Makusanyo TRA yaibua mjadala, wachumi wataka jicho la ziada

Dar es Salaam. Mafanikio ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kuvuka malengo ya makusanyo kwa miaka miwili mfululizo yamechochea mjadala mpya miongoni mwa wachumi na wananchi kuhusu ongezeko hilo linavyoakisi kuboresha maisha ya kawaida ya wananchi.

Wataalamu wa uchumi wanasema kuwa mafanikio haya yanahitaji kuangaliwa kwa jicho la kiuchumi na kijamii, hasa katika uwiano wake na mabadiliko halisi ya maisha ya watu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Tobias Swai amesema kuwa mfumo wa fedha unajengwa katika makundi matatu yanayomiliki uchumi wa nchi: serikali, wafanyabiashara na jamii.

 Serikali, anasema, hupata fedha kutokana na kodi na mikopo, ambapo TRA ni wakala wa ukusanyaji wa kodi na huwasilisha fedha hizo serikalini kupitia Benki Kuu (BoT).

“Makusanyo ya TRA kupanda haimaanishi kuwa mahitaji ya wananchi yamezidiwa; bali ni makubwa zaidi ya matarajio. Hivyo huwezi kuona mabadiliko ya moja kwa moja katika maisha ya wananchi wa kawaida kutokana na ongezeko hilo,” amesema Dk Swai, akibainisha kuwa ongezeko hilo linaakisi zaidi ufanisi wa taasisi, siyo lazima ufanisi wa maisha.

Ameeleza kuwa kuimarika kwa makusanyo kunaweza kuwa kumechangiwa na ongezeko la walipa kodi, kuongezeka kwa idadi ya watu na kuimarika kwa mifumo ya ukusanyaji, lakini bado athari chanya kwa maisha ya watu zinategemea namna serikali inavyotumia fedha hizo.

Kwa upande wake, Profesa Abel Kinyondo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amesema kuwa pamoja na mafanikio ya TRA, serikali inapaswa kuhakikisha mapato hayo yanatafsiriwa kwa vitendo katika ustawi wa wananchi kupitia utawala bora, uwazi na ushirikishwaji wa jamii.

“Kitu kikubwa ni utawala bora. TRA imeonesha uwajibikaji katika ukusanyaji, lakini jukumu kubwa sasa liko kwa serikali kuhakikisha ufanisi huo unahamia kwenye matumizi ya fedha hizo. Bila ushirikishwaji wa jamii, wananchi hawataona mchango wa makusanyo hayo hata kama miradi mingi itatekelezwa,” amesema Profesa Kinyondo.

Ameongeza kuwa ukosefu wa ushirikiano kati ya serikali na wananchi katika kupanga matumizi ya mapato unaweza kuzalisha hali ya wananchi kutoona matokeo ya kodi wanazochangia.

“Bila muunganiko wa mtumiaji wa makusanyo na wananchi wa kawaida, jamii itabaki haioni matokeo, hata kama takwimu zinaonesha mapato kupanda,” amesisitiza.

Kwa mujibu wa takwimu za TRA na Wizara ya Fedha, katika mwaka wa fedha 2024/2025 mamlaka hiyo ilikusanya Sh32.26 trilioni, sawa na asilimia 103 ya lengo la Sh31.5 trilioni, ongezeko la asilimia 16.7 ukilinganisha na mwaka uliopita.

Katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26 (Julai–Septemba 2025), TRA imekusanya Sh8.97 trilioni, sawa na asilimia 106.3 ya lengo la Sh8.44 trilioni, ikiwa ni ukuaji wa asilimia 15.1 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Mafanikio haya yamehusishwa na kuimarika kwa mifumo ya kidijitali ya ukusanyaji, matumizi ya Electronic Fiscal Devices (EFDs), malipo ya kielektroniki na ufuatiliaji wa moja kwa moja wa taarifa za biashara. Mabadiliko haya yameongeza uwazi, kupunguza upotevu na kuongeza uwajibikaji wa walipakodi wakubwa na wadogo.
Hata hivyo, licha ya mafanikio hayo, bado kuna maswali kuhusu uhusiano wake na gharama za maisha. Bei za bidhaa na huduma kama chakula, mafuta na usafiri zimeendelea kupanda, hali inayofanya baadhi ya wananchi kutoona unafuu unaolingana na mafanikio ya ukusanyaji wa mapato.
Serikali, kupitia Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba, imekuwa ikisisitiza kuwa makusanyo hayo ni msingi wa maendeleo ya kweli na kwamba kila senti inayokusanywa inaelekezwa kuboresha maisha ya wananchi kupitia miradi ya maendeleo.
Wachumi wanasema ili mafanikio haya ya kifedha yaende sambamba na ustawi wa jamii, serikali inapaswa kuhakikisha uwazi na ushirikishwaji katika upangaji na utekelezaji wa bajeti, ili wananchi wawe sehemu ya kuona matokeo ya kodi wanazolipa.