Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imeridhia maombi ya mawakili wa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, ya kuwasilisha kiapo cha ziada katika shauri la maombi yanayohusu madai ya kutekwa kwake.
Mahakama hiyo imeridhia maombi hayo yaliyowasilishwa leo, Alhamisi, Oktoba 9, 2025 na jopo la mawakili wa Polepole linaloongozwa na Peter Kibatala, kwenye shauri la maombi ya amri ya mahakama ya kumfikisha Polepole mahakamani.
Shauri hilo namba 24514/2025 linalosikilizwa na Jaji Mfawidhi Salma Maghimbi, lilifunguliwa na Kibatala kwa niaba ya Polepole, Oktoba 7, 2025, chini ya hati ya dharura sana, dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), na wenzake.
Wajibu maombi wengine ni Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZCO) na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZPC), mjibu maombi wa pili mpaka wa tano mtawalia.
Shauri hilo limetajwa leo kwa mara ya kwanza kwa ajili ya maelekezo maalumu, lakini ni mjibu maombi wa pili pekee, DPP, aliyefika mahakamani akiwakilishwa na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Faraji Nguka (kiongozi wa jopo), Debora Mushi, Edith Mauya na Wakili wa Serikali Tumaini Mafuru.

Pamoja na mambo mengine, mawakili wa Polepole wameomba kuwasilisha kiapo cha ziada kwa maelezo kuwa baada ya kufungua shahidi hilo juzi, jana na leo wamepata taarifa mpya.
Pia, wameomba mahakama iridhie shauri hilo kusikilizwa upande mmoja na kuamuru mwombaji, Polepole, afikishwe mahakamani akisubiri uamuzi ya maombi yatakayozisikiliza pande zote.
Pia ameomba shauri hilo lisikilizwe upande mmoja dhidi ya wajibu maombi ambao hawakufika mahakamani, licha ya kwamba walipokea wito wa Mahakama.
Mahakama katika uamuzi wake imekubaliana na maombi ya kuwasilisha kiapo cha ziada huku ikitoa amri nne za maelekezo, kuhusu usikilizwaji wa shauri hilo.
Maelekezo hayo ni mwombaji kuwasilisha mahakamani kiapo cha ziada kesho, Ijumaa, Oktoba 10, 2025, na mjibu maombi wa pili awasilishe kiapo kinzani kujibu maombi hayo, kabla ya Jumanne, Oktoba 14, 2025 saa 6:00 usiku.

Pia, jaji Maghimbi ameelekeza kuwa kutokana na amri ya kwanza ya mwombaji kuwasilisha kiapo cha ziada, hawezi kulitolea uamuzi ombi la pili la shauri kusikilizwa upande mmoja mpaka kiapo hicho cha ziada kitakapowasilishwa.
Vilevile, amelelekeza kuwa shauri hilo litasikilizwa maombi ya pande zote Jumatano, Oktoba 15, 2025 saa 3:30 asubuhi.
Kuhusu wajibu maombi ambao hawakufika mahakamani, amesema wamepoteza haki ya moja kwa moja ya kuwasilisha kiapo kinzani kujibu maombi hayo.
Badala yake, Jaji Maghimbi ameamuru kuwa mjibu maombi ambaye miongoni mwao atahitaji kuwasilisha kiapo kinzani, atawajibika kwanza kuomba kibali cha mahakama.
Awali, Wakili Nguka licha ya kujitambulisha kuwa anamwakilisha DPP, pia ameieleza mahakama kuwa anashikilia mikoba ya mjibu maombi wa tatu, AG, ambaye pamoja na wajibu maombi wengine hawakufika mahakamani wala kutuma wawakilishi wao.
Amesema licha ya DPP kupelekewa hati ya wito wa kufika mahakamani jana, AG hakuwa amepelekewa wito huo.

Hata hivyo, Kibatala akisaidina na mawakili Faraji Mangula, Alphonce Nachipiangu, Deogratius Mahinyila na Grolia Ulomi, wameieleza mahakama kuwa wajibu maombi wote, akiwemo AG, walipelekewa wito huo jana na kwamba wote walisaini na ushahidi uko katika mfumo wa mahakamani.
“Kwa maoni yetu, wote hawa wamekuwa ‘served’ (wamepewa hati za wito), hivyo tunaomba mahakama itoe maelekezo kwa hao ambao hawakufika,” amesema Kibatala.
Hivyo, wameomba amri ya mahakama kuendelea na usikilizwaji wa shauri hilo upande mmoja bila kuwepo wajibu maombi ambao hawakufika mahakamani, kwa kuzingatia kuwa maombi hayo yamefunguliwa chini ya hati ya dharura.
Pia, Wakili Kibatala amesema kuwa DPP hawezi kumwakilisha AG na kwamba iwekwe kwenye kumbukumbu kuwa AG pia hajafika mahakamani.
Katika hati hiyo ya dharura iliyothibitishwa na Kibatala kuunga mkono maombi hayo, mwombaji anaeleza kuwa tangu Oktoba 6, 2025, Polepole aliripotiwa kutekwa na watu wanaodhaniwa ni maofisa wa Jeshi la Polisi waliovamia nyumbani kwake Ununio, Wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.
Pia, Kibatala anadai kuwa mpaka sasa hajashtakiwa kwa kosa lolote la jinai katika mahakama yoyote ya kisheria na kwamba inaaminika kuwa amewekwa kizuizini na wajibu maombi mahali kusikojulikana.
”Hivyo, haki zake za kikatiba zimekiukwa bila sababu za msingi. Ustawi wa mwombaji unahitaji uangalizi na uingiliaji wa haraka, ikiwemo kujua hali ya maisha yake,” amesema Wakili Kibatala.
Kuitia hati hiyo, wanaomba kesi isikilizwe upande mmoja na Mahakama iamuru Polepole afikishwe mahakamani akisubiri uamuzi wa maombi hayo kusikilizwa pande zote.
Pia wanaomba mahakama iwaelekeze wajibu maombi wamwachie mwombaji (Polepole) kwa dhamana au wamfikishe katika Mahakama ya kisheria na kumshtaki kwa mujibu wa sheria.
Kibatala anaeleza kuwa Polepole ni raia wa Tanzania ambaye ameitumikia nchi yake katika nafasi mbalimbali ikiwemo Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Cuba na nchi nyingine za Kilatini.
Pia, anaeleza kuwa katikati ya mwaka huu, Polepole kwa hiari yake alijiuzulu wadhifa huo wa ubalozi huku akieleza sababu mbalimbali zikiwemo kutokuridhika na namna mambo yanavyoendeshwa ndani ya Serikali na nchini Tanzania.
Wakili Kibatala anaeleza kuwa katika taarifa zake ambazo amekuwa akizitoa mara kwa mara, Polepole amekuwa akilalamika kuwa usalama wake uko hatarini kutokana na vitisho ambavyo amekuwa akivipokea kutoka kwa watu wasiojulikana kutokana na msimamo wake katika masuala mbalimbali.
Hivyo, anadai kuwa wakati fulani alfajiri ya Oktoba 6, 2025, wavamizi wasiojulikana walivamia na kuvunja makazi yake ya muda, Ununio kijijini Dar es Salaam, ambapo walimteka na kumpeleka mahali kusikojulikana.

“Haya yamethibitishwa kwa umma na kaka wa mwombaji (Polepole), Godfrey na Agustino Polepole, kama ilivyothibitishwa katika taarifa za vyombo vya habari vya ndani,” amesema Wakili Kibatala katika kiapo hicho.
Wakili Kibatala anaeleza zaidi kuwa mjibu maombi wa tano (ZPC – Jumanne Muliro) amenukuliwa katika taarifa hizo za vyombo hivyo vya habari akitoa taarifa za kupuuza tuhuma hizo nzito za utekwaji wake.

Amesisitiza kuwa mpaka wakati anaapa kiapo hicho, Polepole hajulikani mahali alipo na hakuna hata mmoja kati ya wajibu maombi ambaye ametoa mrejesho wowote kuhusu alipo, hali yake ya ustawi, na hadhi yake ya kisheria; jambo linaloongeza kiwango cha wasiwasi nchini.
“Nina sababu za kuamini kwamba wajibu maombi, na hasa mjibu maombi wa tano ZPC, ana ufahamu na yuko na mamlaka ya kumshikilia mwombaji,” amesema Wakili Kibatala.