Adaiwa kumuua mkewe kwa kuchelewa kurudi nyumbani

Shinyanga. Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia Chimaguli Samamba (54) ambaye ni mkulima na mkazi wa Kitongoji cha Ugede Kijiji cha Songambele, Tarafa ya Nindo, Wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga kwa tuhuma za kumuua mkewe Moshi John (47) kisha mwili wake kuufukia kwenye shimo la choo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 9, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi ameeleza kuwa katika uchunguzi uliofanyika, ugomvi ulianza baada ya Moshi kuchelewa kurudi nyumbani akitoka matembezini.

Pia, Kamanda Magomi amedai kuwa, “Baada ya mtuhumiwa kubaini mkewe amepoteza maisha, alichukua mwili na kuupeleka nje ya nyumba na kuutupa kwenye shimo lililokuwa likichimbwa kwa matumizi ya choo na kuufukia.”

Hata hivyo Magomi ameeleza kuwa majirani walianza kupata wasiwasi baada ya kutokumuona Moshi kama walivyozoea, lakini kutokana na tabia ya mumewe ya kumpiga mara kwa mara hivyo wakaanza kufuatilia na Oktoba7, 2025 taarifa zikafikishwa kwa mwenyekiti wa kitongoji na baada ya mtuhumiwa kuhojiwa alikana kuhusika na uhalifu wowote dhidi ya mkewe.

Jana, Oktoba 8, 2025 saa tano asubuhi taarifa zilifika Kituo cha Polisi Salawe, na polisi walifika nyumbani hapo na kumkamata mtuhumiwa kwa mahojiano ya awali. Kamanda Magomi amedai mtuhumiwa alikiri kumuua mkewe na kumfukia kwenye shimo la choo lililopo nyumbani kwake.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Songambele, Lazaro Enock ameeleza kuwa baada ya polisi kufika eneo la tukio na kufanya mahojiano na mtuhumiwa walishikiriana na wananchi kuufukua mwili huo na kuupeleka katika Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga kwa uchunguzi zaidi.