Watu wengi hawapendi kusema ukweli kwa kuogopa kuchafua hadhi yao. Wengine hufanya hivyo kwa kuhofia kukaribisha ushindani; hasa kwenye kipato na biashara. Ni vigumu sana kwa mtu aliye na mafanikio kidogo kwenye mzunguko wa fedha kukupa siri halisi ya mafanikio yake. Zaidi anaweza kukutafutia simulizi ya kufikirika inayoweza kukutoa machozi, lakini mwisho abaki kuwa shujaa.
Miaka mingi iliyopita nilishiriki kwenye sherehe ya harusi ya mjomba wangu. Alimuoa binti wa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (wakati huo kilikuwa pale Mlimani tu).
Adhimisho lilifanyika mjini, likafuatiwa na sherehe kule Msasani Beach Club. Ulikuwa ni msimu wa mvua za mwisho wa mwaka, hivyo Dar ya wakati ule ilikuwa ya kutisha sana.
Sote tulishangaa tulipopitishwa kwenye barabara ya zamani, iliyokuwa na madimbwi mwanzo mwisho. Kumbe mzee wetu alikuwa na jambo lake. Alikuwa akitafuta mifano halisi katika usia kwa binti yake. Wakati ulipojiri alituambia alitupitisha katika njia ile ili binti akumbuke: maisha ni safari ngumu, si barabara ya lami. Hivyo aende kuishi na mumewe kwa kuvumiliana na kusaidiana.
Kiujumla mzee hakuwa akiongea na bintiye pekee. Hadhira nzima iliguswa na ujumbe wake.
Nadhani japo nilikuwa mdogo wakati ule, lakini naamini nilikuwa ni miongoni mwa walioguswa zaidi.
Hadi hivi leo maneno yale yanaishi rohoni mwangu, ninaamini hakuna linaloshindikana chini ya jua. Hata nikutanapo na maumivu, najipa moyo kuwa safari ingali inaendelea.
Maneno ya mhamasishaji humtia moyo mtu anayepambana kutafuta unafuu. Lakini mtu huyu anaweza akakata tamaa iwapo atasikiliza kila neno. Duniani kuna mabingwa wa kutia moyo, na kila mmoja ana njia zake. Yupo aliyehadithia jinsi alivyopambana mpaka kumiliki kiwanda cha mikate.
Alisema: “Nilianza na mkate mmoja… nikaukata vipande vidogo na kuviuza kwenye mageti ya shule…”
Kwa bahati mbaya, mmoja wa wasikilizaji wake aliikopi simulizi hiyo na kwenda nayo mtaa wa pili: “Mimi nilianza na mchele mmoja, sasa ninaendesha duka la mchele…”
Kama hajui kuongopa ni bora awaachie wenyewe fani yao. Mtu huyu anaweza kuwaimbisha kwamba alianza na tone moja la maji, na sasa anamiliki kiwanda cha kusindika maji! Ni kweli hakuna kinachoshindikana, ila sio kwa hili…
Kama nilivyotangulia kusema, wengi wanaelezea mafanikio yao katika njia chanya tu. Sio vibaya kwani hatupendi watu waige mabaya yao. Lakini kuujua ukweli si dhambi. Si vibaya kujua hata changamoto zilizoshindikana kukwepeka na kumdondosha mtarazaki. Pengine aliwahi kujikuta katika wakati mgumu na hata kuingia kifungoni kwenye mapambano yake, na kadhalika.
Waswahili husema makundi ya watu wakweli ni matatu: watoto, wazee na wagonjwa. Hawa huwa hawana sababu za kuficha ukweli. Watoto hawajui dhambi, na wazee pamoja na wagonjwa huwa hawana cha kupoteza kutokana na ukweli.
Labda hapa linaweza kuongezeka kundi la watu waliokwisha kujikubali na kutubu. Wapo waliokubali makosa na wakatumikia vifungo magerezani.
Mmoja wao alitubu kuwa alipofilisika akaingia shambani kuanza kilimo cha zao la mtama. Hakupata ahueni, shida ikamuelekeza kwenye udanganyifu. Alinyunyizia maji kwenye mazao kila alipoyapeleka sokoni.
Mzani ulisoma uzito mkubwa, hivyo alipata pesa haramu kabla ya kushtukiwa na kufungwa. Alipomaliza kifungo akarudi shambani kwa msaada wa ndugu na marafiki wa zamani, akafanikiwa.
Kufeli ni sehemu ya mafanikio, kwa sababu unapita kwenye mafunzo ya uzoefu wa kile unachokifanya.
Waliogundua umeme walifeli mara nyingi, wakarekebisha makosa hadi kufanikiwa. Tajiri Bill Gates anaelezea wazi jinsi alivyofeli darasani na kufanikiwa kwenye uzalishaji. Shida yangu ni mimi kutambua kuwa kuna mahala wanapindisha stori ili kuzilinda statasi zao.
Kadhalika Serikali yetu inapaswa kuyakiri mapungufu yake. Kwenye kampeni yanaelezewa mafanikio matupu bila kutaja hata jambo moja lililokwama. Iwapo wangeyaweka wazi maeneo waliyoyashindwa, ingewasaidia watafiti wetu kurekebisha njia na kwenda kwenye mapito sahihi. Eneo moja nitakalolitolea mfano ni katika sekta ya afya.
Humu kuna sintofahamu nyingi lakini nitasema chache sana.
Serikali ilisimamia suala la uzazi wa mpango. Baadhi ya wananchi hasa wa kimila walikataa waziwazi hadi walipolazimishwa.
Lakini leo tunaambiwa na wataalamu kuwa asilimia kubwa ya wanawake wenye changamoto ya uzazi na hedhi, ni wale walioshiriki utaratibu wa uzazi wa mpango.
Hili ni jambo mtambuka, likiwekwa wazi litatusaidia kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo kansa kwa kinamama.
Pia tuliona watu wakikataa kuzingatia chanjo ya korona. Walisikia tetesi kuwa baadhi ya waliochanjwa huko nje waliathirika.
Baada ya kulazimishwa, tuliona matokeo yake kwa baadhi ya waliochanjwa. Ukweli unaweza kutupa nguvu ya kufanya tafiti zetu wenyewe kwenye chanjo za watoto, ambazo kwa sasa ni lazima.
Je, tumezichunguza kwa makini kwamba hazitakuwa na athari kwa baadaye?
Ni lazima tutumie akili zetu kuwasalimisha watu wetu. Tunayo malalamiko mengi kuhusu huduma za afya kuzidisha ugonjwa au kupandikiza magonjwa mapya.