Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Cecilia Paresso amewaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kwenda kumpigia kura mgombea urais kupitia chama hicho, Samia Suluhu Hassan kwa kuwa anatosha.
Paresso aliyewahi kuwa mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha, ameyasema hayo katika mikutano ya kampeni za mgombea mwenza wa urais wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi iliyofanyika leo Jumatano, Oktoba 8, 2025 katika visiwa vya Pemba na Unguja.
Kada huyo ambaye ni miongoni mwa wanaounda timu ya Dk Nchimbi aliyetua Zanzibar kusaka ushindi wa Samia wa urais wa Tanzania, Dk Hussein Mwinyi wa Zanzibar, wabunge na wawakilishi.
“Tunatambua huu ni mwaka wa uchaguzi, CCM kimetuletea viongozi wenye sifa za kipekee na kwenye nafasi ya urais, imetuletea mwana mama mzalendo, mpambanaji na shupavu kwelikweli.
“Chama kimemleta ili tumchague kwa kumpigia kura. Katika kazi kubwa aliyoifanya kwa miaka minne na nusu ni udhibitisho kuwa anatosha na kina mama tuna jambo letu Oktoba 29,” amesema Paresso na kuongeza:
“Tukampigie kura za kishindo na za heshima. Kina baba na vijana nanyi twendeni tukapige kura kwa Samia, Dk Mwinyi, wabunge na madiwani wote ili kwa pamoja hii timu ikatuletee maendeleo.”
Pia, Pareso amewaomba Wazanzibar kumwamini tena Dk Mwinyi kwani amefanya kazi kubwa kama iliyofanywa na Rais Samia: “Kazi iwe moja tu kuwachagua tena waendelee kutuongoza.”
T. Wafanyakazi tumeshuhudia mageuzi ya kweli
Mbunge Mteule wa Viti Maalum (Kundi la Wafanyakazi), Halima Nassor, amemshukuru mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan kwa kuwapigania wafanyakazi nchini na kuleta matumaini mapya baada ya miaka kadhaa bila nyongeza ya mishahara.
Akizungumza leo Jumatano, Oktoba 8, 2025 katika mkutano wa kampeni za urais za CCM uliofanyika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza, Halima amesema wafanyakazi nchini walikaa takribani miaka sita bila nyongeza ya mishahara, lakini chini ya uongozi wa Rais Samia wamepata ongezeko la asilimia 35.1, jambo aliloeleza kuwa ni “ishara ya utu na uongozi unaowajali watumishi wa umma.”
“Tulikuwa na takribani miaka sita hatujawahi kupata ongezeko la mishahara, lakini chini ya Rais Samia ametuongezea asilimia 35.1. Sisi wafanyakazi tumehamasika, umetuletea matumaini kwa kiasi kikubwa. Tunakuunga mkono na tutakupigia kura,” amesema Halima.
Akimuelezea Samia kama kiongozi mwenye heshima na moyo wa utu, Halima aliongeza kuwa wafanyakazi watajibu kwa uaminifu na uwajibikaji mkubwa katika kazi zao, wakionesha shukrani kwa vitendo kwa maendeleo yaliyofikiwa.
“Mama umetupa haki zetu, nasi tutakulipa kwa kufanya kazi kwa bidii na uaminifu mkubwa. Tunakwenda kukuchagua Oktoba 29 kwani vitendo vyako vinaleta matumaini kwetu,” amesema huku akipiga magoti kuomba wananchi kumpa kura Samia.