Mbeya. Tatizo Mzumbwe (25), mkazi wa Masoko mkoani Mbeya, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji ya mama yake wa kambo, Merry Yohana (61) kwa madai ya kumkata na panga kichwani.
Merry mwenye ualbino, amefariki dunia baada ya kushambuliwa kwa kukatwa na panga kichwani, kufuatia mzozo wa kugombea mashamba yaliyokuwa yakimilikiwa na marehemu mumewe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa, mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa kwa kina kuhusu tukio hilo.
Kuzaga amedai kuwa, mtuhumiwa alitenda kosa hilo Oktoba 6, 2025, saa 2:00 asubuhi nyumbani kwao katika Kijiji cha Mapinduzi, Kata ya Masoko kwa kumshambulia Merry kwa panga kichwani na kusababisha kumwagika kwa damu nyingi.
Kuzaga amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa, chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa kifamilia uliotokana na mashamba yaliyokuwa ya marehemu mume wa Merry ambaye pia alikuwa baba mzazi wa mtuhumiwa.
“Awali, mtuhumiwa alikuwa akimshinikiza kugawana mashamba ya urithi yaliyoachwa na baba yake jambo ambalo marehemu akakubaliana nalo, ndipo alijichukulia sheria mikononi na kutekeleza mauaji hayo,” amesema Kuzaga.
Amedai mtuhumiwa alitumia panga kumshambulia Merry na kusababisha kutokwa damu nyingi iliyokuwa sababu ya kifo.
Katika hatua nyingine, Kuzaga ameonya jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi kutokana na migogoro ya kifamilia kwa kugombea mali badala yake kutafuta njia mbadala ya kupata mwafaka.
“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa baadhi ya vijana kuacha tamaa ya kujipatia mali kinyume cha sheria na kueleza kuwa mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa kwa uchunguzi zaidi na atafikishwa mahakamani wakati wowote,” amesema Kuzaga.
Baadhi ya wakazi wamekemea kitendo hicho cha mauaji na kuliomba Jeshi la Polisi kufanya mahojiano zaidi na mtuhumiwa huenda lengo la tukio hilo halikuwa mgogoro wa mashamba.
Telezia Joel, ameshauri Serikali kuweka mfumo wa utoaji elimu kwa makundi rika sambamba na wanaoingia kwenye ndoa.