UONGOZI wa KMC unatafuta Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO), baada ya Daniel Mwakasungula, aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo kumaliza mkataba wake, huku taarifa zikieleza Mkurugenzi wa Mashindano wa Yanga, Ibrahim Mohamed, ni miongoni mwa wanaotajwa kumrithi.
Licha ya uongozi wa KMC kutoweka wazi juu ya suala hilo, lakini Mwanaspoti linatambua Ibrahim ni miongoni mwa wanaohitajika ili akakiongoze kikosi hicho, baada ya Mwakasungula kuondoka.
Chanzo kutoka ndani ya timu hiyo kimeliambia Mwanaspoti kuwa, Ibrahim ni miongoni mwa wanaohitajika ili kurithi mikoba ya Mwakasungula, ingawa sio yeye peke yake, kwani hadi sasa yapo zaidi ya majina ya watu sita mezani, japo uongozi haujafanya uamuzi wa mwisho.

“Mchakato ni wa ndani na hakuna uamuzi wa mwisho uliofikiwa hadi sasa, nafikiria tuache kwanza hadi utakapokamilika ndio nitakuwa na nafasi nzuri ya kulizungumzia suala hilo kwa ukubwa, tuvute subra mambo yakamilike,” kimesema chanzo hicho.
Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua, Mwakasungula aliyejiunga na kikosi hicho, Agosti 15, 2022, akichukua nafasi ya Walter Harrison aliyeajiriwa na Yanga kama meneja wa timu hiyo, hataongeza mkataba mpya na kwa sasa anaangalia fursa nyingine.

Mkataba wa Mwakasungula na KMC ulifikia ukomo tangu Septemba 29, 2025, ambapo uongozi wa kikosi hicho cha Manispaa ya Kinondoni unaendelea na mchakato wa kutafuta mrithi wake, wanayeamini ataendeleza mazuri yaliyofanywa na anayeondoka.
Ibrahim anatajwa kuchukua nafasi ya Mwakasungula, ambapo mbali na kuhudumu katika nafasi ya Mkurugenzi wa Mashindano wa Yanga, amewahi kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) katika timu mbalimbali zikiwemo, Kagera Sugar na Singida.