Musoma. Ni simulizi inayosikitisha lakini ndio ukweli ulivyokuwa, kwamba baada ya mume kupiga mshindo wa kwanza na kuvaa kondomu ili kupiga mshindo wa pili, mke alikataa na hapo ndipo balaa lilipozuka hadi mume kumuua mkewe.
Tafrani hiyo iliyotokea Novemba 1, 2020 katika kijiji cha Machimeru katika Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara haikumwacha salama mume aliyekuwa akifanya mapenzi na mkewe shambani, kwani naye alikatwa uume na korodani zikabaki zikining’inia.
Hivi sasa mume, Masunga Ndilanha maarufu kwa jina la Kitambala anasubiri kunyongwa hadi kufa kwa kumuua mkewe, Shida Maduhu baada ya jopo la majaji watatu kubariki adhabu hiyo katika hukumu yao waliyoitoa Oktoba 6,2025.
Katika hukumu yao hiyo iliyowekwa katika mtandao wa mahakama Oktoba 9,2025, Majaji hao, Rehema Kerefu, Abraham Mwampashi na Ubena Agatho, wamesema upande wa Jamhuri ulithibitisha shitaka dhidi ya Ndilanha pasipo kuacha mashaka.
“Tumezingatia kwa makini ushahidi wote na mazingira ya rufaa tunashindwa kugundua kuwa kuna maneno yaliyotamkwa au matendo yaliyoonyeshwa na marehemu yalikuwa ya uchochezi kwa mrufani hadi kuuawa,”wameeleza.
“Mazingira hayo ni kama vile matukio yaliyotokea kabla ya tukio la mauaji, na hasa, jinsi mume na mkewe walivyoenda shambani pamoja, kulima na kufurahia onyesho la raundi ya kwanza (mshindo wa kwanza) hadi mwisho,” wamesisitiza.
Nini kilitokea hadi mauaji?
Awali ilidaiwa na upande wa Jamhuri kuwa Novemba 1,2022 katika kijiji hicho cha Machimeru Wilaya ya Bunda, mshtakiwa alimuua mkewe Shida Maduhu.
Aliposomewa shitaka na kuulizwa kama ni kweli ama la, mshtakiwa alijibu kuwa hakudhamiria wakati anamuua mkewe kwa vile wakati huo alikuwa anadai haki yake ya tendo la ndoa, lakini mwisho wa siku alihukumiwa kunyongwa.
Ushahidi unaonyesha mrufani na mkewe walifunga ndoa ya kimila mwaka 2014 huko Simiyu na baada ya kuoana, walikwenda kuishi Mpanda huko Katavi na katika maisha yao ya ndoa, walibahatika kupata watoto watatu na mali mbalimbali.
Shahidi wa kwanza wa Jamhuri, Suzana Sopi ambaye ni dada wa marehemu, alieleza kuwa maisha ya ndoa ya wawili hao yalitawaliwa na migogoro na kutoelewana na ambayo haikuweza kupata suluhisho la kudumu.
Katika kuishi huko na kutafuta maisha bora, mume aliamua kuhamia Zanzibar kutafuta fursa za kiuchumi huku akimwacha mkewe huko Mpanda mkoani Katavi, akiendelea kuendesha biashara ndogo ya rejareja.
Hata hivyo, mkewe aliamua kuuza kila kitu walichonacho ikiwamo bidhaa za dukani na kurudi nyumbani kwa wazazi wake kijiji cha Manchimeru wlayani Bunda, bila kumjulisha mumewe ambaye alikuwa bado yupo Zanzibar.
Mume alivyorejea kutoka Zanzibar
Baada ya kupokea taarifa za mkewe kuhama Mpanda, Oktoba 28,2020 mume akaamua kusafiri hadi Bunda kukutana na mkewe ili kumaliza tofauti zao.
Hata hivyo, usuluhishi haukwenda vizuri kwani mume alitenganishwa kulala na mkewe, kitendo ambacho hakikumfurahisha kwa vile amekuwa mbali naye kwa muda mrefu, hivyo akaendelea kudai kupewa haki yake ya tendo la ndoa.
Bahati nzuri, Oktoba 31,2020 ikiwa ni siku moja kabla ya tukio la mauaji, inadaiwa mke aliridhia kufanya mapenzi na mumewe lakini kwa sharti kwamba ni lazima akatafute mpira wa kiume (kondomu) kwa kuwa alikuwa hamwamini tena.
Hii ni kwa sababu alihisi hakuwa salama katika magonjwa ya zinaa, hivyo mume akaridhia sharti hilo akaenda kununua kondomu tatu tayari kwa ‘shoo’, lakini hata hivyo baadaye mke alibadili mawazo na hakumpa tendo la ndoa siku hiyo.
Siku iliyofuta kwa mujibu wa shahidi huyo wa kwanza, marehemu aliwaambia kwamba anakwenda shambani ambapo mume naye alimfuata.
Baadaye kidogo, Dawe Maduhu ambaye ni mama wa marehemu naye aliwafuata lakini ghafla shahidi huyo (Suzana Sopi) akamsikia mama yake akilia, aliamua kukimbilia shambani ndipo alimkuta mdogo wake amelala chini shingo ikiwa imekatwa.
Wakati huo bado alikuwa hai, hivyo alimuuliza nini kimetokea ambapo ndugu yake alimwambia alikatwa na mshtakiwa ambaye naye wakati huo alikuwa utupu na uume wake ukiwa umekatwa na korodani zake mbili zikiwa zinaning’inia.
Alimuona shahidi wa pili, Josiah Maduhu ambaye ni mjomba wake na watu wengine wakifika eneo la tukio kutoa msaada ambapo walimchukua dada yake na kumpeleka hospitali, lakini siku hiyohiyo alirudishwa akiwa maiti.
Shahidi wa Pili naye aliunga mkono simulizi hiyo, huku shahidi wa tatu ambaye ni Polisi aliyepeleleza shauri hilo akielezea namna yeye na maofisa wenzake walivyofika eneo la tukio, na kumkamata mshtakiwa na kumpeleka hospitali.
Mpelelezi huyo, Sajenti Chrisant mwenye namba E.9222 alieleza namna alivyoandika maelezo ya onyo ya mshtakiwa na baadaye kumpeleka kwa mlinzi wa amani, ambako kote huko aliandika maelezo na kukiri kutenda kosa hilo.
Katika utetezi wake, mshtakiwa ambaye ni mrufani katika rufaa hiyo, alibadili hadithi ya tukio hilo na kueleza kuwa alimuua mkewe katika harakati za kujitetea kujilinda, baada ya kumkata korodani wakifanya mapenzi.
Alieleza kuwa wakati wakifanya mapenzi shambani na wakati mkewe anavua nguo, kuna kisu kilidondoka kutoka kwenye nguo za mkewe na alipomuuliza ni cha nini, akasema kilikuwa ni kwa ajili ya kumenyea maembe wakiwa shambani.
Muda mfupi tu baadaye walianza kufanya tendo la ndoa na baada ya kumaliza mzunguko wa kwanza (bao la kwanza), mkewe alimtaka alale pembeni ili asafishe sehemu zake za siri kwa ajili ya kuingia mzunguko wa pili.
Aliridhia lakini ghafla alishangaa kuona korodani zake zimekatwa kwa kisu na katika jitihada za kujiokoa, kisu hicho kwa bahati mbaya na katika ile hali ya kuchanganyikiwa, kilimkata mkewe shingoni na yeye kupoteza fahamu.
Alikuja kuzinduka akiwa hospitali na alibaki na uume ambao unafanya kazi tu kama bomba la kukojolea na sio tena kwa ajili ya kufanya tendo la ndoa, na akakanusha kabisa tuhuma za mauaji ya kukusudia ya mkewe aliyoshtakiwa nayo.
Mwisho wa usikilizwaji wa kesi hiyo, Jaji Frank Mahimbali wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma alimtia hatiani na kumuhukumu adhabu ya kifo, hukumu ambayo imepata baraka za Mahakama ya Rufani Tanzania iliyoketi Musoma.
Alivyokata rufaa na kutupwa
Licha ya kukata rufaa kupinga adhabu hiyo akiegemea sababu tatu kuu kwamba Jaji Mahimbali alikosea kisheria na kimantiki alipomtia hatiani na kumuhukumu adhabu ya kifo, Mahakama ya rufani imezitupa sababu hizo za rufaa.
Jopo la majaji watatu walirejea maelezo yake mwenyewe, akisimulia mwanzo mwisho wa nini kilitokea walipokuwa shambani na mkewe na kurejea alivyojibu kortini kuwa “Ni kweli nilimuua (mke wangu) lakini bila ubaya wowote”.
Majaji hao walirejea utetezi wake alioutoa kortini ambako alibadili kile alichokuwa amewaambia Polisi wakati anaandika maelezo yake ya onyo akisema:-
“Wakati napalilia nikamwambia mke wangu, jana ulinitelekeza na kondomu zangu na ninazo hapa mfukoni. Akaniambia tupalilie tukifikisha eneo tulilopanga kupalilia tunaenda kufanya mapenzi leo usiwe na wasiwasi mume wangu”
“Tulipomaliza kulima tukaingia kwenye vichaka watu wasituone. Akavua chupi yote akabaki na gauni la juu. Katandika Khanga yake na mimi nikavua suruali yote ila pensi ya ndani sikuvua yote, nikavaa kondomu nikafanya naye tendo moja”
“Nilivaa kondomu nyingine ili niendelee kufanya mapenzi ndipo mke wangu alikataa. Nilipata hasira ambazo sikufahamu zimetokea wapi. Nikawaza ameuza vitu, nimemtumia pesa kwa roho safi leo ananinyanyasa kwa kiasi hiki.”
“Ndipo nilichukua kisu na kumkamata mikono yake yote nikambana koo lake na kulegea kabisa. Alipolegea ndipo nilichukua kisu na kumchinja kabisa shingoni na kufa muda si mrefu. Nilipoona nimeua nikachukua kisu nikajikata korodani kwa lengo la kujiua lakini sikufanikiwa”, mwisho wa kunukuu maelezo yake.
Ni kutokana na maelezo hayo, jopo hilo lilisema Jaji Mahimbali aliona mrufani alimuua mkewe kwa kudhamiria hasa ikizingatiwa aina ya kisu alichotumia, nguvu aliyotumia, mapigo aliyopiga na maeneo ambayo alisababisha majeraha.
Majaji hao walisema baada ya kupitia ushahidi ulioko jaladani kwa ujumla wake, hawana mashaka kwamba Jaji Mahimbali alichambua na kufanyia tathmini ushahidi huo kwa umakini na alikuwa sahihi kumtia hatiani kwa mauaji.