Wakulima kunufaika fursa uuzaji mbaazi India

Dodoma. Tanzania inaendelea na jitihada za kutafuta masoko kwa ajili ya zao la mbaazi na sasa imeanzisha mazungumzo na  Serikali ya India ili inunue zao hilo ambalo linazalishwa kwa wingi na wakulima hapa nchini lakini bei yake haina faraja kwa wazalishaji.

Katika taarifa iliyotolewa na jana Oktoba 7, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Irene Mlola, amesema mazungumzo yao yanakwenda vizuri na kwamba wanaimani kuwa wakulima wa nchi hii sasa wanakwenda kuneemeka.

Mlola amesema kuwa mazungumzo na Serikali ya India yalifanyika wakati wa ziara ya kikazi nchini humo ambapo ujumbe wa Tanzania ulikwenda kushiriki maonesho ya World Food India 2025 yaliyofanyika jijini New Delhi nchini India.

Amesema katika msimu wa mwaka huu, matarajio katika uzalishaji wa mbaazi nchini Tanzania ni kuwa na zaidi ya  tani 400,000, hivyo Serikali inachukua hatua kuhakikisha inapata soko la uhakika ili kuunga mkono juhudi za wakulima na maandalizi hayo yanafanyika mapema.

Mkurugeni huyo amebainisha kuwa Serikali ipo kwenye mazungumzo na Serikali ya India ili inunue mbaazi za Tanzania kwenda moja kwa moja kwenye hifadhi ya chakula ya nchi na kuchangia uhakika wa chakula katika Taifa hilo ambalo ndiyo soko kuu la kutegemea katika zao la mbaazi.

“Nawapongeza wakulima kwa kazi nzuri ya uzalishaji wa mazao shambani, nchi yetu imeshika nafasi ya pili duniani kwa uzalishaji wa  zao la mbaazi ambapo katika msimu wa mwaka jana  Tanzania  ilisafirisha takriban tani 350,000 kwenda nchini India,” inasema sehemu ya taarifa ya Mlola.

Katika taarifa hiyo inamnukuu Balozi wa Tanzani nchini India, Anisa Mbega  akisema mazungumzo hayo ni mwendelezo wa kazi iliyoanzwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara ya kikazi nchini humo Oktoba 2023.

Balozi Mbega amefafanua kuwa katika ziara hiyo, Rais Samia alikutana na Waziri Mkuu wa India na kuimarisha biashara kati ya nchi hizi mbili ambazo kwa sasa kimekua na kufikia jumla ya Dola za Kimarekani 8.6 bilioni kwa mujibu wa Takwimu za mwaka 2024/25.