Dar es Salaam. Baada ya Serikali ya Marekani kuiweka Tanzania miongoni mwa nchi ambazo raia wake hupaswa kufuata utaratibu wa dhamana ya viza kuingia nchini humo, Serikali imesema itaendelea na majadiliano na nchi hiyo kidiplomasia kutafuta suluhu.
Suluhu hiyo ni yenye usawa, heshima na masilahi ya pande zote mbili kwa kuzingatia uhusiano mzuri wa nchi hizo mbili uliodumu kwa zaidi ya miongo minne.
Leo Oktoba 8,2025 Serikali ya Marekani imetangaza uamuzi huo ikitaja mataifa ambayo raia wake watalazimika kuweka viza zao kama dhamana watakapolitembelea Taifa hilo.
Nchi hizo ambazo zitapaswa kufuata utaratibu huo ni Tanzania, Mauritania, Mali,
Sao Tome, Gambia, Malawi na Zambia.
Utaratibu huo utahusisha raia wa mataifa hayo watakaokwenda Marekani kufanya biashara au shughuli za utalii.
Utekelezaji wa utaratibu huo mpya wa Marekani kwa mataifa hayo, utaanza Oktoba 23,2025 na tayari Serikali ya Tanzania pamoja na kueleza hatua inazochukua, imewataka wananchi wake kuyatekeleza masharti hayo.
Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Oktoba 8,2025 na Serikali ya Tanzania kupitia kwa Msemaji wake, Gerson Msigwa, imeeleza kuwa uamuzi huo umefikiwa wakati majadiliano kuhusu masuala ya uhamiaji yakiendelea baina ya mataifa hayo mawili.
“Pamoja na hatua ya Marekani kutangaza kuanzisha utaratibu wa dhamana za viza kwa raia wa Tanzania watakaoomba viza tajwa hapo juu. Serikali inapenda kuuhakikishia umma kwamba, itaendelea na majadiliano hayo na Serikali ya Marekani kwa njia za kidiplomasia ili kutafuta suluhisho lenye kuzingatia usawa, heshima, na masilahi ya pande zote mbili kwa kuzingatia uhusiano wetu mzuri uliodumu kwa zaidi ya miongo minne,”amesema.
Msigwa kupitia taarifa yake amesisitiza kuwa uhusiano wake na Marekani umejengwa katika misingi ya urafiki, ushirikiano, na kuheshimiana kwa muda mrefu, na hivyo hatua hiyo haitabadilisha dhamira ya Tanzania ya kuendeleza uhusiano mzuri na nchi niyo kwa manufaa ya pande zote.
“Kwa sasa, wananchi wanaombwa kuendelea kufuata taratibu za kawaida za maombi ya viza kupitia ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, na popote ambapo Mtanzania muombaji wa viza husika atakuwepo.
“Serikali itatoa taarifa zaidi kuhusu suala hili pindi mazungumzo yanayoendelea yatakapofikia hatua nyingine,”taarifa hiyo imeeleza.
Marekani katika taarifa yake imeeleza kuwa raia au mtu yeyote mwenye uraia wa nchi kati ya zilizoorodheshwa, ambaye atastahili kupata viza ya B1/B2, anatakiwa kuweka dhamana ya dola za Marekani 5,000, 10,000 au 15,000.
Kiwango hicho cha dhamana kitaamuliwa wakati wa mahojiano ya maombi ya viza.
“Mwombaji atatakiwa kujaza fomu ya idara ya usalama wa ndani (Department of Homeland Security) yenye namba I-352 na waombaji lazima wakubaliane na masharti ya dhamana hiyo kupitia malipo watakayopaswa kufanya kwa njia ya mtandao idara ya hazina ya Marekani, sharti hili litatumika bila kujali sehemu au nchi ambayo mwombaji anaomba viza,”taarifa hiyo imefafanua.
Marekani imefafanua kuwa masharti kwa waombaji wote wa viza ambao wameweka dhamana ya viza wanapaswa kuingia na kutoka Marekani kupitia vituo maalumu.
Kutozingatia masharti hayo kutasababisha muhusika kukataliwa kuingia nchini humo au kuondoka bila kurekodiwa ipasavyo.
Maeneo yaliyoainishwa kuwa ndiko wahusika watapita au kutumia ni uwanja wa ndege wa kimataifa wa Boston Logan (BOS),uwanja wa ndege wa kimataifa wa John F. Kennedy (JFK) na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Washington Dulles (IAD).