Binadamu huota na hujibidisha kufanikisha ndoto. Anajitazama na kujenga matamanio ya jambo. Anatamani kuwa wa kada fulani inayomvutia kwenye maisha.
Msemo wa “mipango si matumizi” hauna tofauti kubwa na “jitihada hazishindi kudra.” Unaweza kupanga, lakini mipango yako isishabihiane na matumizi. Unajitahidi, lakini jitihada zako zisikutane na kudra ambazo Mungu amekupangia.
Hussein Juma Salum, mwanzoni mwa maisha yake, alitamani kuwa mwanasayansi. Kila alipolala na kuamka, alijiona akiwa mtu ndani ya jumuiya ya wanasayansi. Alisoma vizuri elimu ya msingi. Alipofika sekondari, alichagua mchepuo wa sayansi. Masomo ya sayansi huhitaji bidi, Hussein alijibidisha darasani na nje ya darasa.
Ajabu ya Hussein, alijiona mwanasayansi lakini kupitia matokeo ya mitihani na majaribio ya darasani, alionekana mwanasiasa ndani yake. Alikuwa akipata ufaulu mzuri kwenye masomo ya siasa na yenye kufanana na siasa, wakati upande wa sayansi, matokeo hayakuwa na nuru hata kidogo.
Hali iliendelea kipindi chote cha masomo ya sekondari. Hata alipohitimu kidato cha nne, matokeo yalipotoka, yalimthibitishia kwamba alichokuwa anaota na kukipigania hakikuwa sawa na hali halisi aliyokuwa anakutana nayo. Masomo ya sayansi yalimsaliti kabisa, lakini nuru ilionekana kwenye siasa kutokana na alama alizopata.
Tazama Mungu alivyo wa ajabu, anataka uwe mwanasiasa na hakwambii, ila utavutwa kwa namna usiyoitarajia. Ona Hussein, ile misonyo ya hasira za kutofaulu sayansi na kutopenda alivyofaulu siasa, leo anagundua kumbe kila kitu kilikuwa ni wito. Uchaguzi Mkuu 2025, Hussein ni mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Tanzania Labour Party (TLP).
Kwa Hussein, Uchaguzi Mkuu 2025 siyo mara yake ya kwanza kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar, kwani hata katika Uchaguzi Mkuu 2020, jina la Hussein lilikuwa moja ya majina kwenye karatasi ya kupigia kura, alipokuwa anapambana kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Uchaguzi Mkuu 2015, Hussein alikuwa mgombea mwenza wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akichangia tiketi na aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya TLP, Machmillan Elifatio Lyimo. Uchaguzi Mkuu 2000, Hussein aligombea ubunge Jimbo la Kikwajuni, Unguja, Zanzibar. Majaribio yote hayo ya kutafuta uongozi katika vyombo vya dola, Hussein alitumia tiketi ya TLP.
Hussein alikaribishwa kwa mara ya kwanza kwenye ulimwengu wenye mwanga wa jua Mei 27, 1966. Hospitali ya Mnazi Mmoja (MMH), ambayo zamani iliitwa VI Lenin, ndipo mapokezi ya Hussein duniani yalipofanyika.
Ni mtoto wa tatu kwa baba yake, Juma Salum Juma, wakati ni mtoto wa saba kwa mama yake, Zaina Hussein Msumari.
Mwaka 1973, Hussein alianza safari ya elimu alipoanza darasa la kwanza Shule ya Msingi Mkwakwani, Tanga. Hii ni kwa sababu wazazi wake walihamia Tanga kwa kipindi hicho. Hussein alimaliza darasa la saba mwaka 1979 katika shule hiyohiyo ya Mkwakwani.
Matokeo ya mitihani ya darasa la saba yalipotoka, Hussein hakuchaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari upande wa Tanzania Bara. Kwa vile Zanzibar wakati huo elimu ya msingi ilikuwa mpaka darasa la nane, wazazi wa Hussein walimpeleka kuendelea na darasa la nane Shule ya Msingi Hurumji, iliyopo Mji Mkongwe, Zanzibar. Hiyo ilikuwa mwaka 1980.
Hussein alifanya vizuri katika mitihani ya darasa la nane Zanzibar, akachaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari. Mwaka 1981, Hussein alianza kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Shangani, iliyokuwepo Mji Mkongwe, Zanzibar. Shule hiyo kwa sasa haipo baada ya Wizara ya Elimu Zanzibar kuibadilishia matumizi.
Mwaka 1982, Hussein aliendelea na kidato cha pili Shule ya Sekondari Forodhani, iliyopo Mji Mkongwe, Zanzibar. Akiwa Forodhani, Hussein alisoma kidato cha pili na tatu (mwaka 1982 na 1983). Halafu mwaka 1984, alijiunga na Shule ya Sekondari Haile Selassie, iliyopo Mji Mkongwe, Zanzibar, alikosoma na kuhitimu kidato cha nne.
Ufaulu wake katika mitihani ya kidato cha nne haukumwezesha kuchaguliwa kuendelea na masomo ya juu, hivyo alijiunga na mafunzo ya kijeshi, Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Zanzibar. Yalikuwa mafunzo ya mwaka mmoja. Baada ya hapo, kwa kuwa alama zake za kidato cha nne hazikuwa mbaya, Serikali ilimchukua na kumwajiri kama mwalimu asiye na mafunzo.
Septemba 1987 ndipo Hussein alianza rasmi fani ya ualimu. Alianza kufundisha Shule ya Msingi Tumekuja, iliyopo Mji Mkongwe. Mwaka 1990, alihamia Shule ya Msingi Forodhani, Mji Mkongwe. Forodhani alifundisha kwa miezi minne, akahamishiwa Shule ya Msingi Darajani, Mji Mkongwe. Alifundisha kwa miezi mitatu, akaacha kazi kwa hiari.
Sababu ya kuacha kazi, aliona alichokuwa anaingiza na kutumia vilikuwa sawa. Hakuwa na uwezo wa kujiwekea akiba. Ni kutokana na mazingira hayo, Hussein anasema aliamua kuachana na ualimu ili kuangazia fursa nyingine za kimaisha. Ni uamuzi huo ambao umemfikisha leo akiwa mwanasiasa, lakini pia mfanyabiashara.
Kipindi akiwa mwalimu, yupo mwanafunzi wake aliyemvutiwa na Hussein, akamwona anafaa kuwa mwanasiasa. Jina la mwanafunzi huyo ni Mohammed Abdullah. Baada ya Hussein kuacha kazi ya ualimu, sehemu kubwa ya maisha yake ilikuwa Tanga na Zanzibar.
Kipindi yupo Tanga, Hussein alikutana na Mohammed, ambaye alimshawishi kujiunga na United Democratic Party (UDP). Hiyo ilikuwa mwaka 1994. Alibaki mwanachama wa kawaida wa chama hicho. Mwaka 1998, Hussein alijiunga na TLP. Mwaka 1999, alichaguliwa kuwa Naibu Mweka Hazina wa TLP, Zanzibar.
Mwaka 2005, TLP ilifanya uchaguzi mkuu wa chama, Hussein alichaguliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar. Kuanzia hapo, kila uchaguzi aligombea na kutetea nafasi yake mpaka sasa ameendelea kushikilia kiti hicho.
Hussein anasema anataka urais wa Zanzibar kwa sababu kwanza ni haki yake ya kidemokrasia na anaona ni fursa aliyonayo kikatiba. Pili, anaeleza kwamba anaguswa na hali za maisha ya Wazanzibari kwa sababu ni duni, hivyo shabaha yake ni kubadili maisha ya ndugu zake wa Zanzibar.
Anakiri kwamba Zanzibar inapiga hatua kimaendeleo, lakini ukuaji wa uchumi hauna uwiano mzuri na maisha ya wananchi wa kawaida. Anataka awe Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ili awawezeshe wananchi kuwa na maisha bora.
Katika kujenga maisha bora ya wananchi, msingi wa kwanza Hussein anaotaka kuujenga kwa Wazanzibari ni kutoa elimu bora. Dunia inakimbia, kwa hiyo anataka Wazanzibari wawe na elimu ya kutosheleza kukabiliana na kasi ya dunia.
Anaweka kusudi la kujenga hamasa kwa wazazi ili wawe na msukumo wa kuwahimiza watoto wasome, maana elimu ndiyo inaweza kukomboa vizazi, kujenga kesho bora binafsi na Visiwa vya Zanzibar kwa jumla. Mkazo wake wa elimu, anasema, utakuwa kwenye masomo ya sayansi ili Zanzibar iendane na kasi ya kiteknolojia ulimwenguni.
Mapambano dhidi ya rushwa yatakuwa kipaumbele cha Hussein akiwa Rais wa Zanzibar. Anakiri kuwa vyombo vilivyopo vinatosha, lakini vinakosa usimamizi madhubuti. Anaahidi akiingia madarakani, atahakikisha anavisimamia vema vyombo na taasisi zilizopo zenye kukabiliana na rushwa ili kumshinda adui huyo.
Hussein anataka kujenga uchumi imara Zanzibar. Katika hilo, anasema kilimo kimesahaulika na kimerudi nyuma. “Hatuzungumzi kilimo kama zamani kuwa ni uti wa mgongo. Katika kujenga uchumi, nataka turudi nyuma na kutazama fursa zilizokuwepo na sasa zimeachwa, hasa zitokanazo na kilimo,” anasema Hussein.
Anasema sasa hivi Zanzibar watu hawalimi. Zamani Wazanzibari waliuza nazi Dar es Salaam, lakini kwa sasa wananunua nazi kutoka Mafia. Mabonde ambayo yanafaa kwa kilimo cha mpunga hayatumiki ipasavyo.
Anataka akiwa Rais, aitumie ardhi iliyopo kwa njia za kisasa kuhakikisha kilimo cha mpunga kinastawi Zanzibar na Wazanzibari wanapata mchele wa kutosha, hasa kwa kuzingatia kwamba hicho ndicho chakula kikuu Zanzibar.
“Kwa ardhi tuliyonayo, nitaigeuza Zanzibar kuwa uchumi mkubwa utokanao na kilimo. Muhimu, Wazanzibari wenzangu waniamini na wanichague niwe Rais wao,” anasema Hussein, ambaye mwaka 2014 alikuwa mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ukiondoa siasa, Hussein ni mfanyabiashara. Hivi sasa, shughuli yake kubwa ni kuchukua dagaa wa Zanzibar na kuwasafirisha kwenda nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Zambia. Hapo nyuma alishafanya biashara ya matunda kati ya Tanga, Zanzibar na Kilimanjaro. Alishawahi pia kujishughulisha na biashara ya kuku kati ya Tanga na Zanzibar.
Hussein ni mpiganaji. Baada ya kuacha ajira ya ualimu mwaka 1990, alikwenda Mahenge, Morogoro, alipofanya majaribio ya shughuli za uchimbaji na biashara ya madini ya ruby.
Hata hivyo, aliachana nayo alipoona ni ngumu kwake kufanikiwa. Ndipo alipoingia kwenye biashara ya matunda, baadaye kuku na sasa dagaa.
Amana Suleiman Mzee ndiye mke wa Hussein, na kwenye ndoa yao wamejaliwa watoto wawili, wote wa kike— Rukia na Zaina.
Wito wake kwa Wazanzibari ni kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kudumisha amani ya nchi. Anasema amani haichezewi, kwani ikivurugwa ni vigumu kuirudisha upya.
Ubunge: 2000 – Jimbo la Kikwajuni, Zanzibar