Arusha. Mgombea Ubunge wa CCM Jimbo la Ngorongoro, Yanick Ndoinyo ameahidi kusimama imara kutetea maslahi ya wananchi wa jimbo hilo na kuhakikisha kila sauti ya mkazi wa Ngorongoro inafikishwa serikalini bila kupotoshwa.
Ndoinyo amesema jukumu kubwa la wananchi wa Ngorongoro ni kuhakikisha CCM inapata kura za kutosha ili aingie madarakani kusaidia kuendeleza kasi ya maendeleo inayoonekana chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Ndoinyo ameyasema hayo leo Oktoba 9, 2025 katika kata ya Ngorongoro ikiwa ni muendelezo wa kampeni za kumuombea kura Rais Samia na kuomba ridhaa ya kupigiwa kura na wananchi hao katika uchaguzi unaotarajia kufanyika octoba 29 kote nchini.
Mgombea Ubunge wa CCM Jimbo la Ngorongoro Yannick Ndoinyo akizungumza kwenye mkutano wa kampeni katika kata ya Ngorongoro leo Octoba 9,2025
“Niwaambie wananchi wa Ngorongoro, wote tuna jukumu la kupigania chama chetu kupata ushindi mkubwa na kwa sauti moja tuseme hatutakubaliani na mtu yeyote atakayeharibu mchakato wa kura,” amesema na kuongeza.
“Mimi nawaahidi kuwatetea na kufikisha kila ujumbe wenu kwa shida na raha kwa serikali na kushirikiana nao kwa mshikamano bila migongano au malumbano, ili kusaidia kero zenu kutatuliwa lakini kiurahisisha miradi ya maendeleo kuletwa na kutekelezwa kwa urahisi,” amesema Ndoinyo.
Ameongeza kuwa CCM haitakubali kuendekeza siasa za majungu, bali itaendelea kusimamia ukweli na masuala ya msingi yanayohusu maisha ya wananchi.
Aidha, amesisitiza kuwa kila mwananchi, wakiwemo wazee na watu wasiojiweza, atawezeshwa kushiriki ipasavyo katika uchaguzi huo kupitia usafiri wa magari na pikipiki walizoandaa ili kuhakikisha wanapata kura za kutosha.
Katika mikutano hiyo, viongozi wa CCM na Serikali katika kata 11 zilizopo ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) walimpongeza na kumshukuru Rais Samia kwa kurejesha maeneo ya vijiji na mipaka iliyokuwa imefutwa awali, hatua waliyoeleza kuwa imeleta matumaini mapya kwa wananchi.
“Rais Samia ameonyesha uongozi wa kipekee unaojali maisha ya wananchi wa Ngorongoro kwa kuleta usawa kati ya uhifadhi na ustawi wa jamii, jambo ambalo halijawahi kufanyika kwa muda mrefu,” amesema Laizer Joseph mwananchi wa eneo hilo.

Amesema hatua hiyo imeimarisha mshikamano kati ya wananchi na mamlaka ya hifadhi, huku miradi ya maendeleo ikiendelea kutekelezwa kwa kasi katika sekta za elimu, maji na afya.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Olbalbal, James Saringe amesema wameweka mikakati madhubuti kuhakikisha kila kaya inashiriki katika uchaguzi mkuu ujao.
“Tumeanza na kampeni za majukwaani lakini viongozi wa mitaa wanafanya kampeni ya kaya kwa kaya kuhakikisha wanawaeleza umuhimu wa kupiga kura, lengo ni kuhakikisha hakuna mtu anaachwa nyumba”
Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha CCM inarudi madarakani kumalizia miradi ya maendeleo iliyobaki na kuleta maendeleo mapya waliyowasilisha kwenye kero zao.