TEA, UNICEF na Serikali ya Canada Waendeleza Mageuzi ya Miundombinu ya Elimu Sikonge

Sikonge, Tabora

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) pamoja na Serikali ya Canada, wameendelea kutekeleza mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kupitia ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya shule, ukiwemo uboreshaji wa mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji katika Wilaya ya Sikonge, mkoani Tabora.

Jumla ya miradi 10 yenye thamani ya takribani shilingi milioni 284 imetekelezwa katika shule sita za msingi na sekondari wilayani humo kupitia ufadhili huo. Miradi hiyo imejumuisha ujenzi na ukarabati wa maabara, vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata elimu bora katika mazingira rafiki na salama.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua miradi hiyo, Afisa Miradi kutoka TEA, Bi. Atugonza David, alisema miradi yote iliyokuwa ikiendelea tayari imekamilika na iko tayari kuanza kutumika. Alibainisha kuwa shule husika zitakabidhiwa miradi hiyo muda wowote kuanzia sasa, kwa mujibu wa sheria na taratibu za kiserikali.

“Tumekamilisha ukarabati na umaliziaji wa maabara nane za sayansi katika shule nne, ujenzi wa matundu 10 ya vyoo katika shule moja, pamoja na umaliziaji wa vyumba vinne vya madarasa katika shule nyingine wilayani Sikonge,” alisema Bi. Atugonza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Ngulu, Mwl. Israel Mwambikwa, alisema shule yake imenufaika kwa kiasi kikubwa kupitia mradi wa ujenzi wa maabara mbili za sayansi, jambo ambalo limechangia ongezeko la hamasa kwa wanafunzi kujifunza masomo ya sayansi, hususan kwa wasichana.

“Shule yetu ina jumla ya wanafunzi 666, ambapo wasichana ni 333 na wavulana ni 333. Kwa sasa, wasichana wanafanya vizuri zaidi kwenye masomo ya sayansi ukilinganisha na wavulana. Idadi ya wanafunzi wanaochagua michepuo ya sayansi imeongezeka mara mbili ikilinganishwa na mwaka jana baada ya kukamilika kwa maabara hizi,” alieleza Mwl. Mwambikwa.

TEA iliingia makubaliano maalum na UNICEF kwa lengo la kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata fursa na haki ya elimu bora, bila vikwazo vya kimazingira.

Bi. Atugonza David akiwa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Pangale Mwl. Sengi Msaru wakati wa kukagua mradi wa ukarabati wa maabara tatu za Sayansi zilizofadhiliwa na UNICEF, CANADA kwa usimamizi wa TEA.

Muonekano wa ndani wa maabara ya Sayansi shule ya Sekondari Pangale baada ya ukarabati uliofadhiliwa na UNICEF, Serikali ya CANADA na kuratibiwa na TEA