Dar es Salaam. Hatua ya Marekani kuweka sharti la dhamana ya viza kwa raia wa Tanzania wanaoingia nchini humo imezua mjadala miongoni mwa wachambuzi wa masuala ya uchumi na diplomasia, wakionya kuwa masharti hayo yanaweza kuleta athari mbalimbali.
Wameeleza kuwa hatua zilizoanza kuchukuliwa na Serikali zina umuhimu wa kipekee katika kuendeleza uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo, uliodumu kwa zaidi ya miongo minne.
Maoni hayo yanakuja moja tangu Marekani ilipotangaza masharti mapya ya viza kwa raia wa mataifa saba— Tanzania, Mauritania, Mali, Sao Tome and Príncipe, Gambia, Malawi na Zambia, ambapo wasafiri wa biashara na utalii watalazimika kufuata utaratibu mpya wa kuingia nchini humo.
Taarifa ya Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, ambayo imewekwa kwenye tovuti rasmi ya ubalozi huo, imebainisha kuwa kuanzia Oktoba 23, 2025, Tanzania itawekwa katika programu za majaribio ya dhamana ya viza.
Kiwango cha dhamana kilichotajwa na Marekani kwa raia wa mataifa hayo ni Dola 5,000 za Marekani (Sh12.3 milioni), 10,000 (Sh24.5 milioni) au 15,000 (Sh36.7 milioni). Kiwango hicho cha dhamana kitaamuliwa wakati wa mahojiano ya maombi ya viza.
Hata hivyo, jana Oktoba 8, 2025, Serikali kupitia kwa msemaji wake, Gerson Msigwa, ilitoa taarifa kwa umma iliyobainisha kuhusu juhudi za Serikali kuanzisha majadiliano ya kidiplomasia na Marekani katika kulishughulikia suala hilo.
Kwa mujibu wa Msigwa, suluhu ya kidiplomasia inayotafutwa na Serikali ni yenye kuzingatia usawa, heshima na maslahi ya pande zote mbili, kwa kuzingatia uhusiano mzuri wa nchi hizo mbili uliodumu kwa zaidi ya miongo minne.
“Serikali inapenda kuuhakikishia umma kwamba itaendelea na majadiliano hayo na Serikali ya Marekani,” alibainisha Msigwa katika taarifa yake.
Wachumi na wanadiplomasia
Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Oscar Mkude, amesema sharti hilo la Marekani dhidi ya raia wa Tanzania ni kutokana na ajenda yake ya Marekani Kwanza pamoja na kukabiliana na wahamiaji.
“Dhamana ya viza ina athari, lakini si sana kwa sababu hatufanyi biashara nyingi na Marekani, lakini kuna misafara hii ambayo viongozi wetu wanaambatana nayo wanapokwenda ziara, hiyo itawaathiri,” amesema.
Amesema wapo baadhi ya Watanzania huenda Marekani kwa ajili ya biashara, kusoma na kusalimia ndugu zao, ambao hawataweza kumudu gharama iliyowekwa.
Sababu ya kushindwa kumudu, Mkude amesema, ni aina ya vipato ambavyo Watanzania hupata kutokana na kazi za vibarua, jambo ambalo ni gumu kufikia kiwango hicho cha kuingia Marekani.
Mkude ametafsiri hatua hiyo ya Marekani kama kuiweka Tanzania katika taswira mbaya kwa mataifa mengine, ambayo huenda nayo yakaanza kuiangalia kwa jicho la pekee na kuja na utaratibu kama huo kwa Tanzania.
“Hatua ambayo Tanzania imesema itachukua ni jambo zuri, lakini tunaweza kuwa na vitambulisho vya kidijitali (Digital ID) kudhibiti watu wetu. Hii imetokea kwa sababu Watanzania wanaokwenda Marekani hawarudi, wanakwenda kupotelea huko. Kwa hiyo wakaona tatizo letu kwenye uhamiaji, wakaja na utaratibu wao,” amesema.
Kwa upande wake, mwanadiplomasia Profesa Abdallah Safari amesema haoni kama Tanzania itaathirika kutokana na masharti hayo, kwani taifa lenye nguvu sasa kiuchumi duniani ni China na si Marekani.
Amesema endapo China ingeiwekea masharti hayo Tanzania, athari ingeonekana kubwa, akihimiza mataifa ya Afrika kuondoa viza kwa watu baina ya mataifa hayo.
“Ukiangalia mataifa ambayo yanatusaidia kwa kiwango kikubwa, utaiona China na India. Haya masharti ya Marekani hayawezi kutuathiri. Sisi Afrika tunapaswa kuimarisha ushirikiano wetu, haya mataifa ya nje tusiyategemee sana,” amesema.
Profesa wa uchumi, Abel Kinyondo, amesema masharti hayo yanaonesha namna ambavyo Tanzania si rafiki wa karibu na Marekani.
“Rais wa Marekani, Donald Trump, kwa sasa anaangalia maslahi ya ndani ya nchi yake, kwa hiyo anaangalia ni wapi panamsaidia na wapi hanufaiki nako. Alishaweka masharti hadi ya bidhaa kwa kupandisha ushuru. Masharti haya sasa ni kikwazo kwa watu kwenda kule, kwa hiyo Serikali kuonesha nia ya mazungumzo ni jambo jema,” amesema.
Profesa Kinyondo ameongeza kuwa Tanzania ilijipambanua kama taifa lisilofungamana na upande wowote, lakini kadiri siku zinavyokwenda inaonekana inafungamana na mataifa ya mashariki kama China na India, na huenda hiyo ni sababu mojawapo ya ujio wa masharti hayo.
“Hatupaswi kufungamana na upande wowote ili tupate faida, kwa sababu kwa sasa wanafunzi wanaokwenda kusoma kule na wafanyabiashara wataathirika. Marekani ndiyo mama wa demokrasia kwa mataifa mengi duniani. Taifa lolote linalotaka kuendelea lazima liwe karibu na Marekani.
“Hata China, watu wake walikwenda Marekani, wakajifunza na kurudi nyumbani na ujuzi wao, wakaanza kulijenga taifa lao, kwa hiyo hatuwezi kuishi kama kisiwa,” amesema.
Taarifa ya Ubalozi wa Marekani
Taarifa ya Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, iliyowekwa kwenye tovuti rasmi ya ubalozi huo, imebainisha kuwa kuanzia Oktoba 23, 2025, Tanzania itawekwa katika programu za majaribio ya dhamana ya viza.
“Waombaji wote wa viza wanaotaka kwenda Marekani kwa shughuli za biashara na utalii watatakiwa kuweka dhamana kabla ya kutolewa kwao.
“Serikali ya Marekani itarudisha kwa muombaji kiwango chote cha dhamana iliyowekwa pale atakapokuwa amekidhi masharti yote ya viza yake na kuondoka Marekani kabla ya kuisha kwa muda wa viza hiyo,” taarifa hiyo imeeleza.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mwombaji atatakiwa kujaza fomu ya Idara ya Usalama wa Ndani (Department of Homeland Security) yenye namba I-352, na lazima akubaliane na masharti ya dhamana hiyo kupitia malipo atakayopaswa kufanya kwa njia ya mtandao ya Idara ya Hazina ya Marekani.
“Sharti hilo litatumika bila kujali sehemu au nchi ambayo mwombaji anaomba viza,” taarifa hiyo imefafanua.
Marekani imefafanua masharti kwa wahusika kuwa, waombaji wote wa viza ambao wameweka dhamana ya viza wanapaswa kuingia na kutoka Marekani kupitia vituo maalumu vya kuingia.
Maeneo yaliyoainishwa kuwa ndiko wahusika watapita au kutumia ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Boston Logan (BOS), Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa John F. Kennedy (JFK) na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Washington Dulles (IAD).
Kutozingatia masharti hayo kutasababisha mhusika kukataliwa kuingia nchini humo au kuondoka bila kurekodiwa ipasavyo.