MKURUGENZI TWANGE AKAGUA MAENDELEO YA MIRADI YA UMEME DAR ES SALAAM

::::::

Na Josephine Maxime, Dar es Salaam

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Lazaro Twange, amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme jijini Dar es Salaam, ukiwemo ujenzi wa Kituo kipya cha kisasa cha kupoza umeme kilichopo Mabibo pamoja na njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 220 kutoka Kimara–Ubungo–Mabibo hadi Ilala.

Akiwa katika eneo la mradi la Kituo cha kupoza umeme cha Mabibo Oktoba 7, 2025, Bw. Twange amesema licha ya mradi huo kufikia asilimia 70 ya utekelezaji, ujenzi wake unapaswa kukamilika kwa wakati kwa mujibu wa mkataba.

“Ndugu zangu, hii kazi si ndogo. Nataka mfanye kazi usiku na mchana kuhakikisha inakamilika kwa wakati. Haipendezi kufanya kazi kwa presha dakika za mwisho, hasa ikizingatiwa sababu za msingi za utekelezaji wa mradi huu zinajulikana. Hakutakuwa na sababu ya kuomba muda wa nyongeza,” amesisitiza Bw. Twange.

Kwa upande mwingine, mradi wa njia ya kusafirisha umeme yenye urefu wa kilomita 16.5 umefikia asilimia 28.4 hadi sasa ambapo ujenzi wa misingi 13 kati ya 26 katika kipande cha kutoka Ubungo hadi Ilala kupitia Mabibo tayari umekamilika.

Kukamilika kwa mradi huu kunatajwa kusaidia kwa kiwango kikubwa kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa umeme kutoka Kinyerezi hadi Mabibo jambo litakalopelekea kuimarika kwa uwezo wa kituo cha Ubungo sambamba na kuboresha upatikanaji wa umeme katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.