Bajaber azua jambo Simba, kikosi chavurugika

WANASIMBA wana hamu kubwa sana ya kumuona nyota wao mpya, Mohammed Bajaber akikanyaga nyasi za uwanjani na kucheza mechi ya mashindnao msimu huu.

Hamu hiyo inakuja kwani katika mechi tano za mashindano ilizocheza Simba msimu huu, kiungo wake mshambuliaji Mohammed Bajaber hakuonja hata dakika moja, hiyo imetokana na majeraha ya nyama za paja yaliyokuwa yakimsumbua tangu atue kikosini hapo.

Sasa basi kitendo cha Bajaber kupona majeraha yaliyomuweka nje kwa muda mrefu na sasa kurejea kwenye uwanja wa mazoezi, kimemfanya kiungo huyo wa eneo la ushambuliaji kuibua maswali ya nani atang’oka katika kikosi cha kwanza cha Simba ili aingie kuonyesha mavitu yake.

Hiyo imetokana na msimu huu wachezaji tegemeo wa Simba wanaocheza katika eneo hilo kuanza taratibu tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita. Wachezaji hao ni Elie Mpanzu, Kibu Denis na Joshua Mutale.

BAJA 01

Bajaber aliyesajiliwa na Simba msimu huu akitokea Kenya Police, hajacheza mechi yoyote kutokana na majeraha ya nyama za paja yaliyokuwa yakimsumbua, lakini sasa amepona na anafanya mazoezi ya nguvu na wenzake kambini.

Nyota huyo aliyetoka kuipa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya timu ya Kenya Police chini ya kocha Etienne Ndayiragije, ameanza mazoezi na timu hiyo ikiwa ni ishara nzuri ya kucheza baada ya kukaa nje ya uwanja kwa muda.

Bajaber alikuwa anasumbuliwa na majeraha akiwa kambini na timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars, iliyokuwa inajiandaa na Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN 2024), zilizofanyika Tanzania, Kenya na Uganda.

Hata hivyo, wakati akiwa kambini na kikosi hicho, Bajaber aliondoka mapema kabla ya michuano hiyo kuanza Agosti 2, 2025 na kujiunga na Simba, ambayo pia licha ya dili hilo kukamilika, nyota huyo hakucheza mechi yoyote ya kimashindano.

BAJA 02

Nyota huyo mwenye miaka 22 aliyejiunga na Kenya Police, Februari mwaka huu akitokea Nairobi City Stars, ana uwezo wa kucheza katika wingi zote mbili kulia na kushoto sambamba na nyuma ya mshambuliaji jambo linalosubiriwa na mashabiki wa Simba kuuona uwezo wake.

Wakati Bajaber akisubiriwa, miongoni mwa nyota wanaocheza nafasi hiyo kwa sasa katika kikosi cha Simba ni Elie Mpanzu ambaye hivi karibuni baadhi ya mashabiki wa timu hiyo wamekuwa hawaridhishwi na kiwango chake. Mwingine ni Kibu Denis.

Kwa upande wa Joshua Mutale aliyekuwa katika hatari ya kukatwa tangu msimu uliopita kabla ya kubadili upepo hasa mechi za mwishoni za Kombe la Shirikisho Afrika, pia ana uwezo wa kutokea pembeni na kucheza nyuma ya mshambuliaji hali inayoongeza ushindani zaidi.

Kiungo mwingine ni Morice Abraham ambaye kwa sasa ameonyesha kiwango kizuri tangu ajiunge na timu hiyo akiwa mchezaji huru, baada ya kuachana na RFK Novi Sad 1921, aliyokuwa anaichezea kwa mkopo akitokea, Spartak Subotica ya kule Serbia.

BAJA 03

Kiwango cha Abraham, kimevutia mashabiki wa timu hiyo ambao wanashinikiza aendelee kuanza katika kikosi cha kwanza, badala ya Jean Charles Ahoua, ambaye licha ya msimu uliopita kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akifunga mabao 16 sambamba na kuasisti mara tisa, lakini hawaridhishwi na mwenendo wake.

Usajili mpya, Neo Maema kutoka Mamelodi Sundowns, hajaanza vizuri ndani ya Simba tofauti na wengi walivyotarajia, lakini ametoa asisti moja. Naye anacheza eneo la kiungo mshambuliaji anapoweza kucheza Bajaber.

Hata hivyo, taarifa zinaeleza Meneja Mkuu wa Simba, Dimitar Pantev, hana haraka ya kumtumia Bajaber kwa sasa na badala yake anahitaji kumpa muda wa kupona vizuri zaidi, licha ya yeye mwenyewe pia kufosi mara kadhaa kutaka kucheza.

Inaelezwa, sababu kubwa ya nyota huyo kutopona vizuri majeraha yanayomkabili tangu akiwa Kenya, ni kutokana na tabia yake ya upambanaji na njaa yake ya kutaka kucheza wakati wote ilihali bado hajakuwa fiti kwa asilimia 100, jambo linalomsababishia kujitonesha na kuandamwa na kadhia hiyo.

Takwimu zinaonyesha kuwa, katika mechi tano ilizocheza Simba msimu huu, mchezaji aliyeanza kikosi cha kwanza mara zote kati ya hao ni Mpanzu pekee huku akiwa na mchango wa mabao mawili, akifunga moja dhidi ya Gaborone United ugenini na asisti moja dhidi ya Fountain Gate.

Ahoua alianza mechi nne mfululizo za kwanza, kisha akawekwa benchi ya mwisho dhidi ya Namungo. Yeye ndiye amekuwa na mchango mkubwa wa mabao akifunga mabao mawili dhidi ya Gaborone (nyumbani) na Fountain Gate ambapo pia alitoa asisti.

Morice ni mchezaji wa tatu kuanza katika mechi nyingi kati ya tano, akifanya hivyo mara mbili, huku akihusika kwenye bao alilofunga Ahoua kwa penalti dhidi ya Gaborone, hiyo penalti alichezewa faulo yeye. Kibu naye ameanza mechi mbili, hajafunga wala kuasisti.

Maema na Mutale, wameanza katika mechi moja, huku wote wakiwa na asisti moja-moja vs Namungo.