Kiongozi Mbio za Mwenge ahimiza nishati safi kutumika mashuleni

Mbeya. Kiongozi  wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail All Ussi ameagiza kuwepo mkakati wa kuhamasisha matumizi  ya nishati safi mashuleni  ili kutunza  mazingira  na kuunga mkono  agizo la Rais  Samia Suluhu Hassan.

Ussi amesema hayo leo Alhamisi  Oktoba 9, 2025 wakati akiweka jiwe la msingi kwenye bwalo la wanafunzi  wa Shule ya Sekondari Imezu Wilaya  ya Mbeya sambamba  na kugawa mitingi ya nishati  safi  bure kwa kaya maskini wakazi wa vijiji vya Inyala na Itewe.

Kiongozi  wa mbio za mwenge kitaifa mwaka 2025,Ismail Ussi(kuli )  akifunua kitambaa kuashiria  uzinduzi  wa bwalo la Shule ya Sekondari Imezu Wilaya ya Mbeya.Picha na Hawa Mathias

“Nendeni mkaunge mkono kampeni za Rais Samia Suluhu Hassan juu ya matumizi ya nishati safi ili kutunza mazingira haswa matumizi ya gesi ambayo ni salama kwa afya za watanzania,”amesema.

Amesema ni jukumu la kila mwananchi kugeukia  matumizi ya nishati safi ya gesi ili ifikapo  2030 tufikie asilimia  80 lakini tuna kila sababu  kuipongeza Serikali  ya Wilaya kuendelea  kusimamia wajibu  kwa kutoa mitungi ya gesi kwa wananchi kaya maskini, “amesema.

Ussi amesema  ufike wakati walimu mashuleni kubebe jukuhu  hilo kama ajenda ya kutoa  elimu kwa wanafunzi  ili kutimiza matakwa ya Serikali ili kutunza mazingira.

Katika hatua nyinyine, amewataka wananchi hususani wanafunzi kuhamasisha wazazi kushiriki  kikamilifu katika  uchaguzi mkuu Oktoba 29,2025  kupiga za mgombea urais Samia Suluhu Hassan.

Muonekano wa bwalo la wanafunzi wa Shule ya Sekondari Imezu Wilaya ya Mbeya lililowekwa jiwe la msingi  na mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2025.Picha na Hawa Mathias

“Lakini pia nimeona Serikali  ya  Mkoa  wa Mbeya imesimamia vyema utekelezaji  wa miradi ya maendeleo  sambamba  na uwezeshaji makundi ya wanawake, vijana na walemavu  na ndio lengo la Serikali  ya awamu ya sita,”amesema.

Ussi  pia  amepongeza  uongozi  wa halmashauri  ya Wilaya ya Mbeya  kwa usimamizi  mzuri wa  utekelezaji  wa miradi  ya maendeleo  yenye  thamani  ya  zaidi ya Sh1.3 bilioni ambayo imekaguliwa na  mbio  za mwenge  wa Uhuru kitaifa  2025.

“Niwasihi endeleeni kusimamia  vyema utekelezaji  wa miradi  ya maendeleo  ambayo Serikali ya awamu ya sita  imetoa fedha  kwa maslai ya Watanzania  na Taifa kwa ujumla,”amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya  Solomon  Itunda, akitoa taarifa ya mradi wa  ujenzi wa bwalo la Shule ya Sekondari Imezu Wilaya ya Mbeya kwa kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ussi. Picha na  Hawa Mathias

Wakati huo huo ameonyesha  kuridhishwa  na utekelezaji  wa mradi wa kuzalisha  hewa tiba (Oxygen Plant), wenye thamani ya Sh298 milioni ambao utaleta tija katika hospitali  vituo vya afya na zahanati.

Mradi huo una uwezo  wa kuzalisha  mitingi hewa tiba  90  yenye ujazo wa lita kwa masaa 24 na kutoshereza mahitaji ya hosptali kwa mahitaji ya  mitungu 10 hadi 15  kwa siku jambo ambalo litaboresha utoaji  wa huduma za afya.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi    wa miradi mingi ya maendeleo.

“Tunaishukuru sana Serikali ya awamu ya sita   chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, lakini tutahakikisha anapata kura za kishindo   katika uchaguzi mkuu Oktoba29,2025, “amesema.

Mjasiriamali wa kuchoma nyama katika kituo cha mabasi Tarafani, Sambe Joel amesema wameweza kufanikiwa kiuchumi kufuatia mikopo asilimia 10 iliyotolewa na Serikali.

“Tuko bega kwa bega na Mama Samia tumeona alivyoweza kupunguza uharifu  nitaani kwa kutoa mikopo,lakini tunaomba aelekeze halmashauri  kuondoa ukiritimba  wa utoaji  wa mikopo jambo ambalo linawakatisha tamaa na kuitwisha mzigo  Serikali, “amesema.