Mogadishu. Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, ametangaza kuwa Serikali yake inajiandaa kuanzisha lugha ya Kiswahili katika mtaala wa shule za kitaifa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kikanda ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Rais Mohamud alitoa kauli hiyo jana, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Afrika Mashariki (EACCON) uliofanyika mjini Mogadishu, na kuhudhuriwa na mamia ya wajumbe kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika Mashariki.
“Vyuo vikuu vya nchi, hasa Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Somalia, vinapaswa kuzingatia kukuza Kiswahili ambacho ni lugha ya Afrika Mashariki,” amesema Rais Mohamud, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa kuimarisha utambulisho wa kikanda na mawasiliano ya pamoja.
Ameongeza kuwa baada ya Somalia kujiunga rasmi na Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 2024, ni wajibu wa nchi hiyo kukumbatia Kiswahili kama sehemu ya urithi wa pamoja wa kanda.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Farah Sheikh Abdulkadir, amesema Serikali inashirikiana na taasisi za kikanda kuandaa mfumo wa kufundisha Kiswahili katika ngazi zote za elimu.
“Tunataka Kiswahili kiwe lugha ya mawasiliano, biashara na elimu nchini Somalia, na hatimaye kuchukua nafasi kubwa katika mikutano yetu ya kitaifa,” amesema waziri huyo.
Somalia, ambayo sasa ni mwanachama wa nane wa EAC baada ya Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), tayari ina maelfu ya wananchi wanaozungumza Kiswahili, hasa kutokana na mwingiliano wa muda mrefu na nchi jirani za Afrika Mashariki.