Kibonde aahidi kununua bombardier 70, asisitiza amani

Tabora. Mgombea urais wa Chama cha Demokrasia Makini (Makini), Coaster Kibonde ameahidi kununua ndege 70 aina ya Bombadier ili kurahisisha usafirishaji wa abiria hapa nchini.

Vilevile, mgombea huyo amewahimiza wananchi kuwapuuza watu wote wanaohamasisha vurugu na vitendo vya kichochezi, kwani amani ya nchi ni muhimu zaidi ili kupata maendeleo.

Akinadi sera za chama hicho Oktoba 8, 2025, mgombea uraisi kupitia chama hicho, Coaster Kibonde amesema taifa lolote ni lazima liwe na amani kwanza ndipo maendeleo yafuate.

Amesisitiza kuwa endapo itafikia mahali ili mtu apate urais ni lazima watu wamwage damu, hayuko tayari na cheo hicho na hakitokuwa na maana kwake kwa sababu watu wana thamani zaidi kuliko huo uongozi.

“Amani ni mtaji namba moja, kwa hiyo Makini tukiingia tu madarakani, tunaendelea kwanza kudumisha amani huku utekelezaji wa mambo mengine ukiendelea,” amesema.

Amesema akichaguliwa atahakikisha anaimarisha usafiri wa anga kwa kununua ndege 70 aina ya Bombadier ili kurahisisha usafiri wa anga na kufanya biashara zifanyike kwa haraka, watalii wasichelewe kwa sababu za usafiri wa uhakika.

Wananchi wa Tabora wakisikiliza sera za mgombea wa uraisi chama cha Makini. Picha na Hawa Kimwaga

“Nitaleta ndege hapa za kutosha, lazima watu wapande ndege hapa saa 24 wakifanya shughuli zao na wakitalii huku pato likiendelea kuingia kwa maendeleo ya nchi,” amesema mgombea huyo.

Kuhusu afya, Kibonde amesema huduma za afya zitakua bure kwa wananchi kwani atajenga hospitali katika kila kata nchini, ataweka vifaa tiba vya kutosha na watoa huduma wabobevu ambao watakua wamesomeshwa bure na serikali kwa ajili ya kutoa huduma katika hospitali hizo.

Ameahidi ujenzi wa barabara zitakazounganisha mikoa na wilaya zote nchini kwa kiwango cha lami, atajenga reli ya kisasa (SGR) kutoka Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora hadi Mpanda mkoani Katavi ili kurahisisha sekta ya usafirishaji ardhini nchini.

Ameongeza kuwa endapo atachaguliwa atatoa ekari tano pamoja na hati zake kwa kila kijana nchini ili kuwakopesha fedha ambazo wataendesha kilimo na kujiingizia kipato cha kujikwamua wao na familia zao.

“Fedha zipo za kutosha na haya mambo yanawezekana, kwa hiyo nyie nipeni ridhaa niongoze taifa muone maisha yenu yanavyobadilika na mtaishi kwa raha sana kwani hakuna kikwazo chochote,” amesema.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Bara, Grace Ngonyani amesema chama chake hakiweki ahadi tu majukwaani bali kitakwenda kutekeleza yale yote aliyoahidi.

“Sisi hatupigi porojo hapa ni wazi kuwa huduma za afya ni bure kule kinamama watajifungua bure bila gharama yoyote”

Mgombea ubunge wa Tabora Mjini, Idd Mbarouk amewaomba wananchi wampe ridhaa ya kuongoza jimbo hilo ili alete maendeleo kwa kasi mkoani humo.

“Mimi ni mzaliwa wa Tabora na najua wana Tabora wanataka nini, nyinyi jukumu lenu ni kunichagua tu, maendeleo niachieni mimi”

Aisha Juma, mkazi wa Tabora, amesema sera ni nzuri lakini hizo ndege zitakazoletwa nchini basi nauli ziwe rafiki na watu wa hali ya chini waweze kupanda.

“Kweli ndege zinarahisisha usafiri mtu unafika haraka unapokwenda lakini sasa nauli zishuke basi wote tuweze kupanda”

Wananchi wa Tabora wakisiliza sera za mgombea wa uraisi Chama cha Makini. Picha na Hawa Kimwaga

Juma Maganga amesema barabara ni moja kati ya mahitaji ya wanaTabora maana ni wakulima na wanataka kusafirisha mazao, hivyo mgombea ahakikishe anazijenga kweli.

“Barabara alete kweli sisi tunahitaji kusafiri na kusafirisha mizigo yetu na hasa mazao unajua sasa hivi tumeamka sana kibiashara”amesema.