Tumbi yasherehekea miaka 58 kwa matibabu bure ya kibingwa

Kibaha. Zaidi ya wakazi 3,000 kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Pwani na mikoa jirani wanatarajia kufikiwa na huduma ya matibabu ya kibingwa bila malipo yatakayotolewa na madaktari kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 58 tangu hospitali hiyo ianzishwe.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hizo, Muuguzi Kiongozi wa Hospitali hiyo, Joyce Mfyuji, amesema huduma hizo maalumu zinazotolewa kwa siku tatu mfululizo kuanzia Oktoba 7, 2025, katika viwanja vya Mwendapole wilayani Kibaha, zinahusisha uchunguzi, matibabu na ushauri wa kitaalamu kwa wagonjwa wenye changamoto mbalimbali za kiafya.

Mfyuji ametaja huduma hizo ni matibabu ya magonjwa ya mifupa, huduma za macho, afya ya uzazi kwa wanawake, pamoja na uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi.

Amebainisha kuwa lengo ni kuwafikia wananchi wengi zaidi, hasa wale wanaoshindwa kugharamia huduma hizo katika hospitali binafsi au za mbali.

“Wananchi wanapata vipimo, matibabu na ushauri wa kibingwa bila malipo. Ni njia yetu ya kushiriki katika kuboresha afya za wananchi na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya kwa wote,” amesema Mfyuja.

Baadhi ya wananchi waliopata huduma hizo wameelezea furaha yao kwa hospitali kuwasogezea huduma hizo karibu na makazi yao, wakisema imewapunguzia gharama kubwa za matibabu na usafiri.

“Huduma hizi zimeniokoa pesa nyingi. Tulikuwa tukisafiri hadi Muhimbili kwa vipimo vya kibingwa, lakini leo tumepata bure hapa hapa Kibaha,” amesema Nuru Nandi.

Amida Ezekiel na Mussa Mwaimu nao waliiomba Serikali na wadau wa sekta ya afya kuhakikisha huduma kama hizo zinatolewa mara kwa mara, wakisema zina msaada mkubwa kwa wananchi wa kipato cha chini.

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi, iliyoanzishwa mwaka 1967, imeendelea kuwa kimbilio kwa wagonjwa wengi hususan majeruhi wa ajali za barabarani kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutoa huduma za dharura, upasuaji na uangalizi maalumu (ICU).

Kwa sasa, hospitali hiyo ni moja ya vituo vinavyoongoza kwa huduma za kibingwa nchini, ikijumuisha afya ya uzazi, magonjwa sugu, maabara, radiolojia na ushauri wa kisaikolojia.