Serikali ya CCM Itaendelea Kuboresha Huduma za Maji, Elimu na Afya – Global Publishers

Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Misungwi katika muendelezo wa muendelezo wa Kampeni za Uchaguzi kwa CCM, mkoani Mwanza tarehe 07 Oktoba, 2025.

Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali ya CCM haitakuwa na mwisho katika kuboresha huduma muhimu za kijamii kama maji, elimu na afya, akisisitiza kuwa maboresho hayo yataendelea sambamba na ongezeko la watu na mahitaji yao.

Akihutubia Jumanne, Oktoba 7, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Viwanja vya Nyamatala, wilayani Misungwi, mkoani Mwanza, Dkt. Samia alisema Serikali yake itaendelea kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora na kwa ukaribu zaidi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya muda mrefu ya CCM ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

Sehemu ya Wananchi wa wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza waliohudhuria mkutano wa hadhara wa Kampeni wa Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 07 Oktoba, 2025.

Katika hotuba yake, Dkt. Samia alitolea mfano sekta ya maji katika mji wa Misungwi, akibainisha kuwa Serikali imetoa shilingi bilioni 8.88 kwa ajili ya kupanua mtandao wa maji wa kilomita 38.

Mradi huo unahusisha ujenzi wa matenki mawili — moja lenye ujazo wa lita 150,000 na jingine lita 90,000 — katika kata za Misungwi na Igokelo, ili kusambaza maji kwenye maeneo ya mwinuko kama Mbela, Mwambola, Ng’ombe, Iteja na Mwamanga.

Amesema utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 87, na kukamilika kwake kutawanufaisha zaidi ya wananchi 22,482.

Aidha, Dkt. Samia alizungumzia utekelezaji wa miradi ya maji vijijini, ikiwemo miradi 10 yenye thamani ya shilingi bilioni 65, ikijumuisha mradi mkubwa wa Ikiliguru unaotarajiwa kuhudumia vijiji 19 vya kata za Usagara, Ukiliguru na Kolomije.

Katika utekelezaji wa mradi huo, tanki la ujazo wa lita milioni 1.5 limekamilika katika kata ya Usagara, huku tanki lingine la lita milioni 2 likiendelea kujengwa katika kata ya Ukiliguru, miradi hiyo ikitarajiwa kuwanufaisha zaidi ya wananchi 85,500.

Ametaja pia mradi wa maji wa Ilijamata, unaotarajiwa kuhudumia vijiji 16, akiahidi kuwa endapo atapewa ridhaa ya kuunda Serikali, atakamilisha miradi yote ya maji kwa wakati, sambamba na kushughulikia changamoto za miundombinu ya usambazaji maji mkoani Mwanza na wilayani Misungwi.