YANGA haitakuwa na beki wake wa kati, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ katika mechi tano zijazo za Ligi Kuu Bara, lakini hilo haliwaumizi sana vichwa benchi la ufundi.
Romain Folz, kocha anayetajwa kuwa kwenye mazungumzo ya kuondoka Yanga, amemkingia kifua beki wa kikosi hicho, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, akisema adhabu aliyopewa ni kubwa na imemshtua lakini kwa kuwa timu hiyo ina mastaa wengi watakaocheza badala yake, hivyo hakuna kitakachoharibika.
Bacca ambaye ameitumikia Yanga kwa misimu minne, hivi karibuni amekumbana na adhabu baada ya kufanya faulo iliyotafsiriwa ni kuhatarisha usalama wa mchezaji wa Mbeya City, Ibrahim Ame.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 41:21 ya Ligi Kuu, Bacca amefungiwa mechi tano (5) mfululizo, adhabu ambayo ni pigo kwa Yanga inayopambana kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Akizungumza na Mwanaspoti, Folz amesema, ni kweli Bacca amekosea, lakini adhabu aliyopatiwa ni kubwa, huku akisisitiza kwa kuwa ni uamuzi wa Shirikisho hawezi kuupinga.
Amesema, bado hilo sio tatizo kubwa sana kwa upande wa Yanga kwani ina kikosi kipana chenye wachezaji wengi katika kila eneo hilo, hivyo hakuna kitakachopungua.
“Kweli Bacca alifanya kosa lakini adhabu aliyopewa ni kubwa sana na imenishtua ingawa sitaki kuingilia uamuzi wa Shirikisho la Soka, kwani lazima tuheshimu sheria zilizowekwa.

“Lakini maisha lazima yaendelee, kwani tulishajiandaa kwenye changamoto kama hiyo wakati wa dirisha la usajili kwa kuchukua mabeki wa kati wengine endapo itatokea dharura kama hizi.
“Wakati huu tutakuwa na nafasi ya kutengeneza upya ukuta wa timu kwa kuwa kuna wachezaji wazuri kama Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Frank Assinki.”
Mpaka sasa Yanga imecheza mechi tano za mashindano, huku Bacca akianza mechi nne ambazo ni Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete.
Mechi ambazo Bacca atakosa ni za Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar, Tanzania Prisons, KMC, Namungo na Coastal Union, kunatoa nafasi kwa mabeki wengine wa kati ndani ya kikosi hicho kupata nafasi.
Assinki pekee ndiye beki wa kati wa Yanga ambaye hajacheza mechi yoyote msimu huu, huku Bakari Mwamnyeto na Dickson Job wakipata nafasi sambamba na Bacca. Wakati ambao Bacca hakuonekana uwanjani, Job na Mwamnyeto ndiyo waliocheza pamoja.