Mbulu. Benki ya CRDB kupitia CRDB Foundation, kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya Sh66 milioni kwa vikundi 20 vya wanawake, vijana na wenye ulemavu vilivyoko katika Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara.
Mikopo hiyo ya asilimia 10 isiyo na riba imetolewa chini ya mpango wa Imbeju kwa lengo la kuwasaidia wanavikundi hao kuinuka kiuchumi kupitia biashara zao na shughuli nyinginezo za kiuchumi wanazoziendesha.
Akizungumza katika ghafla ya kukabidhi hundi hiyo, leo Oktoba 9, 2025 wilayani Mbulu, Meneja wa CRDB Kanda ya Kaskazini, Cosmas Sadat amesema benki hiyo ilipokea jumla ya maombi 66 ya vikundi yenye thamani ya Sh233 milioni.
Amesema baada ya mchakato wa uchambuzi na mafunzo ya elimu ya fedha, vikundi 20 vilikidhi vigezo na kupatiwa mikopo yenye jumla ya thamani ya Sh 66 milioni, sambamba na pikipiki kwa ajili ya shughuli za uzalishaji.
“Mikopo hii imelenga kuongeza mitaji na kukuza uzalishaji kwa walengwa ambao awali hawakuwa na uwezo wa kupata huduma za kifedha kwa urahisi.
“Tunataka kuona kundi hili la wanawake, vijana na watu wenye ulemavu likibadilisha maisha yao kupitia mtaji huu, na kuwa wazalishaji na walipa kodi na sio tegemezi tena,” amesema Sadat.
Amesema mpango wa Imbeju wa CRDB Foundation inalenga kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwawezesha wananchi kupitia mikopo nafuu na masharti rafiki, sambamba na kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi hasa katika maeneo ya vijijini.
“lengo ni kuhakikisha makundi yenye changamoto za upatikanaji wa huduma za kifedha yanapewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji, hivyo kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael Semindu, wakati akikabidhi hundi ya mfano na pikipiki kwa wanavikundi, amesema serikali itaendelea kusimamia kwa karibu urejeshaji wa mikopo hiyo ili iwe endelevu na iweze kuwanufaisha wananchi wengi zaidi katika siku zijazo.
“Tunatoa wito kwa wanufaika kutumia mikopo hii kwa malengo yaliyokusudiwa na kuepuka matumizi yasiyo na tija”;
“Serikali itakuwa bega kwa bega kuhakikisha kila senti inaleta matokeo chanya kwenu na baadae kwa wengine ili kuwa na taifa lenye watu wanaoweza kujitegemea kiuchumi,” amesema Semindu.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Bodaboda Mbulu, Ibrahimu Bajuta amesema mikopo hiyo itawawezesha vijana wengi kumiliki pikipiki binafsi badala ya kutegemea pikipiki za mikataba au ya kukodi kama ilivyo sasa.
“Hii itatusaidia sana kujipa jukumu la kurejesha haraka ili umiliki pikipiki yako tofauti na sasa tunakodisha za wenzetu au kuchukua za mikataba zenye kuhitaji fedha zaidi ya mara mbili au tatu ya manunuzi ya pikipiki yako mwenyewe,” amesema.
Amesema pikipiki hizo itaongeza kipato chao na kuimarisha maisha yao kama madereva bodaboda lakini pia kwa taifa kwa ujumla.
Naye wanachama wa kikundi cha wanawake ‘Vedi’, Marry Joseph amesema fursa hiyo imekuja wakati muafaka ambao wanawake wanajitafuta kusimama katika uchumi wao kwa manufaa ya familia zao na jamii kwa ujumla.