Serikali yaweka mkakati matumizi ya umeme kufikia Dira ya 2050

Dodoma. Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amekutana na wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango kujadili utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya sekta ya nishati kwa ajili ya kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Msingi wa kikao hicho ni kutambua sekta ya nishati kama moja ya vichocheo vitano muhimu vitakavyoharakisha utekelezaji wa Dira hiyo.

Mramba amesema kwa kuwa upatikanaji wa nishati ya uhakika ni nyenzo ya maendeleo ya viwanda, shughuli za kiuchumi na uboreshaji wa maisha ya wananchi kwa kutoa ajira na kuchochea maendeleo endelevu.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma jana Jumanne, Oktoba 7, 2025 na kushirikisha taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Nishati, Mramba amesema pande hizo mbili zimejipanga kuimarisha uratibu wa miradi ya nishati ili iendane na vipaumbele vya kitaifa vya maendeleo.

“Wizara ya Nishati inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo mradi wa kusafirisha umeme wa kV 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma, unaotarajiwa kukamilika Juni 2026. Mradi huu utaboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika mikoa ya Katavi, Kigoma na maeneo mengine yenye changamoto za upatikanaji wa nishati thabiti,” amesema.

Aidha, ameongeza kuwa kukamilika kwa miradi ya kimkakati kutawezesha kufanikisha moja ya malengo ya Dira 2050, ambayo inalenga kuongeza matumizi ya umeme kufikia wastani wa uniti 3,000 kwa kila mtu kwa mwaka.

“Tunataka Tanzania iwe na nishati ya uhakika, nafuu na safi kwa wote. Serikali inakaribisha sekta binafsi kuwekeza kwenye miradi hii kwani mafanikio ya sekta ya nishati yanategemea ushirikiano wa wadau wote,” amesisitiza Mramba.

Katika kikao hicho, Wizara iliwasilisha pia taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi ya gesi asilia, mafuta, nishati safi ya kupikia, umeme na nishati mbadala.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mtendaji – Menejimenti ya Utendaji na Tathmini, Dk Linda Ezekiel, amepongeza ushirikiano wa karibu kati ya Wizara ya Nishati na Tume ya Taifa ya Mipango, akieleza kuwa mwelekeo wa miradi hiyo unaendana kikamilifu na malengo ya Dira 2050.

“Tume itaendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi hii ili kuhakikisha inachangia moja kwa moja katika ukuaji wa uchumi, ustawi wa wananchi na uhifadhi wa mazingira,” amesema Dk Ezekiel.

Amesema Dira ya 2050 inalenga kuwa na Taifa lenye uchumi wa kisasa, shindani na jumuishi na sekta ya nishati ndiyo mhimili wa kufanikisha hilo.

Wizara ya Nishati na Tume ya Taifa ya Mipango zimekubaliana kuendelea kushirikiana kwa karibu katika upangaji, utekelezaji na ufuatiliaji wa miradi yote ya nishati ili kuhakikisha Tanzania inafikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa ufanisi.