, hivyo kuifanya Zanzibar kuwa dola huru, Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, kabla ya kujiunga na Tanganyika kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hamasa ya wazazi wake kushiriki moja kwa moja siasa za ukombozi wa Zanzibar jumlisha kaka yake, Ali Khamis Hassan, aliyekuwa mwanachama hai wa Chama cha Wananchi (CUF), akishiriki vuguvugu za uenezi wa chama hicho. Hii ilikuwa mbegu iliyopandwa na kuchipua ndani yake, akatamani kuwa mwanasiasa.

Mbegu hiyo iliyochipua ndani ya Mfaume imesababisha familia yao isiishie kuwa ya wanachama hai wa vyama pekee, bali kupitia yeye, amepatikana kiongozi wa kisiasa anayepigania kuingia ofisi namba moja ya uongozi visiwani Zanzibar, Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja Zanzibar (MMH), ipo Barabara ya Kaunda, Zanzibar. Ilijengwa na kuanza kazi miaka 40 kabla ya Mapinduzi. Muda mfupi baada ya mafanikio ya Mapinduzi, hospitali hiyo ilipewa jina la VI Lenin Hospital. Ndipo baadaye ikaitwa Mnazi Mmoja.

Juni 16, 1967, ndani ya hospitali hiyo, MMH alizaliwa Mfaume. Kwa ufafanuzi, Mfaume ni kitinda mimba cha baba na mama yake. Yeye ni mtoto wa saba miongoni mwa watoto saba wa Khamis Hassan Kombo na Miza Silima Khamis.

Safari ya Mfaume kusaka elimu ilianzia Shule ya Msingi Kisiwandui, Zanzibar, akamalizia Shule ya Msingi Forodhani, pia ya Zanzibar. Elimu ya sekondari, ya kidato cha kwanza mpaka cha nne, Mfaume alisoma Shule ya Sekondari Haile Selasie, Unguja, Zanzibar.

Baada ya kumaliza elimu ya msingi, Mfaume alijiunga na mafunzo ya kijeshi, kisha akaajiriwa kwenye Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM), Zanzibar. Ajira yake KMKM ilikuwa ya mkataba wa miaka 15, kutoka mwaka 1985 mpaka 2000, alipoondoka jeshini kwa hiari.

Kati ya mwaka 1962 na 1992, ni miaka 30 ambapo Tanzania ilikuwa dola ya mfumo wa chama kimoja. Katika kipindi hicho, majeshi yote yalikuwa yanafungamana na chama kilichokuwa kinaongoza Serikali, Tanganyika African National Union (TANU) na ASP kabla ya Februari 5, 1977, halafu Chama cha Mapinduzi (CCM), Februari 5, 1977 mpaka Julai 1, 1992.

Mwaka 1987, Mfaume alikuwa bado jeshini (KMKM). Kutokana na mazingira yaliyokuwepo na jinsi majeshi yalivyokuwa yakifungamana na siasa, Mfaume hakuwa na budi, zaidi ya kuchukua kadi ya uanachama wa CCM.

Mwaka 2000, baada ya kuondoka jeshini, alianza kupanga kuingia kwenye siasa za ushindani. Hakutaka kubaki mfuasi kama wazazi wake na kaka yake. Mwaka 2002, alijiunga na chama cha National League for Democracy (NLD).

Ndani ya miezi sita tangu alipojiunga na NLD, Mfaume aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania Bara, nafasi aliyohudumia kwa mwaka mmoja. Mwaka 2003, Mfaume alithibitishwa na Mkutano Mkuu wa NLD Taifa kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar.

Oktoba 15, 2015, aliyekuwa Mwenyekiti wa NLD na mwasisi wa chama hicho, Dk Emmanuel Makaidi, alifariki dunia. Baada ya hapo, Mfaume alirithi mikoba ya uongozi wa chama hicho. Hadi sasa, ndiye Mwenyekiti wa NLD Taifa.

Uchaguzi Mkuu 2025, si mara ya kwanza kwa Mfaume kuwania urais Zanzibar, kwa kuwa alifanya hivyo pia katika Uchaguzi Mkuu 2020. Vilevile, Mfaume aliwania ubunge jimbo la Kiwajuni, Zanzibar, katika Uchaguzi Mkuu 2010 na 2015.

Ukimwondoa kwenye ofisi na majukwaa ya kisiasa, Mfaume ni mkulima na mfugaji. Pia amejishughulisha na uvuvi na biashara kwa kipimo cha wastani. Kifamilia, Mfaume ni baba mwenye wake watatu na watoto wanne, wawili wa kiume na wengine wa kike.

Mfaume anasema kuwa shabaha yake ya kuutaka urais wa Zanzibar ni kuwatumikia wananchi wa Zanzibar na kuwapa maendeleo, muhimu zaidi kuwaongoza katika misingi ambayo itahakikisha amani inatamalaki visiwani humo.

Anataja vipaumbele vyake kuwa ni afya bora, elimu bora, kutokomeza udhalilishaji Zanzibar, na ajira kwa vijana.

Anasema kuwa kijana akiwa na ajira, atakuwa na shughuli ya kufanya, hivyo hatafungamana na vishawishi visivyofaa mitaani na mitandaoni. Kijana hushawishika kufanya vitu vibaya endapo hatakuwa na kazi ya kufanya.

Anabainisha kuwa msingi mkuu wa kumdhibiti kijana ili awe na nyenendo njema kijamii ni kumpa kazi, awe na kipato, na ajielekeze kujenga maisha yake.

Ahadi ya Mfaume ni kwamba, akiwa Rais wa Zanzibar, kila kijana kwenye visiwa hivyo lazima atakuwa na kazi. Anasema kuwa hatamwacha kijana mtaani, kwani kuwaacha vijana bila shughuli ni sawa na kuliangamiza taifa. Ndiyo maana baadhi yao wanakuwa walevi kupindukia au kutumia dawa za kulevya.

Mfaume anasema kuwa ahadi yake ya kumpa kazi kila kijana itahakikisha siyo kazi ya lazima tu, bali shughuli zenye tija, zitakazowapa vipato vya kutosha, na Serikali itakusanya kodi kupitia kwao.

“Hili la kila kijana kuwa na shughuli ya kufanya linawezekana, Wazanzibari waniamini,” anasema Mfaume.

Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, hakutaka vijana wawe mitaani bila kazi. Aliwachukua na kuwaingiza kwenye vikosi mbalimbali vya jeshi ili wawe na mchango kwa taifa, lakini zaidi kuwaepusha na matokeo mabaya yanayowakumba vijana bila shughuli.

Mfaume anasema kuwa aina yake ya uongozi itashabihiana na Sheikh Karume, kwani haoni sababu ya vijana wa Zanzibar kutotumika katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya visiwa vyake, wakati uwezo huo upo.

Wito wa Mfaume, Uchaguzi Mkuu Zanzibar unapokaribia, ni kuwa Wazanzibari wawe watulivu na wadumishe amani. Anawataka wawe na umoja, kwa maana hiyo ndiyo ngao yao.

Anawakumbusha kujiandaa kujitokeza kwa wingi kupiga kura, na siku ikifika, ajitokeze kwa amani na akimaliza, arejee nyumbani kwa amani.

Ombi la Mfaume kwa Wazanzibari na Watanzania wote ni kutoshawishiwa na hamasa ya maandamano yenye lengo la kuvuruga amani na utulivu wa nchi. Anakumbusha kuwa yeye ni mwanajeshi, kwa hiyo anajua amani ikivurufika hali itakuwaje.