MGOMBEA UBUNGE CHATO KUSINI ABISHA HODI KWA MGANGA WA JADI

Kulia ni mgombea Ubunge,Paschal Lutandula, akisalimiana (kushoto) na Mganga wa Jadi maarufu, Chenela Maswaduki

Kulia ni mke mkubwa wa Mganga wa Jadi,Pili Misalaba, akikabidhi fedha kwa mgombea Ubunge wa Jimbo la Chato Kusini, Paschal LutandulaKushoto ni mke wa kati wa Mganga wa Jadi,Mondester Malula,baada ya kumaliza kumfanyia dua maalumu mgombea Ubunge wa Jimbo la Chato Kusini,Paschal Lutandula,(katikati)

………,…….

CHATO

WAKATI Kampeni za Uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani mwaka 2025 ukienndelea kote nchini, Mgombea wa Ubunge(CCM) Jimbo la Chato Kusini, Paschal Lutandula,amefika nyumbani kwa mganga maarufu wa jadi kwenye kijiji cha Busambilo kata ya Minkoto wilayani Chato mkoani Geita kwa lengo la kuomba kura.

Amefika nyumbani kwa mganga huyo Majira ya saa 5:30 mchana nakukutana na watu mbalimbali ikiwemo familia na wagonjwa waliolazwa eneo hilo kwaajili ya kupata huduma za tiba za magonjwa yanayowasibu.

Lutandula baada ya kufanya mazungumzo ya takribani dakika 15 na mganga huyo,Chenela Maswaduki, pamoja na wake zake watatu, ameahidi kutatua changamoto ya ukosefu wa umeme nyumbani hapo baada ya kuambiwa kuna wagonjwa zaidi ya 400 wanaotibiwa hapo.

Kadhalika ameiomba familia hiyo pamoja na wagonjwa waliopo kwa mganga huyo kumpigia kura ifikapo Oktoba 29 mwaka huu ili aweze kuwa Mbunge wa Jimbo hilo pamoja na kumchagua kwa kura nyingi mgombea Urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan na Diwani wa kata ya Minkoto, Paulo Mfanisi.

Akizungumza na Torch Media, Mganga huyo wa Jadi, amedai kufurahishwa sana na ujio wa mgombea huyo kwa madai hajawahi kutembelewa na kiongozi yoyote wa CCM kwa lengo la kumuomba kura licha ya kuwa na wagonjwa wapatao 471.

Hata hivyo ameahidi kuwahamisha wagonjwa wake wote kumpigia kura mgombea huyo wa Ubunge kwa kuwa ameonyesha moyo wa kizalendo kwa kumtembelea nyumbani kwake pamoja na kuona changamoto zinazowakabili wananchi wa kitongoji cha Kalembela.

Mke mkubwa wa mganga huyo, Pili Misalaba,amelazimika kutoa zawadi ya fedha kwa mgombea huyo ikiwa ni ishara ya mafanikio katika harakati za mgombea huyo kufanikiwa katika harakati zake za nafasi ya Ubunge.

Kwa upande wake mke wa kati wa mganga huyo, Mondester Malula,akadai kuridhishwa na nia njema ya mgombea huyo kusaidia wananchi wa Jimbo hilo ikiwa ni pamoja na kukubali kutatua changamoto ya suala la umeme nyumbani hapo, ambapo amelazimika kutoa dua maalumu ya kumwombea Lutandula ili asipatwe na mabaya popote atakapokuwa.

                            Mwisho.