Chalamila ahimiza Watanzania kuibeba ajenda nishati safi

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewataka Watanzania kuibeba ajenda ya nishati safi kama moja ya njia ya kuliponya Taifa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Chalamila ametoa kauli hiyo leo Oktoba 9, 2025 katika hafla ya uzinduzi wa programu ya Konekt pika kwa Umeme inayotekelezwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambayo pia inahusisha ukopeshaji wa majiko ya umeme kwa wananchi.

Majiko hayo wanayokopeshwa, yatakuwa yakilipiwa kidogokidogo kupitia umeme wanaonunua hadi deni linapokwisha.

Akizungumza katika hafla hiyo, Chalamila amesema mabadiliko tabianchi yanaweza kudhoofisha rasilimali watu na kuifanya Tanzania kuwa Taifa lenye mali lakini halina rasilimali watu.

“Ni vyema tuwe na mali na rasilimali watu wanaoweza kuwa na mchango wa kubadili maisha ya Watanzania,” amesema Chalamila.

Ili kufanikisha hilo aliwataka Watanzania kutumia nishati safi ikiwemo ya umeme huku akuwahakikishia kuwa si gharama kama ambavyo watu wanadhani.

“Wapo wanaosema umeme ni gharama nikuhakikishie kuwa kama chakula kinaweza kuiva kwa uniti moja ukaona gharama kesho ukiambiwa mapafu yameharibika na hatuna uwezo wa kubadili, ukawa unachungulia mlango wa kaburi utajua umuhimu wa bei ya afya na bei ya umeme,” amesema.

Amewataka kwenda hospitali kuangalia namna watu wanavyopata tabu ya kujitibia magonjwa ikiwa hatua za awali zingeweza kutumika.

Amesema kulambana na mabadiliko ya tabia nchi ni moja ya njia ya kulinda amani ya nchi ambayo haihitaji bunduki bali kwa elimu ya kujitambua na kuhama katika matumizi ya nishati chafu kwenda safi.

“Wazo hili litaponya mazingira ya Tanzania na Afrika kwa ujumla kwani ni lazima watu waanze kutumia nishati safi hasa Dar es Salaam inayosimama kama soko kubwa la mkaa unaozalishwa nchi,” amesema.

Amesema ikiwa wakazi wa Dar es Salaam wataamua kutotumia mkaa soko lake litakuwa dogo jambo litakalofanya watu wapunguze ukataji miti maeneo mbalimbali nchini.

“Nishati safi inalinda ndoa, matumizi ya nishati yanafanya sura iwe chafu, kuna wanawake ukiwaangalia ni wazuri wa sura lakini nishati chafu inawaharibu, hakuna namna matumizi ya nishati chafu yakazalisha sura nzuri,” amesema.

Akizungumzia mpango wa ulipiaji majiko kidogokidogo kupitia ununuzi wa umeme amesema njia hiyo hutumika duniani kote nabhata nchi Ulaya haitumii fedha taslimu.

“Katika hili, Tanesco na Wizara ya Nishati wameonyesha ubunifu, sekta nyingine ziige mipango kama hii inayookoa maisha ya watanzania tuunge mkono mpango huo wa Konekti umeme pika kwa umeme,” amesema Chalamila.

Alitumia nafasi hiyo kuwatoa hofu Watanzania juu ya matumizi ya umeme katika kupikia huku akisema kabla ya majiko hayo kuuzwa yamefanyiwa uchunguzi wa kutosha na wataalamu.

Mkurugenzi wa Tanesco, Lazaro Twange amesema mpango huo unazinduliwa ili kuunga mkono ajenda ya serikali ya nishati safi ya kupikia inayolenga kuhakikisha asilimia 80 ya watanzania inahamia kwenye nishati safi wakati wao wakilenga kuhakikisha umeme unatumika kikamlifu

Amesema majiko yote wanayotoa yanaweza kupika chakuka chini ya uniti moja.

“Wakati tunakua umeme ulikuwa ni anasa lakini sasa ni huduma na vifaa vya umeme vinatumia umeme kidogo. Katika safari hii tunao wenzetu wa mexi ambao wametoa zaidi ya Sh2.5 bilioni ili kusambaza majiko kwa watumishi wote wa Tanesco kwa mkopo na sasa programu hiyo inakwenda kwa wananchi hasa wanaounganishiwa umeme.

“Ukiunganishiwa umeme unaweza jiko na ukawa unalipia kadri anavyonunua umeme. Tanzania imekuwa ya kwanza kuwa na huduma hii wenzetu watafuata ili kuhakikisha kuwa majiko haya yanatumika katika kupika,” amesema.

Akizungumzia wiki ya huduma kwa wateja iliyoadhimishwa kwa siku mbili katika viwanja hivyo amesema inalenga kupokea maoni ya wateja wao kujua nini wanataka nini ili waweze kupatiwa huduma nzuri.

Ndani ya siku mbili wateja 350 wamehudumiwa na ili kuhakikisha jambo hili haliishi hapa tumeamua kuwa na kamati maalumu inayoshughulikia mteja,” amesema.

Amesema kwa Tanesco mteja ni zaidi ya neno lenyewe na ndiyo maana wanatamani kusikia wateja wanahudumiwaje jambo ambalo limeenda sambamba maboresho ya kitengo cha huduma za wateja ikiwemo mitandao ya kijamii, makundi ya whatsapp.

Pia wamesogeza huduma kwa wateja ili kuhakikisha taarifa zinafika kwa wateje bila kuchelewa.

“Kwenye maeneo ambayo magari hayafiki tumenunua bajaji na pikipiki ili kuhakikisha wito wa wateja unafikiwa bila sababu,” amesema Twange.

Mwakilishi wa Ubalozi wa Uingereza, Charles Barnabas amesema kwa sasa wanafanya kazi na Tanesco kuwasaidia wateja wao kutumia umeme katika kupika.

Kwa kuanzia walitoa mikopo kwa wafanyakazi wa Tanesco Agosti 14, mwaka huu na sasa programu hiyo inazinduliwa kwa wateja wao.

“Hili ni jambo la kwanza kufanywa katika Ukanda wa Jangwa la Sahara na hakuna nchi yoyote iliyofanya afua hii. Sisi kama ubalozi wa Uingereza tutaendelea kuwasaidia ili wapate hela nyingine kwani tunatambua ukosefu wa fedha kama moja ya changamoto inayowakabili,” amesema.