DK.SAMIA ATAJA MABILION YA FEDHA YALIVYOLETA MAENDELEO MWANZA

 Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Mwanza 

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imetoa Sh.trilioni 5.6 ambazo zimetumika katika Mkoa wa Mwanza kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Akizungumza katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Nyamagana Mjini Mwanza leo Oktoba 8,2025 Dk.Samia ameeleza mbali ya miradi ya maendeleo katika ujenzi wa miundombinu ya barabara,madaraja, nishati,afya,maji, elimu, na huduma za jamii pia Serikali imefanya maboresho katika hospitali za Mkoa huo.

“Serikali  katika mkoa huo imefanya maboresho katika hospitali mbili kubwa za rufaa ambazo ni Sekou Toure ambako kumejengwa jengo la ghorofa tano kwa ajili ya mama na mtoto kwa Sh.bilioni 10.1.Jengo hilo linauwezo kubeba vitanda 261 hivyo kuchangia kupunguza vifo vya kinamama na watoto kwa kiasi kikubwa.

Vilevile, amesema vimewekwa vifaa vya kisasa zikiwemo mashine za CT Scan, mashine ya Endoscope na mtambo wa uzalishaji hewa safi.

“Zamani tulikuwa tunasafirisha mitungi kusambaza katika hospitali, sasa hivi hospitali zetu za rufaa na mikoa zote zinazalisha oksijeni.Mgonjwa anayezidiwa pumzi hapati huduma ipo palepale kwani mashine za kisasa zinapatikana,” amesema.

Kwa upande wa Hospitali ya Bugando, amesema kuwa zaidi ya Sh.bilioni tisa zimepelekwa kuboresha huduma, vifaa tiba na ujenzi wa wodi ya wagonjwa mahututi (ICU)

Pia, amesema Serikali imejenga jengo la matibabu ya saratani ikiwemo kununua mashine za uchunguzi wa saratani za matiti ambapo kinamama wameanza kupata huduma za uchunguzi.

Ameeleza kwamba mashine za mionzi ya saratani zimenunuliwa Bugando hivyo wagonjwa wa saratani kutoka Kanda ya Ziwa haiwalazimu kwenda Ocean Road kupata matibabu.

Ameongeza uwezo wa hospitali kuhudumia wagonjwa umeongezeka kutoka 1,200 hadi 1,500.

“Tunataka huduma za kibingwa zote zipatikane hapa Mwanza tupunguze rufaa kwenda Dar es Salaam. Mkitupa ridhaa ya kuongoza nchi hii, kipekee katika kisiwa cha Ukerewe tutaboresha Hospitali ya Nansio kuweka majengo ya wagonjwa wa dharura.”

Ameongeza maboresho hayo yatahusisha ujenzi wa hospitali moja ya kibingwa wilayani humo.”Yale ya mgonjwa kazidiwa kivuko kimeondoka, atapata huduma zote Ukerewe.”

Kuhusu elimu amesema  kuwa mbali na ujenzi wa shule za msingi na sekondari, serikali imeendelea kutekeleza sera ya elimu bila ada.

“Serikali imejenga vyuo vitatu vya VETA Magu, Misungwi na Buchosa kuhakikisha kila wilaya inapata chuo cha kutoa mafunzo ya ufundi stadi kuwawezesha kumudu maisha yao.

Pia, amesema kwa upande wa elimu ya juu katika mkoa  huo wa Mwanza , Serikali imejengwa kampasi ya Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) katika Wilaya ya Ilemela.

Ameongeza kuwa kampasi ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) imejengwa wilayani Misungwi.”Tumeboresha chuo cha maendeleo ya michezo Malya kilichopo Kwimba kwani sekta ya michezo ni chanzo kuhimu cha ajira kwa vijana.

“Tumewekeza zaidi ya sh. bilioni 34 chup cha Malya ili tuzidi kukuza vipaji na kuandaa walimu wengi zaidi kufundisha michezo shuleni,” ameongeza Dk.Samia.

Kwa upande wa nishati ,Mgombea Urais Dk.Samia awamu ya kwanza Serikali ilitoa mitungi ya gesi kwa ruzuku kwa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Amesema mitungi hiyo ilitolewa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kama ukombozi kwa afya ya kinamama.”Katika maeneo ambayo bado mwitikio ni mdogo serikali itaendelea kutoa mitungi hiyo kwa njia ya ruzuku.”