Tanzania kutumia data, teknolojia kupambana na NCDs

Dar es Salaam. Tanzania imepiga hatua kubwa katika kukabiliana na changamoto inayoongezeka ya magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) kwa kutumia takwimu na teknolojia hali inayosaidia kuanza kubaini wagonjwa mapema.

Wakati magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu, saratani, na magonjwa ya moyo yakiongezeka miongoni mwa jamii ya Watanzania, Serikali kwa kushirikiana na wadau wanabuni mbinu mpya kidijitali kupambana nayo.

Hayo yalibainishwa katika mdahalo maalumu kando ya Mkutano wa 12 wa Afya Tanzania, chini ya mada kuu “Kutumia takwimu na teknolojia za NCDs kuongeza kasi ya utekelezaji wa huduma za afya kwa wote (UHC) kupitia huduma za afya za msingi.”

Akiwasilisha mada kuhusu mfumo wa GoT-HoMIS, Geofrey Mwakijungu kutoka Chama cha Kisukari Tanzania (TDA) alisema mfumo huo umesaidia kubadilisha huduma za kisukari na shinikizo la damu nchini.

Mwakijungu alionyesha jinsi mfumo wa kidigitali wa GoT-HoMIS unavyorahisisha ufuatiliaji wa wagonjwa na ukusanyaji wa takwimu.

Mfumo huu, ulioboreshwa kwa ushirikiano na Wizara ya Afya, umeanza kutekelezwa katika mikoa ya Pwani na Lindi na unakusanya taarifa za wagonjwa wa kisukari na shinikizo la damu kwa njia ya moja kwa moja.

“Mfumo huu wa kidigitali unarahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wakati, unarahisisha maamuzi ya kitabibu, na unapunguza muda wa uandikaji wa mikono. Tunajipanga kuusambaza nchi nzima,” alisema Mwakijungu.

Alisema GoT-HoMIS sasa umeunganishwa na mfumo wa kitaifa wa DHIS2, na unatarajiwa kusaidia kuanzisha rejesta ya kisukari aina ya kwanza (Type 1 Diabetes Registry) nchini.

Kulingana na takwimu za Shirikisho la Kisukari Duniani (IDF, 2024), asilimia 9.8 ya Watanzania wazima wanaishi na kisukari, ongezeko kubwa kutoka asilimia 1.6 mwaka 1984.

Nchini Tanzania, magonjwa yasiyoambukiza yanachangia takribani asilimia 40 ya miaka ya ulemavu (DALYs) na asilimia 33 ya vifo vya mapema.

Akizungumzia ujenzi wa uwezo kupitia mafunzo ya kidigitali, Meneja wa Programu TDA Dk Rachel Nungu, aliwasilisha jinsi chama hicho kinavyowajengea uwezo watoa huduma za afya kupitia majukwaa ya mafunzo mtandaoni.

“Hadi sasa, watoa huduma zaidi ya 6,000 kutoka vituo 924 wamefundishwa kuhusu huduma bora za kisukari na shinikizo la damu kupitia Morogoro E-learning Hub na World Continuing Education Alliance (WCEA), ambazo zinatoa alama za CPD zinazoidhinishwa na Baraza la Madaktari na Baraza la Uuguzi,” amesema Dk Nungu.

Kwa upande wake, Shirikisho la Vyama vya magonjwa yasiyo ya kuambukiza Tanzania, TANCDA lilionyesha mafanikio katika kutumia wasaidizi wa afya ya jamii (CHWs) kukusanya takwimu za NCDs na kutoa huduma za uchunguzi wa awali.

Hayo yalifanywa kupitia mpango wa watoa huduma ngazi ya jamii 40 kufundishwa, kupima watu 1,600, kubaini wagonjwa wapya wa NCD 400, kupeleka wagonjwa 250 kwenye matibabu zaidi.

“Ushirikishwaji wa jamii ni msingi wa kufanikisha huduma jumuishi za afya,” alisema Meneja wa Miradi wa TANCDA, Happy Nchimbi.

Wakati mifumo ya takwimu ya afya ikiendelea kusukwa, Serikali imeongeza bajeti ya sekta ya afya kutoka Sh2.1 trilioni mwaka 2020/21 hadi trilioni 3.1 mwaka 2025/26. Hata hivyo, asilimia 85 ya wananchi bado wanalipa gharama za afya moja kwa moja, huku walio na bima wakiwa ni chini ya asilimia 15.

Matumizi katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza yameongezeka kwa asilimia 30 kati ya mwaka 2023 na 2024, ishara ya gharama kubwa za matibabu na ongezeko la wagonjwa.

Mkutano ulimalizika kwa wito wa kuwekeza zaidi katika kinga, takwimu, ubunifu wa kidigitali, na huduma za afya za msingi kama njia bora ya kufikia UHC nchini Tanzania.

“Kila shilingi inayowekezwa katika kinga na mifumo ya takwimu inaleta faida kubwa kwa uchumi na ustawi wa wananchi,” alisema mwakilishi kutoka Wizara ya Afya.

Mkutano huo uliandaliwa na Wizara ya Afya kwa ushirikiano na Chama cha Kisukari Tanzania (TDA) na Muungano vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA), na uliwaleta pamoja wataalamu wa afya, watunga sera, na wadau wa maendeleo kujadili namna data na ubunifu wa kidigitali vinavyoweza kubadilisha mfumo wa afya nchini.