Karibuni Pantev na Roro, msituamini sana Wabongo

KUNA uwezekano wa zaidi ya asilimia mia moja kwamba mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara baina ya Yanga na Simba ukakutanisha makocha wawili wapya wa timu hizo ambao hawakuwapo zilipokutana katika mechi ya ufunguzi wa msimu ya Ngao ya Jamii.

Kwa Simba ni uhakika maana tayari Fadlu Davids aliyekuwa katika Ngao ya Jamii kwa sasa hayupo na nafasi yake imechukuliwa na Dimitar Pantev.

Yanga nayo inaonekana ni suala la muda tu kabla haijafanya uamuzi mwepesi wa kuachana na Romain Folz na kisha kumleta Kocha mpya ambaye anatajwa kuwa Romuald ‘Roro’ Rakotondrabe.

Kijiwe kinaamini kwamba kuachana na Folz ni uamuzi mwepesi kwa Yanga kwa vile mashabiki wengi wa timu hiyo hawamkubali pamoja na kwamba hajapoteza mchezo wowote hadi sasa.

Uzuri mashabiki wa hizo timu mbili wameona kazi iliyofanywa na Pantev na Rakotondrabe katika timu walizopita kabla ya kujiunga na miamba hiyo miwili ya soka hapa Tanzania.

Pantev aliiongoza Gaborone United kupiga soka safi dhidi ya Simba katika mechi mbili za raundi ya kwanza ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika japo ilitolewa.

Rakotondrabe aliifanya timu ya taifa ya Madagascar kuwa gumzo katika mashindano ya CHAN 2024 ambayo timu hiyo ilifika fainali na kupishana hasa na Morocco japo ilipoteza lakini pia hivi sasa ipo nafasi ya pili katika kundi lake la kuwania kufuzu Kombe la Dunia.

Jambo la muhimu ambalo kijiwe kinawasisitiza Roro na Pantev waliweke akilini ni kuwa makini na sisi watu wa mpira hapa bongo kuanzia wale wa ndani ya timu zao na hata wa nje ya timu zao.

Ushauri na ukosoaji ambao tutawapa wauchuje kwa uangalifu maana sio kila wakati unakuwa wa nia nzuri kwa makocha ila inawezekana ukawa wa kuwapigisha shoti.