Rufiji. Wakati mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi akiahidi miradi mbalimbali ya maendeleo Wilaya ya Rufiji na Kibiti Mkoa wa Pwani, wao wameomba wapatiwe mkoa mpya.
Wamesema wanatembea zaidi ya kilomita 200 kufika Kibaha yalipo makao makuu ya mkoa huo ambapo hulazimika kupita mikoa ya Dar es Salaam na au Morogoro.
Maombi hayo yametolewa leo Alhamisi, Oktoba 9, 2025 na mgombea ubunge wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa katika mkutano wa kampeni wa Dk Nchimbi uliofanyikia Uwanja wa Soko la TASAF, Nyamwage, Jimbo la Rufiji.
Dk Nchimbi ameanza mikutano Pwani akitokea Zanzibar alikofanya mikutano jana Jumatano mikoa miwili ya Kusini Unguja na Kaskazini Pemba. Mpaka sasa ameifikia mikoa 21.
Dk Nchimbi amewaahidi endapo chama hicho kitapata ridhaa wanakwenda kuimarisha Hospitali ya Wilaya:”Na CCM inataka ifanye huduma zote za kisasa ili ifanane na Waziri wetu wa Tamisemi anapotoka.”
Amesema wanakwenda kujenga Zahanati tano, vituo vya afya vipya vinne, kuongeza nyumba za watumishi saba wilayani Rufiji.
Eneo la elimu, shule mpya za msingi nne, madarasa mapya 214 katika shule za zamani. Madarasa mapya 160 kwa shule za msingi, mabweni mapya 30.
Dk Nchimbi ameahidi eneo la kilimo mbali ya kuongeza mbolea ya ruzuku lakini watajenga skimu za umwagiliaji na ujenzi wa soko la kisasa na stendi ya mabasi eneo la Ikwiriri.
Amesema stendi za bodaboda 30, stendi ndogo ya mabasi itajengwa Utete. Dk Nchimbi amesema soko na stendi za aina hizo zitajengwa Kibiti.
Ujenzi na uboresha wa barabara za Rufiji na Kibiti za ndani na zinazounganisha wilaya na wilaya ama mkoa zitajengwa kwa kiwango cha limi na changarawe.
Miongoni ni barabara za Mji wa Ikwiriri na Mji wa Kibiti. Barabara ya
Utete hadi Nyamwage kilomita 30 ya lami. Lakini, ujenzi wa madaraja mbalimbali Rufiji na Kibiti yote ni kurahisisha shughuli za usafiri.
Dk Nchimbi amesema ghala kubwa la kuhifadhi chakula litajengwa Kibiti, machinjio ya kisasa, minada ya kisasa iwe mizuri na kujenga majosho mapya.
Dk Nchimbi amempongeza Mchengerwa ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa kuwa msaidizi mzuri na makini wa Rais Samia.

Amesema ujenzi wa shule, madarasa, mabweni, vituo vya afya, zahanati maeneo mbalimbali, Waziri huyo amehusika.
“Mwaka 2015 nilipojaza fomu ya kuwania uspika, miongoni mwa timu yangu alikuwa Mohamed Mchengerwa, bahati yao jina halikurudi. Lakini alipokuwa Waziri wa Utumishi, alikuwa hakubali mtumishi aonewe, alikuwa mtu anasimamia hali za watumishi. Mimi nachukia uonezi, nikiona mtu anachukia uonezi basi anakuwa rafiki yangu,” amesema Dk Nchimbi.
‘Tunaomba Rufiji iwe mkoa’
Mgombea ubunge wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa amesema Rais Samia amegusa kila kijiji, kila kata, kila wilaya, kila mkoa kupeleka maendeleo.
“Kila Mtanzania anajua kazi kubwa iliyofanywa na kama kuna wasiwasi basi si Rufiji na sisi tulimaliza siasa mwaka 2015. Kazi kubwa imefanyika mwaka 2015 na 2020, wananchi walikuwa na hasira na walikuwa sahihi kwani maendeleo yalikuwa bado na sasa chama chetu kiko salama hapa Rufiji, tumeungana na kazi inaendelea,” amesema Mchengerwa.
Mgombea huyo amesema:”Wahenga walisema Kijiji cha Mwenge hakizimwi bali kinapotezwa, uongozi ni kijiti na hii inatukumbusha Rais Samia alipokabidbiwa kijiti na Hayati John Magufuli na yeye akaendeleza na kufanikisha ndoto za Mwalimu Nyerere za kuwa na umeme wa uhakika.”
Mjumbe huyo wa Halmashauri Kuu amesema Bwawa kubwa la Umeme lipo Rufiji na kikao cha kwanza kilifanyikia Nyamwage wakati huo vijini vitano tu vya Rufiji kati ya 38 vilikuwa na umeme na sasa vyote vina umeme.
Amesema wakati anaingia mwaka 2015, walikuwa na shule za msingi 19, lakini sasa zimejenga 64, wamejenga shule hata sehemu ambazo hazikutarajiwa. Kulikuwa na shule nne za sekondari, lakini sasa wamejenga shule 24 za sekondari.
Mchengerwa amesema zipo kata wanafunzi walisafiri kilomita 70 kufuata shule za sekondari, ilikuwa halali wananchi wanaichukia CCM kwa sababu ilikuwa haijawapelekea shule. Shule ya kidato cha tano na sita ilikuwa moja lakini tumejenga saba.
“Vituo vya afya vilikuwa vitatu, wilaya kubwa kuliko mkoa wa Kilimanjaro, lakini miaka mitano ya Rais Samia vituo tisa vimejengwa, tumepeleka vituo vya afya kule ambako walikuwa wanasafiri zaidi ya kilomita 100.
Kulikuwa hakuna barabara za lami, lakini miaka 2020 hadi 2025, kutoka barabara hata nusu kilomita na sasa zipo zaidi ya kilomita 20,” amesema.
Amesema kulikuwa na barabara ya Nyamwage- Utete, ambayo mbunge wa kwanza, Bibi Titi Mohamed alianza kuiomba ijengwe mwaka1964, haikujengwa, leo yeye ni mbunge wa tisa ndiyo utekelezaji umeanza chini ya Rais Samia.

Baada ya kueleza hayo, Mchengerwa akasema wana maombi wanayompa Dk Nchimbi ambaye baada ya uchaguzi atakuwa msaidizi namba moja wa Rais Samia ya kuwapungudhia adha wananchi kusafiri umbali mrefu kufika makao makuu ya mkoa.
Amesema amekwisha kutoa maelekezo kama Waziri wa Tamisemi kwa Makatibu Tawala wa Mikoa ya Pwani na Lindi ili kuangalia mchakato wa kugawa maeneo yao kwani kwa sasa wananchi wanasafiri zaidi ya kilomita 200 tena kupitia Dar es Salaam au Morogoro.
Mchengerwa amesema zikigawanywa kule upande wa Kibaha zibaki Halmashauri tano na huku Halmashauri tanona:”(Dk Nchimbi) tutakuletea haya maombi, utuhurumie wana Rufiji kwani wanasafiri umbali mrefu sana na Rais ardhie kwani wananchi wanahangaika ili wapate mkoa na uitwe Rufiji.”
Wanu alivyomwombea kura mama, mmewe
Kabla ya Mchengerwa kuzungumza, aliomba apewe fursa mke wake, Wanu Hafidh Ameir awasalimie, ‘shemeji na wifi zake’. Tukio liliibua shangwe na matarumbeta juu.
Wanu ambaye ni mtoto wa Rais Samia amesema:”Mimi nisiseme mengi, yale yote yaliyoelezwa na Rais Samia na Dk Nchimbi, naomba niongezee, twendeni tukamchague Rais Samia kwa kura nyingi.”
“Msije kufanya makosa, twendeni kumchagua Samia Suluhu Hassan, lakini twendeni tukamchague Mohamed Mchengerwa, mtu kazi, amefanya mengi,” amesema Wanu.
Huku akishangiliwa na yeye kuonesha uso wa tabasamu, Wanu ambaye pia ni Mgombea ubunge wa Makunduchi akasema:”Rufiji niliyokuwa nakuja mwaka 2010 si Rufiji ya sasa, Mohamed Mchengerwa amefanya mengi sana, tumpe mitano tena.”
Alichokisema Pareso
Kada wa CCM, Cecilia Pareso amesema, Rais Samia ni kielelezo cha wanawake mashujaa waliotangulia mbele za haki waliokuwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya nchi akiwemo Mohamed Bibi Titi.
Pareso aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalum kupitia Chadema amesema, Rais Samia amebeba matumaini ya Watanzania, amebeba mwenge wa matumaini na tujitokeze kwa wingi kumchagua.
“Kwa kura yako ya ndio Oktoba 29, Rais Samia na Dk Nchimbi, wanakwenda kutekeleza ilani yetu ya uchaguzi yenye kuzingatia kazi na utu,” amesema Pareso.
Mbunge huyo wa zamani amewaomba wananchi kuwa makini siku ya kupiga kura ili isiharibike kwa kuhakikisha wanaweka tiki kwenye kisanduku kilicho pembeni kwani tofauti na hapo kura inaweza kuharibika.