WATU wawili wanapeperusha vyema bendera ya Tanzania katika upande wa utawala wa soka hivi sasa ambao ni Wallace Karia na Injinia Hersi Said.
Alianza Karia ambaye ni Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuchaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Baadaye akateuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya uchumi na fedha ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na mwaka huu akachaguliwa kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya shirikisho hilo.
Halafu kuna Hersi. Huyu alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Klabu za Soka Afrika (ACA) na baadaye akateuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya mashindano ya CAF.
Sasa juzi wote wamelamba uteuzi katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) wakiingia katika kamati za shirikisho hilo baada ya baraka za baraza lake.
Karia ameteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya soka la ufukweni ya FIFA ambayo pia ameteuliwa kuwa Makamu wa Rais wake huku Hersi akiteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya mashindano ya soka ya wanaume.
Habari hizi zimepokewa vizuri sana hapa kijiweni kwa vile ni heshima kubwa kwa nchi yetu kuona tuna watu ambao wanatambulika utendaji kazi wao na mamlaka kubwa za soka.
Uteuzi huo hapana shaka umetokana na kazi nzuri ambazo wamezifanya katika nyadhifa zao walizoteuliwa awali na kuivutia FIFA iwaamini kuwa wanafaa katika kamati zake.
Jambo la muhimu kwao ni kuhakikisha wanatumia vyema fursa hizo kusaidia mpira wa Tanzania na sio kuangalia zaidi maslahi na sifa zao binafsi.