Misri imejihakikishia tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya leo kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Djibouti katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Larbi Zaouli, Casablanca Morocco.
Mabao ya Ibrahim Adel na Mohamed Salah aliyepachika mawili yameifanya Misri kuwa timu ya tatu ya taifa ya Afrika kufuzu Kombe la Dunia 2026 baada ya Morocco na Tunisia.
Licha ya Burkina Faso kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Sierra Leone, Misri imefikisha pointi 23 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine kwenye kundi A la mashindano ya kuwania kufuzu kupitia kanda ya Afrika.
Kwenye Uwanja wa Ben M’Hamed El Abd, Jadida, Morocco, Ghana imeibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Matokeo hayo yameifanya Ghana ihitaji angalau pointi moja tu katika mechi yake ya mwisho nyumbani dhidi ya Comoro, Oktoba 12, 2025 ili itinge Kombe la Dunia.
Kwa Ghana sasa inaongoza msimamo wa kundi I ikiwa na pointi 22 huku Madagascar iliyoifunga Comoro kwa bao 1-0 ikishika nafasi ya pili na pointi zake 19.

Cape Verde imelazimika kutoka nyuma baada ya kutanguliwa kwa mabao matatu na Libya na kutoka sare ya mabao 3-3 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Tripoli, Libya.
Sare hiyo imeifanya Cape Verde kuendelea kuongoza msimamo wa kundi D ikifikisha pointi 20 na sasa inahitaji ushindi wa nyumbani dhidi ya Eswatini, Oktoba 13, 2025 ili iandike historia ya kufuzu kwa mara ya kwanza Fainali za Kombe la Dunia.