Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Macho leo, Oktoba 9, 2025 matumizi ya vifaa vya kielektroniki ikiwemo simu yametajwa kutishia usalama wa macho, huku wataalamu wa afya wakipaza sauti wakitaka Serikali ichukue hatua za haraka ili kunusuru hali mbaya inayoweza kujitokeza katika miaka michache ijayo na kulinda afya ya macho.
Matumizi hayo ya kasi yameibua tatizo la uchovu wa macho wa kidijitali (Digital eye strain), hali inayosababisha kuona ukungu, maumivu ya kichwa, macho kukauka au kuwasha.
“Wizara ya Afya bado haijayapa macho kipaumbele, na sababu kubwa tunaambiwa jicho haliui ikilinganishwa na magonjwa mengine, lakini tunasahau kwamba jicho linaleta utegemezi,” anasema Rais wa Chama cha Madaktari wa Macho Tanzania, Dk Asha Mweke, na kuongeza:
“Sasa magonjwa yanayosababishwa na mtindo wa maisha, huzalisha presha ya macho ambayo pia haifahamiki na wananchi wengi. Ile inaleta ulemavu wa macho usiotibika. Nadhani umefika wakati Serikali ione haja ya kuwawezesha wataalamu ili kuifikia jamii.”
Anasema wengi hawatambui kuwa uchovu wa macho, maumivu ya shingo, usingizi hafifu na hata msongo wa mawazo, vinasababishwa na matumizi makubwa ya skrini.
“Mtu akiwa anatumia kifaa cha kieletroniki kama simu, kompyuta na televisheni kila baada ya dakika 20 anatakiwa kutazama kitu kilicho umbali wa futi 20 kwa sekunde 20,” anasema.
Pia anasema ikiwa mtu anaangalia vifaa hivyo kwa saa mbili, anatakiwa kujipa dakika mbili za kupumzisha macho na dakika mbili za kufanya mazoezi ya macho au afunge macho kwa dakika mbili.

Anasema matumizi ya muda mrefu kwenye vifaa hivyo huharibu macula ya jicho na husababisha uwezo wa mgonjwa kuona karibu unapotea, sababu mionzi hupita moja kwa moja. (Macula ni sehemu ndogo, yenye umbo la duara, iliyopo katikati ya retina, utando wa ndani wa jicho unaopokea mwanga. Macula ina jukumu kubwa katika kuona kwa uwazi).
Anaonya wale wanaotumia simu wakiwa kwenye chumba chenye giza kuwa ni kosa, kwani matumizi ya muda mrefu hufanya mionzi hiyo kutoboa macula. Wenye umri mkubwa hupata changamoto hiyo.
“Tunashauri matumizi mazuri ya simu. Mwanga ni tatizo, vaa miwani inayosaidia kupunguza mionzi. Kama unatumia sana kompyuta, ziwe na screen filter. Nenda kwa daktari wa macho upate vipimo sahihi, uvae miwani kusaidia kupunguza mwanga au mionzi,” anashauri.
Mtaalamu wa macho Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songwe, Dk Otilia Ngui, anasema wengi wana tabia wanapokuwa wamepumzika wanazima taa na kubaki na mwanga wa simu peke yake, hali iliyotajwa kutotakiwa kwa afya ya macho.
Anasema ni muhimu mwanga wa simu udhibitiwe na mwanga wa taa kabla ya kulifikia jicho. “Unapobaki na mwanga wa simu pekee, jitahidi uwe mdogo sana. Vifaa vya kielektroniki hutoa mwanga mkali, na macho nayo yanahitaji mwanga kwa kiwango fulani. Jicho halitakiwi kupokea mwanga mkubwa sana au mdogo sana,” anasema.
Dk Ngui anasema bila kuzingatia hayo, mhusika hupata changamoto ikiwemo dalili za ukavu wa macho, maumivu ya kichwa pembeni au hisia za kama macho yana mchanga.
Dk Ngui anasema kwa wale ambao kazi yao inahusisha vifaa vya kielektroniki, wanaweza kujilinda kupitia lensi maalumu za kupokea, ambazo anashauri kuzitumia katika kompyuta au simu badala ya mwanga kumfikia moja kwa moja kwenye macho.
Aidha, Dk Mweke anasema wanachokishauri ni matumizi mazuri na sahihi ya simu kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya na waliotengeneza simu hizo.
“Kuwe na muda maalumu wa kutumia vifaa vya kielektroniki. Kama mtu anatumia kompyuta, asizidishe saa nane, kuna athari kwenye macho, shingo na mgongo,” anasema.
Zaidi ya uchovu wa macho, wataalamu wa afya ya akili wanatahadharisha kuwa matumizi ya kupindukia ya vifaa vya kielektroniki yanachangia ongezeko la unyogovu, upweke na kukosa umakini.
“Vijana wengi wanapoteza uwezo wa kuishi bila simu. Wanapata wasiwasi mkubwa pindi wanapokatika mawasiliano (kuishiwa bando au intaneti), hali ambayo ni dalili ya utegemezi wa kisaikolojia,” anasema Dk Alex Ndalu, mtaalamu wa saikolojia.
Mratibu wa huduma za macho, Benedicta Shila, anasema mapumziko ya sekunde 20 kila baada ya dakika 20 yanaweza kuokoa macho, hivyo ameishauri jamii kufuata miongozo na elimu wanayopewa, akisisitiza kuwa matumizi ya simu kwa kiasi kidogo ni salama, lakini ukizidisha si salama.
“Kila baada ya dakika 20, pumzika kutazama skrini kwa sekunde 20, angalia kitu kilicho umbali wa futi 20 kutoka ulipo,” anasema.
Katika tamko lake leo Alhamisi, Oktoba 9, 2025 katika maadhimisho ya Siku ya Machi Duniani, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe, anawahimiza wananchi kufanya uchunguzi wa macho angalau mara moja kwa mwaka na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya. Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Penda macho yako, simulizi yako ni mwanga kwa mwingine.”
Dk Magembe anasema hapa nchini inakadiriwa kuwa takriban watu milioni 12 wanahitaji huduma za afya ya macho.
Anayataja magonjwa yanayoongoza kuwa ni pamoja na mtoto wa jicho, upeo mdogo wa macho kuona mbali au karibu unaorekebishika kwa miwani, shinikizo la macho, madhara ya ugonjwa wa kisukari kwenye pazia la jicho, pamoja na mzio na maambukizi ya macho, akisema magonjwa haya yanarudisha nyuma maendeleo ya familia, jamii na Taifa kwa ujumla.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2024, jumla ya watu milioni 1.5 walihudumiwa kwenye kliniki za macho nchini, ambapo asilimia 42 walikuwa watoto chini ya miaka 15, kati yao asilimia 6.3 walifika wakiwa tayari na ulemavu wa kutokuona.
“Kwa mwaka 2025, jumla ya huduma mkoba 59 zimefanyika katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo wananchi 132,107 wamefikiwa na kupatiwa huduma katika maeneo wanayoishi.
“Aidha, katika kipindi cha miaka mitano, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeimarisha huduma za macho katika hospitali za kanda na Taifa. Mwaka 2024 pekee, zaidi ya watoto 1,000 walifanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho na kupatiwa miwani, sawa na asilimia 55.6 ya wahitaji waliolengwa,” anasema.
Miaka ya hivi karibuni imeshuhudia simu zikigeuka kuwa sehemu ya maisha, wengi wakiamka nazo, kula nazo, kulala nazo, bila kujali gharama zake kiafya, kisaikolojia na kijamii kwa matumizi yasiyo na mipaka.
Katika mikutano ya familia, kila mmoja anatazama simu yake. Kwenye mabasi, treni na migahawa, midomo imefungwa lakini vidole vinacheza. Teknolojia imetukutanisha, lakini pia imetutenganisha kwa namna isiyoonekana.
Tafiti mbalimbali zinaonesha kwa wastani mtu mzima hutumia zaidi ya saa nane kwa siku mbele ya skrini, huku vijana wakiwa na muda unaozidi saa 10. Kwa wengi, simu zao ndizo “rafiki wa karibu zaidi” zikibeba ratiba, mawasiliano, burudani na hata hisia.
Wazazi wengi wanajikuta wakishindwa kudhibiti watoto wao wanaokua katika ulimwengu wa TikTok na YouTube badala ya michezo ya nje au mazungumzo ya ana kwa ana.
Hali hiyo inaonekana pia katika maeneo yanayotolewa WiFi bure, kumekuwa na mrundikano wa watu wakiwa wameinamia simu zao.
“Shughuli zangu nazifanya pembeni mwa reli. Huwa nasogea hapa nikitaka kujibu meseji zilizoingia sababu kuna intaneti ya bure (WiFi). Tatizo, wakati mwingine huwa nashtuka nimetumia dakika 30 mpaka 40 nimeinamia simu,” anasema Juma Hamis, mjasiriamali wa Tabata Relini jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, wapo baadhi ya watu walioshuhudia kwamba wamekuwa wakipambana na changamoto za maumivu ya macho kutokana na hali hiyo.
Janeth Lyimo, mkazi wa Mbezi, anasema ana uraibu wa simu yake ya mkononi. “Nikitumia sana simu huwa napata maumivu ya macho, yanakuwa kama yana mchanga, na siku nisipotumia sana simu hiyo hali siisikii,” anasema.