Je, kuna ubaya wowote kuchukua mkopo?

Katika soko la uchumi wa leo, kukopa kumekuwa jambo la kawaida kabisa. Watu binafsi, kampuni, na hata mataifa hukopa ili kuharakisha utekelezaji wa malengo yao.

Lakini kuna swali kuu la kujiuliza: Je, kukopa ni njia ya kujenga maisha bora ya baadaye, au ni mtego unaowazamisha wakopaji kwenye shimo la madeni lisilo na mwisho?

Kwa hakika, kukopa si jambo baya au jema bali inategemea umekopa kwa ajili ya kufanya jambo gani. Ukitumia mkopo kwa busara, inaweza kuwa daraja linalounganisha ndoto zako na uhalisia wa maisha.

Ndiyo maana mara nyingi kuchukua mkopo kwa kuzingatia kanuni za ukopaji bora, hudhihirisha matokeo mazuri.

Ipo mifano mingi, inayodhihirisha mikopo yenye tija, lakini kwa uchache kukopa kwa ajili ya kuanzisha au kukuza biashara, au kuwekeza katika elimu, au kupata mtaji wa uzalishaji, mara nyingi ni jambo muhimu na lenye faida.

Mfanyabiashara anayekopa ili kuongeza mtaji wa muda mfupi ana nafasi kubwa ya kuongeza faida kwa mahitaji yake binafsi, na mkulima anayekopa kununua vifaa vya kisasa vya umwagiliaji anaweza kuongeza uzalishaji wa mazao yake.

Katika hali kama hizi, mkopo ni jambo jema kwa sababu, unachochea ukuaji wa kipato na maendeleo ya kiuchumi.

Hata hivyo, hali inabadilika kabisa pale mikopo inapochukuliwa kwa madhumuni yasiyofaa.

Ukikopa pesa kwa ajili ya maisha ya starehe, kama vile kununua bidhaa za kifahari, kufanya sherehe za gharama kubwa, au kusafiri likizo zisizo za lazima, kuna uwezekano mkubwa wa kuingia katika matatizo ya kifedha.

Muda unaotumika kulipa deni hutumia kipato cha kila mwezi, huvuruga mipango ya baadaye, na hatimaye unaweza kusababisha kufilisika. Deni halibaki tena kama chombo cha maendeleo, bali linakuwa mtego unaodhoofisha uhuru wa kifedha.

Hii ndiyo sababu nidhamu ya kifedha na upangaji wa mapema ni muhimu kabla ya kuchukua mkopo. Kabla ya kukopa, jiulize maswali haya: Je, fedha hizi zitazalisha kipato? Je, nina mpango thabiti wa kuzirudisha? Je, masharti na riba ya mkopo yapo ndani ya uwezo wangu? Ukijibu “hapana” kwa swali lolote kati ya haya, basi huenda kukopa si uamuzi sahihi kwa wakati huo.

Hivyo, jamii ina wajibu wa kujenga utamaduni wa kukopa kwa uwajibikaji kwa kuhakikisha inafanya tafiti kabla ya kuchukua mkopo ili kufahamu taasisi zinazotoa mikopo kwa masharti nafuu na kwa urahisi zaidi, pamoja na kuwekeza katika elimu ya fedha.

Jamii inapaswa kufahamu kwamba mkopo si “pesa ya bure” bali ni fedha inayohitaji matumizi ya kimkakati yanayokusudia lengo maalumu ili kupata matokeo mazuri.
 
Ni muhimu kujua kuwa kukopa sio adui wa mafanikio yako bali kutojibidisha kupata elimu ya fedha ndiyo adui halisi. Ni Dhahiri kwamba mkopo ni chombo kinachoweza kukupeleka kwenye mafanikio ya kifedha au kukuingiza kwenye madeni zaidi.

Siri ya mafanikio ipo katika namna unavyoutumia. Kopa ukiwa na lengo, kuwa na mpango wa kurejesha fedha ulizokopa, na nidhamu ya kutumia mkopo huo kwa uzalishaji.

Kukopa ni kama mfano wa moto ambao unaweza kupikia chakula au kuchoma nyumba yako. Uamuzi uko mikononi mwako. Tumia mkopo kujenga maisha yako ya baadaye na si kuyaharibu.