Dar es Salaam. Magari kwa ajili ya matumizi ya nyumbani yanashika namba nane katika orodha y bidhaa ambazo Tanzania inaagiza sana kutoka nchi za nje, Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza.
Kuongezeka huo kwa uingizaji wa magari kunatajwa na wataalamu wa uchumi kuchangiwa na ukuaji wa kipato cha mtu mmojammoja hadi kufikia kiwango cha kuweza kumudu mahitaji mengine nje ya yale muhimu kama chakula, malazi na mavazi.
Haya yanaelezwa wakati ambao ripoti ya tathmini ya hali ya uchumi ya Septemba mwaka huu iliyotolewa na BoT kuonyesha kuwapo kwa ongezeko la zaidi ya mara mbili la fedha zinazotumika kununua magari katika mwaka ulioishia Agosti mwaka huu, ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2021.
Takwimu zinaonyesha hadi kufikia Agosti, 2025 uagizaji wa magari ulitumia Sh1.002 trilioni katika ikilinganishwa na Sh492.88 bilioni zilizotumika katika kipindi kama hicho mwaka 2021.
Magari yanatajwa kuwa moja ya bidhaa ambayo imechochea kuongezeka kwa matumizi ya fedha za kigeni katika kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi, ikitanguliwa na vifaa vya viwandani vilivyokuwa na thamani ya Sh12.443 trilioni hadi kufikia Agosti mwaka huu.
Bidhaa za mafuta ya petroli zilishika nafasi ya pili zikitumia Sh6.17 trilioni, shehena za mizigo zilikuwa na thamani ya Sh3.187 trilioni, spea mbalimbali Sh2.827 trilioni, mitambo ya usafirishaji viwandani Sh2.821 trilioni, mashine na mitambo Sh2.654 trilioni.
“Unajua kwa tulipofikia sasa magari siyo kitu cha anasa tena, ni hitaji muhimu kwa watu wengi hususani wafanyakazi, kuna kiwango cha maisha ukifika unakuwa hauna budi kuwa na usafiri wako kwa ajili ya kukusaidia kutoka sehemu moja kwenda nyingine,” amesema Ramadhan Juma mfanyakazi katika moja ya kampuni za uagizaji wa magari.
Amesema tofauti na zamani ambapo walihitaji nguvu kubwa kuwashawishi watu kununua magari, siku hizi watu wametambua umuhimu wake huku wao wakiwapa nafasi ya kulipa kidogokidogo ili waweze kukamilisha ndoto zao.
“Unampa kianzio labda asilimia 20 hadi 40 wengine 50 ya gharama ya gari husika halafu unamuachia aendelee kulitumia huku akileta marejesho kila mwezi, wengine wanataka ukae na gari hadi wakimaliza kulipia ndiyo achukue, ni namna tu ya kuhakikisha wote wenye uhitaji wanapata,” alisema.
Wataalamu wa uchumi wanatafsiri ongezeko la ununuaji wa magari kwa ajili ya kaya kama moja ya kiashiria cha kukua kwa kipato cha mtu mmoja mmoja.
Mtaalamu wa uchumi na Biashara, Dk Donath Olomi amesema hiyo ni kiashiria cha kukua kwa uchumi wa watu japokuwa si lazima uwe umegawanyika kwa watu wote.
“Si lazima uchumi uwe umegawanyika kwa watu wote ndiyo hivyo watu wenye uwezo wanaweza kununua magari, kama ambavyo watu wengine wanajenga nyumba za bati, wanatumia tofali za saruji, wanatumia vigae badala ya bati,” amesema.
Amesema hadi mtu anafikia hatua ya kununua gari ni dhahiri kuwa tayari ameweza kumudu mahitaji mengine ya muhimu na ziada ya fedha inayobaki anaamua kutafuta usafiri.
Maneno yake yaliungwa mkono na Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora aliyesema jambo hilo linahusiana na ukuaji wa uchumi kwani watu hawawezi kumiliki vyombo vya moto kama hawana uwezo wa kumudu mahitaji mengine.
“Mtu hawezi kulala njaa halafu akanunua gari, uchumi wa mtu mmoja mmoja unaonyesha kuwa kila mtu anataka kutumia gari zuri, kuishi vizuri, kusafiri na ndege lakini tunashindwa kwa sababu hela hatuna hivyo inapotokea mtu anapata hela ni lazima atafanya kile alichokuwa akihitaji,” amesema.
Amesema uwezo huu wa watu kumudu magari ni ishara kuwa shughuli za kujiingizia kipato wanazofanya zinazaa matunda wakati ambao mazingira mazuri ya ufanyaji biashara yamewekwa.