Chaumma yaahidi barabara ya njia nane Kibaha – Chalinze

Pwani. Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ameahidi kukamilisha ujenzi wa njia nane Barabara ya Morogoro kuanzia Kibaha hadi Chalinze kama mkakati wa kuifungua Dar es Salaam na Pwani kiuchumi, endapo atachaguliwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Kwa sasa kipande cha barabara ya njia nane kimeanzia Ubungo jijini Dar es Salaam hadi Kibaha mkoani Pwani.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo Oktoba 9, 2025 eneo la Picha ya Ndege, Kibaha mkoani Pwani, Mwalimu amesema foleni za mara kwa mara katika barabara hiyo ni changamoto kwa wananchi na uchumi wa Taifa.

Amesema foleni hupunguza tija na kuongeza gharama kwa watu wanaotafuta kujikwamua kiuchumi.

“Ajali haziishi kila siku. Barabara hii ndiyo tegemeo la Taifa, lakini inakwamisha uchumi. Tunaenda kumalizia kuijenga kwa njia nane kuanzia Kibaha hadi Chalinze ili kuifungua Dar es Salaam na Pwani kwenye fursa za kiuchumi,” amesema Mwalimu.

Ameeleza kuwa, Serikali ya Chaumma haitafanya mzaha na miundombinu ya msingi kama barabara hiyo, akisisitiza kuwa, uzembe uliopo sasa unalazimisha watu kutumia muda wa wiki nzima kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi Zambia, hali ambayo chama chake kitaikomesha.

“Chaumma tukiingia madarakani, tabia ya kutumia wiki nzima hadi Zambia itaisha. Tutaijenga barabara hii kwa njia nane hadi Chalinze,” ameahidi huku akisisitiza kuwa Taifa linahitaji viongozi wenye fikra mpya na maono, si umri au historia pekee.

Amesema barabara hiyo ni kiungo muhimu kwa uchumi wa nchi, lakini kwa sasa inakabiliwa na msongamano mkubwa wa magari unaokwamisha juhudi za wananchi kujikwamua kiuchumi.

“Foleni ya kila siku katika barabara hii ni kikwazo kikubwa kwa wananchi na uchumi kwa jumla. Tunaenda kujenga wananchi msiwe na wasiwasi nichagueni Mwalimu, tuone kama kutakuwa na foleni,” amesema.

Mwalimu ameongeza kuwa, Serikali ya Chaumma itakuwa ya vijana, yenye maono na mikakati ya kweli ya maendeleo, tofauti na Serikali zilizopita ambazo, amedai zimekosa ubunifu na dira thabiti.

“Tabia ya kutumia wiki nzima kufika Zambia kupitia barabara hii itaisha mara moja Chaumma kitakapoingia madarakani. Ikulu kunahitaji ubongo safi na Dodoma kunahitaji akili mpya, siyo umri tena,” amesema.

Khadija Rungwe, mgombea ubunge Kibaha Mjini kupitia Chaumma, amesema licha ya jimbo hilo kuwa na mazingira mazuri na watu wengi, bado linakabiliwa na changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara, jambo linaloathiri usafirishaji wa bidhaa na huduma muhimu kwa wananchi.

 “Kibaha ina wakazi wengi lakini hatuna vituo vya kutosha vya afya. Mkinichagua nitakuwa sauti yenu, nitapigania mageuzi yatakayoleta huduma bora kwa wote,”amesema Khadija.  

Ameahidi kuwa, kipaumbele chake ni elimu, kwa kusimamia ujenzi wa shule bora zenye vifaa vya kisasa vitakavyowasaidia wanafunzi kupata maarifa na kujitegemea.

Aidha, ameweka mkazo kwenye uwezeshaji wa makundi maalumu hasa wanawake na vijana.

“Kinamama nitawasaidia kupata mikopo ili waendelee na shughuli zao, pia vijana hasa waendesha bodaboda, nitahakikisha mnapata mikopo yenye masharti nafuu ili mjikwamue kiuchumi,” amesema Khadija.

Mwenyekiti wa chama hicho, Hashim Rungwe amesema chama hicho kimejipanga kuboresha huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na kugawa chakula cha ubwabwa bure kwa wanafunzi kuanzia Chekechea hadi kidato cha sita; na hata kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini.

“Hatutaki mtu alazwe bila kula. Serikali inapaswa kutumia fedha zake kuimarisha maisha ya watu, na sisi Chaumma tunathamini nguvu kazi ya wananchi,” amesema Rungwe.

Rungwe amewataka wananchi wa Kibaha kutumia uchaguzi mkuu kama fursa ya ukombozi na mabadiliko ya kweli, akisema chama tawala (CCM) kimetawala kwa muda mrefu bila kuleta mabadiliko makubwa.

“Wananchi tumechoka na ahadi zisizotekelezwa. Ni wakati wa kuwapigia kura wawakilishi wa kweli, waliokuja kwa nia ya kuwakomboa wananchi wa Kibaha,” amesema.