JKT Queens imeifuata Simba Queens katika fainali ya Ngao ya Jamii baada ya kuitoa Yanga Princess kwa mikwaju ya penati 6-5 kufuatia sare ya bao 1-1.
Katika mechi ya nusu fainali iliyokuwa na ushindani wa aina yake iliyopigwa leo Oktoba 9, 2025 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar ikiwa ya pili baada ya ile ya awali, Simba Queens kuifumua Mashujaa Queens mabao 2-0, JKT Queens ilikuwa ya kwanza kufunga bao kupitia Winfirda Gerrald dakika ya 27.
Winfrida alifunga bao hilo kwa juhudi binafsi baada ya kuukokota mpira akitokea pembeni na kuingia ndani, akapiga shuti lililomshinda kipa wa Yanga, Zubeda Mgunda.

Dakika 44, Jeaninne Mukandayisenga akaisawazisha Yanga Princess baada ya timu hiyo kupata pigo la kona.
Kipindi cha kwanza kinatamatika timu zote zikienda mapumziko kwa sare ya bao 1-1, matokeo yaliyodumu dakika zote 90.
Hata hivyo, mambo hayakwenda sawa kwa Yanga baada ya beki wa kushoto, Wincate Kaari kupewa kadi ya njano ya pili na kulamba nyekundu iliyowafanya Wananchi kumaliza wakiwa pungufu.
Katika mikwaju ya penati, kila timu ilipiga saba ambapo JKT Queens ilikosa moja kupitia Winfrida Gerrald, huku Yanga Princess waliokosa ni Agnes Pallangyo na Chinemerem Angela.

Rasmi sasa fainali itawakutanisha timu Simba Queens dhidi ya JKT Queens kwenye Uwanja wa KMC Complex, Oktoba 12, 2025.
Timu hizo zinakwenda kukutana zikiwa na kumbukumbu ya mchezo wa fainali ya Ngao ya Jamii mwaka 2023 iliyomalizika kwa Simba Queens kushinda kwa penalti 6-5 baada ya dakika 90 matokeo kuwa sare ya bao 1-1.
JKT Queens na Simba Queens, ndiyo timu zilizofanikiwa kubeba taji la Ngao ya Jamii tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo. Simba Queens ilianza kubeba mwaka 2023, ikafuatia JKT Queens 2024.
Yanga Princess: Zubeda Mgunda, Igwe Uzoamaka, Lydia Akoth, Jeaninne Mukandayisenga, Aregash Kalsa, Wincate Kaari, Ester Akudo, Precious Christopher, Agness Pallangyo, Wema Maile na Ritticia Nabbosa.

JKT Queens: Naijath Abbas, Donisia Minja, Lidya Maximilian, Stumai Abdallah, Sarah Joel, Elizabeth Chenge, Ester Maseke, Jamila Rajabu, Winifrida Gerald, Janeth Christopher na Christer Bahera.